Na. Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor, hivi karibuni aliwaongoza watumishi kutembelea eneo la Magoroto ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utalii na vivutio.
Akizungumza baada ya kufika sehemu hiyo, Mhe. Mansoor ambaye aliongozana na Viongozi wengine wa Mahakama alisema kuwa lengo la kufanya utalii huo ni kuondoa msongo wa mawazo baada ya majukumu mengi ya kiutendaji.
“Jambo hili ni muhimu kwa afya ya akili zetu, awe Jaji, Hakimu, Karani au yeyote yule, ni muhimu kupata tiba hii ili wote tunaporejea katika majukumu yetu tuwe na morari mpya ya kuwajibika,” alisema Mhe. Mansoor na kuongeza kuwa safari ya pamoja kwa watumishi huleta umoja na kufahamiana.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni aliwashukuru watumishi kwa kushiriki kwenye safari hiyo na kueleza matumaini yake kuwa wanatarajia matokeo chanya katika utendaji kazi.
Kwa upande wake, Bi. Mwajuma Nyundo alisema, “Sisi kama watumishi tumefurahi sana kufika hapa, tumeongozana na Majaji na Viongozi wetu, hili jambo limetuvutia sana kwani linatuondolea hofu ya kufanya nao kazi.”
Watumishi hao wa Mahakama walipata wasaa wa kutalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kutembea juu ka milima, kujionea Ziwa na kuvua samaki, kupanda mtumbwi, kuona namna Jua linavyozama, maporomoko ya maji na kuendesha baiskeli.
Akitoa jiografia ya eneo hilo lililoko Mashariki mwa Milima ya Usambala, Mwongoza Watalii, Bw. Alfred Ngena alisema kuwa Magoroto ipo umbali wa kilomita za mraba 850 kutoka usawa wa bahari.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyenyoosha mkono juu) akiwa pamoja na watumishi wa Mahakama wakifurahia utalii wa boti.
Watumishi wa Mahakama wakifurahia utalii wa Ziwa ndani ya eneo la Magoroto.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa (kulia) wakiwa katika maeneo ya vivutio Magoroto.
Sehemu ya mahema yaliyotumiwa na watumishi wa Mahakama kupumzikia ndani ya Hifadhi ya Magoroto.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati waliokaa mstari wa nyuma) akiongoza watumishi kwenye maporomoko ya maji ndani ya Magoroto.
Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro (wa pili) akiendelea na utalii wa kupanda mlima.
Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni