Jumatano, 11 Septemba 2019

UONGOZI MADHUBUTI NA UTASHI WA KISIASA: SILAHA, MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA


Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa suala la mapambano dhidi ya rushwa linahitaji utashi wa kisiasa ‘political will’ pamoja na uongozi madhubuti kwa kila nchi ya Afrika ili kufikia azma inayokusudiwa.

Akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika (African Union Convention on Preventing and Combating Corruption-AUCPCC) mapema Septemba 11, 2019 walipomtembelea Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa hayo yatapelekea kufikia mafanikio ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa barani Afrika.

“Utashi wa Kisiasa pamoja na Utawala madhubuti ikiwemo Uwazi katika utoaji huduma ni mambo muhimu yanayohitajika kwa nchi zote za Afrika katika mapambano dhidi ya rushwa,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliueleza Ujumbe huo kuwa Mahakama ya Tanzania ni moja ya Taasisi iliyopo mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya rushwa ambapo alisema mapambano hayo yanafanyika kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama ambapo nguzo zote tatu (3) za Mkakati huo zinagusia mapambano dhidi ya rushwa.

“Nguzo hizo tatu ambazo  ni Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali,  Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau zinalenga katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya haki kwa umma na kwa gharama nafuu,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Hali kadhalika; Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa katika mwendelezo wa Mapambano dhidi ya Rushwa, Mahakama pia imesambaza mabango maalum ya ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa (yenye namba za simu) ambayo yamebandikwa katika Ofisi za Mahakama zote nchini na katika ofisi za Wadau.

Hata hivyo; Mhe. Jaji Mkuu alikiri kuwepo na changamoto ya wananchi kutojitokea hadharani kutaja mtu/mhusika anayetuhumiwa na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Naye; Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Kupambana na Kuzuia Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika (African Union Convention on Preventing and Combating Corruption-AUCPCC), Mhe. Miarom Begoto alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuwakubalia kumtembelea na kusema kuwa lengo la Bodi hiyo kutembelea Mahakama ni pamoja na kujua jinsi gani Mhimili huu unashiriki katika mapambano dhidi ya Rushwa.

“Naamini mapambano dhidi ya rushwa yatafanikiwa endapo kuna Mahakama imara na Watumishi imara wafanyao kazi ndani yake,” alisema Mwenyekiti huyo.

Ujumbe wa Bodi hiyo upo nchini kwa sasa na tayari umefanya mikutano kadhaa ya majadiliano ya kubadilisha uzoefu kuhusu rushwa na Taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Mahakama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG), Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na nyinginezo.

Kwa sasa Bodi hii ambayo makao yake makuu yapo Arusha-Tanzania ina jumla ya nchi uachama 37 za Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi mwanachama ambapo iliridhia rasmi uanachama wake mnamo Februari 22, 2005.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma (katikati) akizungumza na wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika (AUCPCC) mara baada ya kumtembelea mapema Septemba 11, 2019  ofisini kwake Mahakama ya Rufani (T)  jijini Dar es Salaam na kuzungumza naye kuhusiana  na suala la mapambano ya rushwa katika mhimili wa Mahakama.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma  akizungumza na wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika mara baada ya kumtembelea   ofisini  kwake leo, jijini Dar es Salaam ambapo  alizungumzia kuhusu  suala la mapambano ya rushwa katika mhimili wa Mahakama.

Wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu  alipokuwa  akizungumza nao walipomtembelea ofisini kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma akiwa na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika mara baada ya kumtembelea   ofisini leo, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika, Mhe.  Miarom Begoto akizungumza jambo na Mhe.Jaji Mkuu mara baada ya kumtembelea.
Jaji Mkuu  akiwaonesha  wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika, bango maalum  la mapambano  dhidi ya  rushwa la Mahakama ya Tanzania,  wakati alipokuwa akizungumza nao  ofisini kwake leo,jijini Dar es Salaam.

Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Adrian Kilimi akiwaonyesha kwa karibu bango maalum la mapambano dhidi ya rushwa la Mahakama ya Tanzania wajumbe hao.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma  akimpatia  nakala ya kitabu cha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania, Mwenyekiti  wa wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika, Mhe.   Miarom Begoto. mara baada ya kumtembelea   ofisini leo kwake jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika wakiwa katika mazungumzo hayo.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa  wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika, Mhe. Miarom Begoto.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma (wa tatu kulia)akiwa katika picha ya pamoja na  wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika na baadhi ya Maafisa wa Mahakama, (wa pili kushoto) ni  Mwenyekiti wa  bodi hiyo Mhe. Miarom Begoto.

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma  (kulia)akiagana  na  mmoja wa  wajumbe wa Bodi ya  Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika,

(Picha na Magreth Kinabo)

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni