Jumanne, 30 Aprili 2024

WATUMISHI WAHIMIZWA KUWA WAMOJA

 

Na. Francisca Swai, Mahakama – Musoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wahimizwa kuwa wamoja katika utendaji kazi wao kwa kuwa  umoja ndio msingi wa mafanikio katika maeneo ya kazi. 

Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya pamoja na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Mara Bw. Hamis Mwisa katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo uliofanyika hivi karibuni.

Akifungua mkutano huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya aliwaasa watumishi kutumia nafazi hiyo  kwa umoja wao kusema kwa uwazi changamoto wanazokutana nazo katika kazi ili zifikishwe kwa mwajiri kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi. 

‘‘Miaka ya zamani, nafasi hizi hazikuwepo, mfanyakazi alikuwa hapati nafasi ya kuoongea na mwajiri. Hivyo tutumie fursa hii kufikisha hoja zetu kwa mwajiri, tuongee changamoto na mafanikio yetu kwa umoja na kwa uwazi kuliko kuongelea pembeni. Vikao hivi ndio nafasi ya pekee ya uhuru inayomkutanisha mwajiri na mwajiriwa kwa pamoja ili kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kazi na utendaji kazi kwa ujumla,’’ alisema Mhe. Jaji Mtulya.

Naye Katibu wa TUGHE Mkoa wa Mara Bw. Hamis Mwisa, alitoa elimu juu ya umuhimu wa vyama vya wafanyakazi, mabaraza ya wafanyakazi na haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Ambapo kupitia elimu hiyo amewaasa watumishi kujiunga na TUGHE kwa wingi ili kuendelea kukipa chama hicho nguvu ya kuwasilisha masuala mbalimbali ya watumishi kwa mwajiri na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi.

Aidha, Mwisa, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa ya mazingira ya kazi hususani miundombinu ya majengo ya Mahakama. Alisema watumishi hawawezi kufanya kazi kwa moyo au kuwa na utendaji kazi mzuri kama hata mazingira ya kazi ni magumu. 

Pamoja na pongezi hizo, Bw. Mwisa, amepongeza pia salamu ya Mahakama isemayo uadilifu, weledi na uwajibikaji. Amewaasa watumishi kuzingatia salamu hiyo kwani imejitosheleza na kila mmoja akiizingatia basi hatutakuwa na migogoro kazini, tutaishi kwa umoja na upendo.

Nao viongozi wa Kanda ya Musoma walioshiriki katika baraza hilo wakiwemo Naibu Wasajili Mhe. Salome Mshasha na Mhe. Monica Ndyekobora pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi waliwasisitiza watumishi kuzingatia na kutekeleza yaliyojadiliwa na kukubaliana kwa pamoja ili kuboresha utendaji kazi wa Kanda hiyo.

Katika mkutano huo mengi yalijadiliwa. wajumbe walishiriki kikamilifu katika kujadili hoja mbalimbali za kuwasilisha kwa mwajiri pamoja na kusisitiza umoja kati ya watumishi wote.

 Watumishi wakiimba kwa pamoja wimbo wa mshikamano daima wakati wa kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma akisema neno la ufunguzi wa baraza hilo na kuwakaribisha wajumbe.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Leonard Maufi, akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo wa baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma.

 Katibu wa TUGHE Mkoa wa Mara Bw. Hamis Mwisa akiongea akitoa elimu ya vyama vya wafanyakazi, mabaraza ya wafanyakazi pamoja na kujibu hoja mbalimbali katika mkutano wa baraza la wafanyakazi Kanda ya Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na mwenyekiti wa baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akisisitiza jambo wakati wa baraza hilo. (Kushoto) ni Katibu wa baraza hilo Bw. Kandana Lucas na (kulia) ni Katibu Msaidizi Bi. Farajaa Barakazi.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha akizungumza na kusisitiza jambo wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma.



Picha juu na chini ni  baadhi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma wakiongea na kuwasilisha hoja zao katika baraza hilo.


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni