Na
Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania
ipo katika jitihada mbalimbali za kuhakikika kuwa inamaliza mlundikano wa mashauri ya Migogoro ya kazi ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya
karibu na Wadau wake ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Akifungua Warsha ya
siku tatu ya Wadau wa masuala ya Kazi kujadili juu ya Utatuzi na Usuluhishi wa
Migogoro ya Kazi mapema Mei 14, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi,
Mhe. Aisha Nyerere alisema lengo ni kuwa na uelewa wa pamoja jinsi ya kutatua migogoro
ya kazi.
“Tumewaita Wadau wetu
ambao tunafanya nao kazi kwa karibu ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya
utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya kazi ili wote twende pamoja katika kutatua
migogoro hiyo,” alisema Mhe. Jaji Nyerere.
Jaji Mfawidhi
aliendelea kusema kuwa kuna changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo katika
uondoshaji wa mashauri ya kazi mojawapo ikitokana na upande wa Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo kuna baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja upungufu wa rasilimali fedha,
rasilimali watu zinazopelekea kuchelewa kwa mashauri hayo.
Mbali na changamoto
hizo kwa upande wa CMA, Mhe. Jaji Nyerere alibainisha kuwa miongoni mwa sababu
zinazopelekea malalamiko kwa upande wa Mahakama ya Kazi ni kutokana pia na uchache wa
Majaji katika Divisheni hiyo.
Hata hivyo, Mhe. Jaji
Nyerere alisema kuwa ili kukabiliana na upungufu wa Majaji wa Divisheni hiyo,
Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia tamko lake la Aprili 30, 2018 ameelekeza kuwa
kila Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania atasikiliza mashauri ya masuala ya kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema
kuwa katika Warsha hiyo Wadau hao watafundishwa juu ya Sheria mbalimbali za
masuala ya kazi.
“Katika Warsha hii tutapata wasaa wa kuwa na uelewa wa pamoja juu ya Sheria mpya
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mahusiano kazi ya mwaka 2004,” alieleza
Mhe. Kihwelo.
Warsha hii ya Siku tatu
inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo kilichopo katika eneo la Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu imeshirikisha baadhi ya Wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO).
Katika utekelezaji wa
Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020) Mahakama ya Tanzania
imejielekeza kuboresha huduma zake kupitia ushirikishaji wa Wadau mbalimbali.
Warsha hii imeandaliwa
na Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
chini ya Ufadhili wa Fedha za Mradi wa Benki ya Dunia.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama,Lushoto(IJA) , Mhe. Dkt .Paul Kihwelo akizungumza jambo kabla ya kuanza kwa warsha ya wadau kuhusu usuluhishi wa migogoro ya kazi lililoanza leo na linatarajia kumalizika Mei 16,2018 linalofanyika kwenye Kituo cha Mafunzo, kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam. |
Baadhi ya wadau wakiwa katika warsha hiyo. |
Baadhi ya wawezeshaji wa warsha hiyo waliosimama wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu. |
Baadhi ya wadau wa
warsha hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu.
(Picha na Magreth
Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni