Ijumaa, 27 Novemba 2026

TAWJA NJOMBE YAADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

·         Watoa elimu kwa Wanafunzi na Walimu wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo - Njombe

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama - Njombe

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Tawi la Njombe kimetoa elimu kuhusu kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia, hususan dhidi ya Wanawake na Watoto kwa wanafunzi na watumishi wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo kilichopo mkoani Njombe ikiwemo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.

Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 25 Novemba, 2026, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa aliwaeleza wanafunzi na watumishi umuhimu wa kutambua aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia, athari zake pamoja na wajibu wa kila mmoja katika kuzuia na kutoa taarifa za vitendo hivyo vinapotokea.

Mhe. Nongwa alieleza kuwa, ukatili wa kijinsia unaweza kujitokeza katika mazingira mbalimbali, ikiwemo familia, Taasisi za Elimu na hata kwenye mitandao ya kijamii. Alisisitiza faida za matumizi ya teknolojia ya mawasilano pamoja na kueleza changamoto zake ikiwemo, baadhi ya watu kutumia mitandao kurekodi, kusambaza au kuchapisha maudhui yanayodharirisha na kuathiri heshima ya wengine.

Alitoa wito kwa wanafunzi na watumishi kutumia teknolojia kwa uwajibikaji, kuepuka kurekodi au kusambaza maudhui yasiyofaa na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha madhara kwa wengine. Aidha, alieleza umuhimu wa kulinda taarifa binafsi, hususan za watoto, kwa kuzingatia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Akifafanua kuhusu sheria zinazohusiana na makosa ya mtandaoni, Mhe. Nongwa alieleza kuwa, Sheria ya Makosa ya Mtandao (the Cybercrimes Act) inaweka utaratibu wa kushughulikia makosa yanayofanyika kupitia mitandao ya mawasiliano, ikiwemo ukusanyaji wa ushahidi na utambuzi wa wahusika. Aliwahimiza wanafunzi kuwa waangalifu katika matumizi ya mitandao na kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili wa mtandaoni.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nongwa alizungumzia suala la rushwa ya ngono na kueleza kuwa, matumizi mabaya ya madaraka kwa lengo la kushawishi au kudai vitendo vya kingono ni kosa linaloweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Aliwaasa watumishi kutotumia nafasi zao kuwaweka wanafunzi katika mazingira ya unyanyasaji, huku wanafunzi wakihimizwa kutokubali kushawishiwa au kujihusisha na vitendo vya rushwa ya ngono, pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokumbana na vitendo hivyo.

Aidha, aliwakumbusha wanafunzi na watumishi kuwa jukumu la kulinda watoto ni la jamii nzima, na hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha watoto, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata ulinzi na haki zao bila ubaguzi.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo, alieleza kuwa, elimu hiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Kadhalika, alitambulisha pia Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2026, kuwa ni: “Tuungane Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa Imara Lenye Haki Na Usawa Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.”

Akichangia mada hiyo, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomol, aliyeambatana na Uongozi wa TAWJA kwa nafasi yake kama Mratibu wa Mafunzo Mahakama Kuu Njombe, alifafanua masuala mbalimbali ya kisheria yaliyoulizwa na wanafunzi, ikiwemo usambazaji wa maudhui ya faragha mtandaoni na rushwa ya ngono.

Akihitimisha zoezi hilo, Jaji Nongwa aliwasisitiza wanafunzi na watumishi kutokaa kimya wanapofanyiwa au kushuhudia ukatili, bali kutoa taarifa katika vyombo husika, ikiwemo Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Alieleza kuwa, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa familia, Taasisi za elimu, vyombo vya sheria na jamii kwa ujumla ili kujenga mazingira salama na yenye kuheshimu haki na utu wa kila mtu.

Awali, akikaribisha ugeni wa TAWJA walipotembelea chuoni hapo, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo, Bw. Octavian Chongolo, aliwatambulisha watumishi na kuelezea mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, yakiwemo Afya ya Wanyama, Kilimo, Maendeleo ya Jamii pamoja Ualimu.

Elimu hiyo ilitoa fursa kwa wanafunzi na watumishi kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, haki za watoto, matumizi ya teknolojia na hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (aliyesimama) akitoa elimu kwa Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo. Wengine katika picha wa pili kulia ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Matilda Kayombo, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Octavian Chongolo wakifuatilia kwa makini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa.

Sehemu ya Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo mkoani Njombe wakifuatilia kwa makini na utulivu elimu iliyokuwa ikitolewa na Viongozi wa TAWJA Tawi la Njombe walipofanya ziara Chuoni hapo tarehe 25 Novemba, 2026 kwa lengo la kutoa elimu kuhusu kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia, hususan dhidi ya Wanawake na Watoto. 


Mkuu wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo
, Bw. Octavian Chongolo (aliyesimama) akitambulisha Watumishi na kuelezea mafunzo yanayotolewa chuoni hapo. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Matilda Kayombo (aliyesimama) akiwa pamoja na Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola wakati wa ziara ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo.


Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola (aliyesimama upande wa kulia), akiwa pamoja na Viongozi wa TAWJA, akijibu maswali yaliyoulizwa na wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo Haghafilo. Walioketi kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Njombe, Mhe. Victoria Nongwa kushoto kwake ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Matilda Kayombo.

Mwanafunzi Gayson Mtitu, akiwa amesimama kuuliza swali kwa viongozi wa TAWJA kuhusu mada zilizokuwa zikitolewa, huku wanafunzi wenzake wakisikiliza kwa makini.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama - Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni