Jumamosi, 7 Desemba 2019

JAJI MKUU: KUWENI NA UMILIKI MADHUBUTI WA MAJUKUMU YENU


 Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji Wafawidhi nchini kuwa na umiliki ‘ownership’ ya masuala mbalimbali yanayohusiana na kazi zao kwa maslahi mapana ya Taasisi na jamii kwa ujumla.
 
Akifunga rasmi Mafunzo Elekezi ya siku tano (5) kwa Majaji Wafawidhi na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa ‘EAC’ jijini Arusha, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama ni Mhimili wa Dola uliopewa dhamana kubwa ya mwisho ya utoaji haki, na tafsiri ya sheria hivyo kila Jaji ama Hakimu ana haki na wajibu wa kusimamia dhamana hii.

“Kama viongozi wa maeneo yenu, mna wajibu wa kumiliki/ kusimamia maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa sheria mbalimbali, usimamizi wa utekelezaji wa Mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (JSDS II), kusimamia uadilifu na maadili ya Watumishi walio chini yenu nk,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.

“Ili kuhakikisha kuwa mfumo wa JSDS II unafanya kazi vizuri, ni vyema mkaendelea kutoa mawazo yenu yenye tija  kwa timu yetu ya ndani inayoendelea kutengeneza mfumo huu ili kuwezesha mfumo huu kufanya vyema,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao wanapotoa huduma kwa wananchi kuhakikisha kuwa kiwango cha wananchi wanaotumia huduma za Mahakama wanaridhika, kuwa na upatikanaji wa taarifa muhimu za kesi na kujiuliza endapo huduma zetu ni rafiki kwa wahudumiwa.

Awali, akimkaribisha Mhe. Jaji Mkuu kufunga rasmi mafunzo hayo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali kufanyika kwa mafunzo hayo yenye mafanikio makubwa.

“Napenda nikushukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo haya, na vilevile nishukuru kamati nzima ya maandalizi kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo haya, kitu ambacho nasisitiza ni kuendelea kufanya kazi kama timu moja ili kufanikisha mipango tuliyoazimia/tuliyojiwekea,” alisema Mhe. Jaji Kiongozi.

Katika Mkutano huo ulioanza rasmi Desemba 02,2019 na kuhitimishwa Desemba 06 mwaka huu, mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama na Mradi wa Maboresho wa huduma za Mahakama,  Mfumo wa ‘JSDS’ II, Ukaguzi na Usimamizi wa Mahakama za chini ‘Surbodinate Courts’, Mirathi na nyinginezo.

Kwa pamoja Wahe. Majaji hao wamekubaliana/wameridhia kuyafanyia kazi yale yote yaliyojadiliwa na kuibuliwa katika mkutano huo kwa lengo la kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

 Pichani ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifunga rasmi Mafunzo elekezi ya siku tano (5) kwa Wahe. Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu yaliyofanyika katika Ukumbi wa ‘EAC’ jijini Arusha.
 Picha za Wahe. Majaji wakifuatilia hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa akifunga rasmi mafunzo.

Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na Wahe. Majaji katika Mafunzo hayo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru akifuatilia kinachojiri katika Mafunzo hayo.
 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akitoa neno.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Zahra Maruma akinukuu masuala/maelekezo muhimu yaliyokuwa yakitolewa wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimpatia cheti cha Ushiriki wa Mafunzo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Amir Mruma, wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kulia ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna. Wahe. Majaji walioshiriki katika Mafunzo hayo wote walipatiwa vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo.
Akiwa katika uso wa furaha, Mhe. Jaji Mkuu akionyesha cheti chake cha ushiriki wa Mafunzo akiwa kati ya Wahe. Majaji walioshiriki kikamilifu katika Mafunzo hayo. Hali kadhalika Mhe. Jaji Kiongozi alipatiwa pia cheti cha ushiriki wa Mafunzo hayo.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni