Jumatano, 19 Februari 2020

JAJI MENGISTU APENDEZWA NA UENDESHAJI MASHAURI KWA MAHAKAMA MTANDAO


Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu ameonyesha kufurahishwa na uendeshaji wa mashauri manne (4) yaliyosikilizwa kwa njia ya video ‘Video Conference’ kati ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa usikilizwaji wa mashauri hayo yaliyoendeshwa mapema Februari 19, 2020 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Augustina Mmbando, Jaji Mkuu huyo alisema zoezi la usikilizwaji limeenda vizuri. 

“Nimefurahishwa na jinsi ambavyo Hakimu ameendesha kesi, ameonyesha kuwa makini na mwenye kujiamini kwa wakati wote aliokuwa akiendesha mashauri hayo,” alisema Mhe. Jaji Mengistu.

Mashauri yote manne yaliyosikilizwa ni ya uhujumu uchumi, yaliyohusisha Jamhuri dhidi ya Rafael Herman na wenzake, Jamhuri dhidi ya Raia wa China aitwaye Chen Jian Lin, Jamhuri dhidi Maarifa Abasi Nasoro na Jamhuri dhidi ya Mohamed Yohana Mohamed.

Watuhumiwa wawili kati ya hao wamepatiwa dhamana na wawili wamerudishwa rumande.

Aidha Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bw. Wankyo Simon alimweleza Hakimu huyo kuwa upelelezi dhidi ya kesi hizo haujakamilika hivyo zimeahirishwa hadi Machi 04 mwaka huu.

Mbali na  kushiriki katika uendeshaji wa mashauri hayo, Mhe. Jaji Mengistu pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia walipata fursa ya kusikiliza wasilisho linalohusu Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto lililowasilishwa na Mkuu wa chuo hicho, Mhe. Jaji.Dkt. Paul Kihwelo.

Naye, Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock aliwasilisha kwa ujumbe huo wasilisho la Mifumo mbalimbali ya Kielektroniki inayotumika Mahakamani.

Bw. Enock aliitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Kusajili na Kuratibu Mashauri Mahakamani (JSDS II), Mfumo wa kusajili na kuratibu Mawakili (TAMS), Mfumo wa anuani za Kijiografia wa Mahakama (J-MAP), Mfumo wa Kiielektroniki wa kutunza maamuzi ya Mahakama (Tanzlii) pamoja na Maktaba Mtandao (‘E-Library).

Jaji Mkuu huyo leo amehitimisha ziara yake ya siku tatu (3) ya kuitembelea Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia ziara hiyo amepitishwa katika maeneo mbalimbali ya maboresho yaliyofanywa na Mahakama nchini.
 Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu akizungumza jambo katika Kituo cha Mafunzo na Habari za Kimahakama Kisutu ambapo jumla mashauri manne (4) yamesikilizwa.
 Jaji Mkuu wa Ethiopia pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Dunia wakifuatilia wasilisho kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo.
 Muonekano wa picha ya video ikionyesha mandhari ya Chuo na Wajumbe wanavyofuatilia.
 Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia) pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama wakifuatilia kinachojiri.
 Mhe. Jaji Kihwelo akifafanua jambo kwa Jaji Mengistu kuhusiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto.
 Mkuu wa Kitengo cha Maboresho- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma akizungumza jambo katika majadiliano hayo.
 Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock (kushoto) akiwasilisha mada ya maendeleo ya TEHAMA Mahakamani.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)












Hakuna maoni:

Chapisha Maoni