Alhamisi, 19 Julai 2018

WAANDISHI WA HABARI ZA MAHAKAMA WAFANYA MAFUNZO KWA VITENDO MKOANI MOROGORO


Waandishi wa habari za Mahakama wamefanya mafunzo kwa vitendo katika Mahakama za Mkoa wa Morogoro ili kuona namna Mahakama hizo zinavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wadau wa mahakama wakiwemo waandishi wa habari wanakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa weledi.

Akitoa maelekezo namna mahakama zinavyofanya kazi, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Elizabeth Nyembele amesema kuwa , katika mahakama zipo kesi zinazosikilizwa katika Mahakama za wazi na nyingine husikilizwa Mahakama za ndani( Chamber).

” Kesi zote zinazohusu unyanyasaji wa kijinsia mfano ubakaji, kesi za mambo ya ndoa au kesi yoyote ambayo itamhusisha mtoto kesi zao husikilizwa katika mahakama za ndani (Chamber)” ameongeza Mhe. Hakimu Nyembele.

Aidha, Mhe. Hakimu Nyembele amesema kuwa kwa mkoa wa Morogoro wamekuwa wakipokea kesi nyingi zinazohusiana na masuala ya unyang’anyi, madawa ya kulevya na ujangili unaosababishwa na mkoa huo kuzungukwa na mapori.

Akizungumza kuhusu suala la rushwa kwa makarani wa mahakama, Mhe. Nyembele ametoa rai kwa watumishi wote wa mahakama kuepuka kupokea rushwa na kuwa waaminifu katika utendaji wao.

Vilevile amesema kuwa katika kudhibiti suala la rushwa katika mahakama nchini, mahakama imetoa elimu kwa umma pamoja na matangazo ya huduma mbalimbali za kimahakama zinazotolewa bure mfano nakala za hukumu.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Morogoro Mjini Mhe. Agnes Ringo amesema kuwa kwa sasa kuna utaratibu mpya wa namna kesi za watoto zinavyoendeshwa bila kutoa utambulisho rasmi wa mtoto husika.

Nae Mtendaji Mkoa wa Mahakama Nestory Mjunangoma amesema kuwa katika mkakati wa kuboresha huduma za mahakama, Mahakama mkoa wa Morogoro inatarajia kuanza ujenzi wa ghorofa nne katika mwaka huu wa fedha zitakazokuwa na huduma zote za kimahakama kuanzia Mahakama ya Mwazo hadi Mahakama Kuu.

Aidha, Mjunangoma ameongeza kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Mafunzo hayo ni moja ya mradi wa maboresho ya huduma za mahakama inayotekeleza programu mbalimbali chini ya mpango mkakati wa mahakama wa miaka mitano 2015/2016-2019/202 iliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Elizabeth Nyembele akizungumza na waandishi wa habari leo wakati walipotembelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kwenye moja ya ziara za kimafunzo wakiwa katika semina ya Waandishi wa habari za mahakama mkoani Morogoro.
 Waandishi wa Habari waliotembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro wakimsikiliza Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Mhe. Elizabeth Nyembele (hayupo pichani) alipokuwa akiwapa ufafanuzi juu ya matumizi ya Mahakama ya wazi ‘open court’
 Mwandishi kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Bw. Alpha Wawa akiuliza jambo kwa Mhe. Nyembele.
 Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Bw. Nestory Mujunangoma akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari waliotembelea katika Mahakama hiyo.
 Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Elizabeth Nyembele akiendelea kutoa somo kwa waandishi wa habari waliopo katika semina ya uandishi  wa habari za mahakama mkoani Morogoro, lengo la ziara hiyo ni kujifunza kwa vitendo jinsi Mahakama inavyofanya kazi.
 Waandishi wa Habari waliotembelea Mahakama ya Mkoa Morogoro wakisoma tangazo linaloonesha dalili za Rushwa lililobandikwa katika Mahakama hiyo, lengo la Matangazo hayo ambayo yamebandikwa katika Mahakam azote nchini ni kuzuia na kutokomeza vitendo vya rushwa Mahakamani.
 Hakimu Mkazi Mfawidhi-Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Agnes Ringo (aliyesimama kulia) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari waliotembelea Mahakama hiyo mapema Julai 19.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni