Jumamosi, 14 Novemba 2026

JAJI RWIZILE AFANYA UKAGUZI MAHAKAMA ZA MWANZO KIGOMA

  •  Aonesha kufurahishwa na historia ya Mahakama ya Mwanzo Mgunzu
  • Aelekeza kufanyika kwa maboresho ya haraka katika Miundombinu ya Mahakama hizo

Na AIDAN ROBERT, Mahakama - Kigoma

Katika jitihada za kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo, hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile alifanya ziara ya kikazi katika Mahakama za Mwanzo mkoani Kigoma kwa lengo la kukagua hali halisi ya miundombinu ya Mahakama hizo.

Ziara hiyo ya ukaguzi katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo za vijijini, Jaji Rwizile alijionea miundombinu mbalimbali ikiwemo majengo ya zamani yanayohitaji ukarabati mkubwa, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na uhaba wa nyumba za kuishi kwa ajili ya watumishi wa Mahakama katika maeneo ya pembezoni.

Mhe. Rwizile alifurahi alipofika katika Mahakama ya Mwanzo Mgunzu au Nyerere iliyopo katika Kata ya Mgunzu Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma, ambapo kwa historia ya mwaka 1950, ilijengwa na Mkoloni Mjerumani ambapo mashauri ya wakati huo yaliamriwa hapo, hata hivyo 1974 Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius Kambarage Nyerere alifika katika Kijiji hicho cha Mgunzu na alilala hapo kwa muda wa siku tatu akiwa katika usimamizi wa ujenzi wa nyumba za Maofisa wa nyumba kumi wakiwa Walinzi wa mipaka ya Tanzania na Burundi…

Akiwa katika eneo hilo Mzee Richard Mabhago, wazazi wake ndio alitoa eneo lao la shamba kwa Serikali ya kipindi hicho ili ijengwe Mahakama hiyo,  ilijengwa na mpaka leo Mahakama ya Mwanzo Mgunzu ambayo kwa sasa ni chakavu imehifadhiwa kwa ajili ukarabati na kutunza historia ya eneo hilo muhimu katika Mkoa wa Kigoma na Mahakama ya Tanzania.

Licha ya changamoto hizo, wananchi wa maeneo ya Mahakama hizo za Mwanzo walionesha furaha yao kuona Viongozi wakubwa wa Mahakama wakishuka hadi ngazi ya chini ili kujionea kero zinazowakabili badala ya kusubiri taarifa tu.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama mojawapo  mara baada ya ukaguzi huo, Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza na kutoa wito kwa Mtendaji wa Mahakama kuweka mipango ya ukarabati wa baadhi ya Mahakama zinazohitaji ukarabati mdogo ili kuharakisha upatikanaji wa huduma za kimahakama katika  majengo hayo yaliyochakaa ili yaendane na hadhi ya utoaji haki na kulinda nyaraka muhimu za kimahakama na watumishi wanaohudumu katika Mahakama hizo.

Aliwakumbusha Watumishi wa Mahakama za Mwanzo kuzingatia weledi, maadili na kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa mlundikano wa mashauri na kupunguza kero kwa wananchi wanaotafuta haki.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka, aliridhia kwa moyo mkunjufu kupokea maagizo hayo ya ukarabati ambapo ameonesha nia ya dhati ya kusimamia utekelezaji wake ili kurejesha huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha miundombinu inaboreshwa bila kuchelewa katika baadhi ya Mahakama ambazo zinahitaji ukarabati mdogo ambao unaweza kufanyika kwa fedha za kuendeshea ofisi.

Ziara hiyo imetajwa kuwa chachu kubwa ya mabadiliko katika utendaji kazi wa Mahakama za Mwanzo mkoani Kigoma, huku ikitarajiwa kuleta suluhu ya kudumu kwa changamoto za miundombinu zilizoripotiwa ili wananchi wa vijijini waweze kupata haki katika mazingira rafiki na salama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitazama baadhi ya matangazo yaliyopo kwenye kuta za Mahakama ya Mwanzo Itaba iliyopo Wilaya Kibondo mara baada ya kuwasili mahakamani hapo hivi karibuni kwa lengo la ukaguzi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (wa kwanza kulia), Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka (wa pili kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maira Makonya (wa kwanza kushoto. Katikati ni Mzee maarufu, Bw. Richard Mabhago ambaye familia yake ilitoa eneo la shamba lao ili ijengwe Mahakama ya Mwanzo Mgunzu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kulia) akiwa pamoja na Viongozi wengine wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Itaba wilayani Kibondo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akiwa na Viongozi wengine wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Kifura wilayani Kibondo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile pamoja na Viongozi wengine wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Nyavyumbu iliyopo wilayani Kakonko.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile na Viongozi wengine wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Muhange wilayani Kakonko.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile na Viongozi wengine wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Makere wilayani Kasulu.

Wakiwa Mahakama ya Mwanzo Mabamba iliyopo Wilaya Kibondo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni