Jumanne, 24 Novemba 2026

JAJI NKWABI AKABIDHI PIKIPIKI MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO KIGOMA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama - Kigoma

Katika mwendelezo wa kuboresha utoaji wa huduma za kimahakama na kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata haki mapema ipasavyo bila vikwazo vya miundombinu, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo Kigoma Mhe. John Nkwabi amewakabidhi Mahakimu Pikipiki sita (6) zitakazotumika Mahakama za Mwanzo ili kurahisisha usafiri wa Watumishi hao kufika katika Vituo vya Mahakama na maeneo ya pembezoni yanayotembelewa.

Zoezi la makabidhiano ya Pikipiki hizo lilifanyika tarehe 20 Novemba, 2026 ambapo Mhe. Nkwabi alisema, “mnaokabidhiwa Vyombo hivi vya Usafiri ni rai yetu mvitunze vema ili viweze kudumu katika kusaidia safari zenu za kutoa haki kwa haraka na mapema ipasavyo katika vituo vyenu.”

Akizungumza baada ya kupokea Pikipiki hizo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kalinzi, Mhe. Mussa Nzige, alisema kuwa, vyombo hivyo vinaenda kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri katika vituo wanavyotembelea sambamba na maono mapana ya Uongozi wa Mahakama nchini ya kujenga mazingira rafiki ya utendaji kazi, kuongeza ufanisi na kuharakisha usikilizaji wa mashauri. 

“Kupatikana kwa usafiri huu utatuwawezesha sisi Mahakimu kufanya ziara za mara kwa mara kwenye vituo vya mbali, kusikiliza mashauri karibu na wananchi na hivyo kupunguza gharama na muda uliokuwa ukipotea kwa wananchi kusafiri masafa marefu kufuata huduma za kisheria,” alisema Mhe. Nzinge.

Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa amewasihi Mahakimu hao kutembelea Pikipiki hizo kwa umakini huku wakizingatia sheria za usalama barabarani wanapotembelea Mahakama ili kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo yote anayohudumu kwa ratiba maalum watakayojipangia.

Zoezi la kukabidhi Pikipiki hizo limeshududiwa na Viongozi, Watumishi wa Kada mbalimbali pamoja na Wakuu wa Vitengo na Mtendaji wa Mahakama Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo. 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu sita wa Mahakama baada ya kuwakabidhi Pikipiki mara baada ya tukio hilo lililofanyika tarehe 20 Novemba, 2026 Mahakama Kuu Kigoma. 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi akisema neno kabla ya kukabidhi Pikipiki na kadi zake kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi (kulia) akimkabidhi Kadi ya Pikipiki Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kasanda, Mhe. Jonas Kilimba.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi akifurahia jambo alipokuwa akimkabidhi Kadi ya Pikipiki Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kalinzi, Mhe. Mussa Nzige.


Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi akimkabidhi Kadi ya Pikipiki Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji,  Mhe. Kalimunda Yagalila tayari kwenda kuhudumia wananchi

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akimkabidhi Kadi ya Pikipiki Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kifura, Mhe. Shadrack Constatine tayari kwenda kuhudumia wananchi.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni