Na
Lydia Churi-Mahakama, Manyara
Mahakama ya Tanzania
imeshauriwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya namba
za simu zilizotolewa kwa ajili ya wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa
Mahakama pamoja na mapambano dhidi ya rushwa.
Akizungumza jana mjini
Babati mkoani Manyara, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani humo, Jacob
Swalle alisema upo umuhimu wa kuwaelimisha wananchi zaidi juu ya matumizi sahihi
ya simu hizo kwa kuwa wengi wao wanazitumia kwa kupiga badala ya kutuma ujumbe.
Alisema licha ya changamoto
za simu hizo, mabango yaliyosambazwa yenye namba hizo yamesaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza malalamiko kwa wale wanaotumia kwa usahihi.
Mtendaji wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Manyara, Jacob Swalle
Kuhusu utekelezaji wa
Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania, Mtendaji huyo alisema
wanajitahidi kutekeleza nguzo zote tatu ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Alisema hivi sasa nakala za hukumu zinatoka kwa wakati.
Alisema ili kujenga
taswira chanya kwa Mahakama, wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara na
watumishi ili kukumbushana majukumu yao ya kutekeleza Mpango Mkakati ikiwa ni
pamoja na umuhimu wa kuhudumia wateja vizuri na kufuata maadili
Kuhusu mikakati ya
kuondosha mashauri ya muda mrefu Mahakamani, Bwana Swalle alisema wamekuwa
wakifanya vikao na wadau pamoja na kuondoa changamoto zinazochelewesha kesi
kumalizika mahakamani. Aidha, wamekuwa wakiomba
Mahakimu kutoka Arusha kusaidia kumaliza kesi kwa haraka.
Mahakama ya Hakimu
Mkazi mkoa wa Manyara inakabiliwa na changamoto za upungufu mkubwa wa watumishi
kama Mahakimu, Makarani, wahudumu na walinzi. Mahakama hiyo hivi sasa ina hakimu
moja tu.
Mahakama ya Tanzania
ilianza kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za
Mahakama tangu mwaka 2015 kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili
Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kuhakikisha
wananchi wanapata haki kwa wakati.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Manyara likiwa katika hatua za mwisho
Jengo la Mahakama ya Wilaya
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Karatu lililomalizika hivi karibuni
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni