Jumanne, 30 Aprili 2024

MAHAKAMA KUU SONGEA YATOA MAFUNZO YA NDANI KWA WATUMISHI

Na Hasani Haufi- Mahakama, Songea

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, jana tarehe 29 Aprili, 2024 wamepatiwa mafunzo ya ndani kuwajengea uelewa wa mambo mbalimbali, ikiwemo miongozo, kanuni na sheria, stahiki zao  na maadili kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Nyembele aliwahimiza watumishi wote katika Kanda hiyo kuzingatia yale watakayofundishwa na watoa mada mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Watoa mada walikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Japhet Manyama, Afisa Utumishi Mahakama Kuu Songea, Bi. Paulina Kapinga, Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bi. Catherine Okum na Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Tunduru, Bw Alex Hotay.

Akiwasilisha mada yake, Mhe. Manyama alihimiza washiriki kama watumishi wa umma kuwa na maadili yanayokubalika kwani Taasisi yoyote huchafuka ikiwa na watu ambao hawana nidhamu.

Sambamba na hilo alieleza kuhusu sheria ya maadili ya Viongozi wa umma, mwongozo wa uendeshaji wa kamati za maadili na kuwapitisha kuhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama inavotekeleza majukumu yake.

Naye Bi. Kapinga alitoa mada kuhusiana na ushughulikiaji wa upandishwaji vyeo kwa watumishi, ambapo alieleza sifa zinazoweza kupelekea mtumishi akapanda cheo, muundo wa cheo cha mtumishi husika na mambo mengine.

Kwa upande wake, Bw. Hotay aliwapitisha washiriki kwenye utaratibu wa uombaji wa likizo na ruhusa, aina za likizo na hutolewa kwa wakati na misingi gani ili kwenda na matakwa ya sheria ya za utumishi wa umma.

Bi. Catherine yeye alisisitiza usalama wa data, taarifa na nyaraka na vifaa vya ofisi na usalama wa taasisi kwa ujumla kwa kuzingatia taratibu za kiusalama wa mifumo. 

Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wote wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea huku watumishi kutoka Mahakama za Wilaya Nyasa, Mbinga, Namtumbo na Tunduru na wengine walishiriki kupitia njia ya mtandao.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Japhet Manyama akiwasilisha mada.

Afisa Utumishi, Mahakama Kuu Songea, Bi. Paulina Kapinga, akiwasilisha mada.

Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Tunduru, Bw Alex Hotay akiwasilisha mada kupitia mtandao.


Sehemu ya watumishi (juu na chini) wakifuatilia kwa karibu watoa mada. 

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Bw. Epaphras Tenganamba, akitoa neno kwa washiriki kabla ya kuhitimisha mafunzo hayo. 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni