Na MARY GWERA, Mahakama-Mbeya
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George
Masaju ameyasihi Madhehebu ya Dini zikiwemo Dini za asili kama Machifu kuendelea
kuhimiza usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na umoja wa
kitaifa ili kuendelea kuchangia katika kuimarisha amani na
maendeleo ya nchi.
Mhe.
Masaju ameyasema hayo leo tarehe 20 Novemba, 2026 jijini Mbeya alipokuwa akifungua Kongamano la Kuliombea Taifa lililofanyika mkoani humo.
“Madhehebu ya dini yana mchango mkubwa sana katika ustawi wa Taifa. Na tunaposoma Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lengo la Serikali ni ustawi wa wananchi. Hakuwezi kuwa na ustawi wa wananchi kama Taifa halina amani. Taifa lolote lile, ndio maana kuna Taasisi za kiserikali, Serikali yenyewe inakuja kusimamia ustawi wa taifa, wa wananchi katika miundombinu yake mbalimbali. Na ndio maana madhehebu ya dini mnafanya vizuri sana, ili kukiwa na amani, watu waweze kufanya shughuli zao za kisiasa, za kijamii na kiuchumi kwa amani,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, Viongozi wa dini wa Madhehebu mbalimbali wakishindwa
kufundisha maadili ya Mwenyezi Mungu kupitia vitabu kama Biblia, Quran na Machifu
kwa mila zao wanapoteza umuhimu wa kuwepo kwao na hivyo, nafasi hizo
zitachukuliwa na watu wengine.
Aidha, Mhe. Masaju amerejea, Ibara ya 19(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu madhehebu ya dini ambapo hifadhi ya haki zilizotajwa katika ibara hiyo itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika jamii ya kidemokrasia. "Pamoja na uhuru waliopewa, wamepewa sharti la kuzingatia sheria. Amesema, “mimi nikikuta Kiongozi wa Dini anafundisha au kuhubiri chuki, nadhani huyo haijui vizuri Biblia. Kwa sababu Mungu ni upendo. Sio ‘abstract’ kwa maana ya tabia yake,” amesema.
“Niwakumbushe kitu ambacho Mwalimu Nyerere alisema ilikuwa mwaka 1988 pale Arusha akihutubia kwenye mkutano wa ALAT ‘Mamlaka ya Serikali za Mitaa, aliwaambia Serikali ni Sheria. Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila sheria. Na sheria zikishatungwa lazima zifuatwe. Na ndio maana tuna kitu kinaitwa utawala wa sheria. Kila kitu mnavyokiona hapa kinatawaliwa na kuongozwa na sheria,” ameeleza.
Katika hotuba yake, Jaji Mkuu
Masaju amebainisha kuwa, amani ndiyo msingi wa uhai, ustawi na shughuli za
kijamii na kiuchumi za wananchi, akirejea vifungu mbalimbali vya maandiko
matakatifu, ikiwemo Mathayo 18:20, Mathayo 22:34 - 40, Luka 10:25 - 28, Mathayo
5:9, Mathayo 28:18 - 20 na Mwanzo 2.
Ameeleza kuwa, Viongozi wa Dini
wana jukumu kubwa la kuwaunganisha watu na Mungu pamoja na wanadamu wenzao
kupitia upendo na msamaha, huku akisisitiza kuwa, mahubiri ya chuki yanapingana
na asili ya Mungu ambayo ni upendo. Aliongeza kuwa wale wanaokaidi maadili na
kuvunja sheria ndio huletwa mahakamani ili kutendewa haki kwa mujibu wa Katiba,
Sheria za nchi na ushahidi unaowasilishwa.
Aidha, Jaji Mkuu amewapongeza
wananchi wa Mbeya kwa uzalendo, bidii ya kufanya kazi na kujitambua, pamoja na
kuwashukuru Viongozi wa Dini na Machifu akiwemo Chifu Mwashinga kwa mchango wao
katika maadili, umoja wa kitaifa na utunzaji wa mazingira.
Kadhalika, amewahimiza pia
Watanzania kuendelea kudumisha uhuru na umoja wa Taifa kwa mujibu wa Nembo ya Taifa,
akibainisha kuwa, Taifa ni watu wake na Serikali inatambua mchango wa maombi ya
viongozi wa dini katika kuombea amani ya nchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewapongeza Viongozi wa
Dini wa Mkoa wa Mbeya kwa kuandaa kongamano hilo na kusema kuwa, “na mimi
nimefarijika sana mlipoandaa kongamano hili mkanialika. Kwa sababu nyinyi
mnafanya kazi ya upatanisho. Mnatupatanisha na Mungu pale tulipokosea, ndio
maana hata maudhui ya ibada yetu hapa pamoja na kumuomba Mungu amani na haki na
upendo vitamalaki katika jamii yetu, tumeomba msamaha wa dhambi kwa rehema na
fadhili zake za milele.”
“Lakini kwa sababu mmenialika katika hili jambo jema, hivi
mimi ni nani kukataa? Kukataa jambo jema linaloimarisha amani, upendo na haki
katika jamii ya Muungano wa Tanzania. Kama ilivyo kaulimbiu yetu kwenye ile Kamati
ya amani na maridhiano ambayo ndio nimeanza nayo: "Dini mbalimbali,
upendo, haki na amani." Mungu ni Mungu wa haki, ni Mfalme wa haki, ni
Mfalme wa amani. Mungu ni upendo. Na haya yote yanatuunganisha pamoja ndio
maana leo hapa tuko madhehebu mbalimbali,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, anatambua Mbeya kama Mkoa una wananchi ambao
wanalipenda sana Taifa hili na rasilimali zake. Ni wazalendo na wapenda
maendeleo, wana hofu ya Mwenyezi Mungu lakini ni watu ambao wanapenda kufanya
kazi, wanawajibika na wanatambua kwamba kazi ni kipimo cha utu kama Ibara ya 25
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyotaka.
Akihusianisha ujumbe wa
kongamano hilo na misingi ya kitaifa, Jaji Mkuu Masaju amerejea; Ibara ya 8 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977): Lengo la Serikali ni ustawi
wa wananchi, jambo linalohitaji amani na utulivu, Ibara ya 19 ya Katiba: Uhuru
wa kuabudu na kutambuliwa kwa madhehebu ya dini, pamoja na sharti la kuzingatia
sheria, usalama, maadili, amani na umoja wa kitaifa.
Amerejea pia, Ibara ya 25 na
28 za Katiba: Wajibu wa kufanya kazi na wajibu wa kila mwananchi kuchangia
katika usalama na utawala wa sheria pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
inayoelekeza kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
Kadhalika, Mhe. Masaju amekumbusha juu ya umuhimu wa Watanzania
kujitambua, ambapo amesema moja ya sifa ya watu wa Mbeya wanajitambua. “Taifa
hili tunataka tubaki kuwa watu tunaojitambua. Tumepewa destiny kuishi
katika taifa letu hili. Libaki huru lakini lenye umoja,” amesema.
Katika Kongamano hilo lililohudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa
Serikali na Dini wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Sagini, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, Mkuu wa
Wilaya ya Mbeya, Maaskofu, Masheikh pamoja na Wananchi wapatao 6,000 lilipambwa
na Maombi kutoka Dini zote zilizokuwepo wakiwemo Wakristo, Waislamu pamoja na
Machifu huku msisitizo mkubwa uliotawala ukiwa ni kudumisha amani, upendo na
umoja wa nchi. Kadhalika kwaya mbalimbali zilitumbuiza katika siku hiyo muhimu
kwa Taifa la Tanzania.



























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni