Jumanne, 30 Aprili 2024

BUNGE LAIDHINISHA BILIONI 441.3 BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NA TAASISI ZAKE

  •    Wabunge waipongeza Mahakama kwa maboresho ikiwemo matumizi ya TTS
  • Wapongeza Uanzishwaji wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki ‘IJCs’

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana tarehe 29 Aprili, 2024 lilipitisha jumla ya fedha za Kitanzania Bilioni 441.3 ikiwa ni bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo Miradi ya Maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zilizopo chini yake.  

Akizungumza wakati akiwasilisha Hotuba ya Mipango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025 katika Mkutano wa 15 wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) alisema Wizara hiyo imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mipango inayolenga kufanikisha jukumu la kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kuweka mazingira yanayohakikisha usawa kwa wote na kwa wakati.

Mhe. Dkt. Chana alisema Serikali kupitia Wizara imejikita kushughulikia masuala manne muhimu ili haki ipatikane kwa wote na kwa wakati ambayo ni pamoja na kufanya mapitio ya mfumo wa Haki Jinai na kuandaa mpango wa marekebisho ya Sheria ambazo zinatoa mianya ya ama kuchelewesha upatikanaji wa haki au ukandamizaji katika upatikanaji wa haki.

“Katika kuendelea kusimamia upatikanaji wa haki kwa wananchi, Mahakama imeendelea na mpango wa kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Mahakama imeshughulikia jumla ya mashauri 196,592,” alisema Mhe. Dkt. Chana.

Alieleza kuwa, kati ya mashauri hayo, mashauri 133,82 yamesikilizwa na kuhitimishwa na mashauri 62,769 yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa.

Aliongeza kwamba, katika mashauri yanayoendelea kusikilizwa, mashauri ya umri mrefu ni 2,087 pekee sawa na asilimia tatu (3) ya mashauri
yote yaliyobaki Mahakamani.

Akizungumzia kuhusu, utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, hadi kufikia Aprili, 2024, Miradi ya Ujenzi iliyokamilishwa ni Mahakama za Wilaya ya Ulanga, Kwimba na Liwale; Ukarabati wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya
Maswa.

Ujenzi wa Majengo ya Mahakama za Mwanzo Usevya Mlele, Nyakibimbili Bukoba, Mahenge (Kilolo), Newala Mjini, Madale Dar es Salaam, Kinesi Rorya na Luilo Ludewa.

"Majengo ya Mahakama yanayoendelea ama kujengwa au kukarabatiwa ni kama Ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita vya Katavi, Songea Ruvuma, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita," alieleza Balozi Mhe. Dkt. Chana.

Waziri huyo alisema ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo tatu ambazo ni Ilangala (Ukerewe), Mbalizi (Mbeya) na Machame (Kilimanjaro).

Miradi mingine ni ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya sita (6) ambazo ni Kibiti Pwani, Nachingwea Lindi, Simanjiro Manyara, Hanan’g Manyara, Mbulu Manyara na Tunduru Ruvuma pamoja na Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 61, ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Ubungo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 98 na ukarabati wa jengo la zamani la Mahakama Kuu Dodoma ambapo ukarabati wake umefikia asilimia 49.

Kadhalika, Waziri huyo alizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ambapo hadi sasa umefikia asilimia 97.3 huku akiongeza kuwa, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kabanga-Ngara unaendelea na kwa sasa upo asilimia 97, ujenzi wa nyumba 48 za Majaji eneo la Iyumbu Dodoma ambao umefikia asilimia 98 na kuendelea kwa ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu jijini Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 53.

Kwa upande mwingine, Waziri Mhe Dkt. Chana alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imesajili jumla ya watoa huduma 46 walioomba kuthibitishwa kama Watoa Huduma za Utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala, ambapo Waendesha Maridhiano ni watatu (3), Watoa Huduma za Majadiliano watatu (3), Wapatanishi 13 na Wasuluhishi 27.

”Hadi kufikia Aprili, 2024 wapo Watatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala 576, kati ya hao, Waendesha Maridhiano 38, Watoa Huduma za Majadiliano 60, Wapatanishi 185 na Wasuluhishi 293,” alisema Waziri Chana.

Aliongeza kwamba, Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (Tanzania International Arbitration Centre), Taasisi hiyo itakuwa na Kituo Dar es Salaam ambapo tayari jengo kwa ajili ya kuanzisha Kituo hicho limepatikana.

Akizungumza wakati akichangia bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu wa Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa matumizi ya Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS).

“Napenda kuipongeza Mahakama kwa hatua kubwa ya kuanza matumizi ya Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS), nipende kuishauri Mahakama kufunga Mfumo huu katika Mahakama zote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa Haki,” alisema Mhe. Dkt. Mhagama.

Wabunge mbalimbali wamepata nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa; miongoni mwa maoni na pongezi zilizotolewa ni pamoja na pongezi kwa Mahakama juu ya uanzishwaji wa Vituo Jumuishi vya utoaji Haki (IJCs), uwepo wa Mahakama zinazotembelea (Mobile Courts).

Kati ya Shilingi 441,260,152,000 zilizopitishwa na Bunge, jumla ya fedha za Kitanzania Bilioni 241.6 ni bajeti ya Mfuko wa Mahakama fungu 40. Baadhi ya Taasisi ambazo bajeti yake imesomwa na Wizara ni pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mahakama, Tume ya Kurekebisha Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. 

Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara iliidhinishiwa na Bunge jumla ya Shilingi 383,619,511,000 (bilioni 383.62) kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi 97,815,618,000 (bilioni 97.82) ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi, Shilingi 176,148,324,000 (bilioni 176.15) ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi 109,655,569,000 (bilioni 109.66) ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo Shilingi 44,112,800,000 (bilioni 44.11) ni fedha za ndani na Shilingi 65,542,769,000 (bilioni 65.54) ni fedha za nje.

 

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akisoma Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 Bungeni jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe., Eva Nkya wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma
Sehemu ya Viongozi wa Wizara ya KJatiba na Sheria pamoja na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma

Sehemu ya Viongozi wa Wizara ya KJatiba na Sheria pamoja na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma




 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni