Na. Innocent Kansha- Mahakama
Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan
Belete ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa niaba ya Banki ya Dunia kwa uamuzi
wa busara wa kufanya kazi na Benki hiyo.
Akizungumza
leo tarehe 20 Mei, 2024 alipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha
masuala ya familia Temeke jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukangua
na kujifunza mambo mbalimbali ya maboresho yanayoendelea kustawisha utoaji haki
nchini yanayofanywa na Mahakama kupitia mradi wa Banki ya dunia Bw. Belete
amesema Mahakama ya Tanzania imefanya kazi kubwa ya kustawisha utoaji haki
kwa wananchi wake.
“Mekuwa
mara nyingi mkitushuru sisi lakini napenda kusema sisi ndiyo tunapaswa
kuwashuru ninyi kwa kutupatia nafasi ya kufanya kazi nasi Benki ya Dunia na
imani kubwa mnayoendelea kuonyesha kwetu. Tunawapongeza sana kwa kazi kubwa
mnayoifanya ya kuboresha mazingira ya utoaji haki kwa wananchi,” amesema
Mkurugenzi Mkazi Bw. Belete.
Bw.
Belete amesema kuwa, kitu ambacho viongozi wengi wa nchi za Afrika wanapaswa
kufanya ni kuhakikisha wanaboresha mifumo ya utoaji haki kwa wananchi wao ili
kuhakikisha haki za wananchi zinalidwa kupitia mfumo wa utoaji haki ulio huru
na wa uwazi.
“Kilicho
nivutia katika ziara yangu leo ni pale nilipoambiwa kwamba watu wengi wa hali
za kawaida wanakosa huduma nzuri za kimahakama. Uwepo wa Kituo cha kisasa kama
hiki ni dhahili shairi kwamba Mahakama ya Tanzania imetoa dirisha la uhakika la
kuwahudumia wananchi wake,” amesema Bw. Belete.
Bw.
Belete amesema msingi wa maboresho ya miundombinu kama hiyo ni kusaidia
kurahisisha utoaji haki, kupunguza gharama na kuondoa ucheleweshaji wa mashauri
kwa wananchi wakati wa kutafuta haki.
Aidha,
Mkurungezi hiyo ameongeza kuwa, kupitia vituo hivyo Mahakama ina nafasi ya
kujifunga ili kuboresha miradi mingine inayoendelea kujengwa kwa kuboresha
zaidi mazingira ya utoaji haki kwa kusanifu na kuongeza mambo mazuri zaidi ili
kuimarisha utoaji haki kwa wananchi.
“Kitu
kizuri kingine nilichojifunza kutoka Mahakama ni namna ambayo Mahakama inafanya
kazi kwa kushirikiana na wadau wake katika mnyororo mzima wa utoaji haki.
Nimeona wataalum mbalimbali kama vile kutoka ustawi wa jamii, dawati la
njinsia, vyama vya kutoa msaada wa kisheria na wadau wengine. Hii inaonyesha
kwamba Mahakama haijioni kama ndiyo kila kitu katika kutoa haki bali
ushirikishwaji wa wadau ndiyo msingi wa maboresho,” ameongeza Mkurungenzi huyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel
amemshukuru Mkurugenzi huyo na ujumbe wa Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Mahakama katika safari ya maboresho na mageuzi makubwa ya
kuboresha utoaji haki.
Mtendaji
Mkuu amemuhakikishia Mkurugenzi Mkazi huyo kwamba, mikopo inayotolewa na
inayoendelea kutolewa kwa masharti nafuu itaendelea kusimamiwa vizuri ili
kuhakikisha inakidhi mahitaji halisi ya uboreshaji wa utoaji haki kwa ustawi wa
wananchi.
Prof.
Ole Gabriel amesema Mahakama ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki kisiwani Pemba ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuboresha
miundombinu ya utoaji haki nchini.
“Maboresho
makubwa yanayofanyika na yanayoendelea kufanyika mahakamani na kwa mafanikio
makubwa siri yake ni ushirikiano uliopo anaotupa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma. Jaji Mkuu ni mtu wa vitendo ni ni mtu wa matokeo, mtu
asiye taka mzaha kwenye mambo ya muhimu kama uboreshaji wa huduma za
kimahakama,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.
Aidha,
Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine maboresho yamekuwepo pia
katika upande wa mashauri Mwaka 2015 mashauri ya mlundikano yalikuwa asilimia
10 hadi 12 na kufika Mwaka 2023 Desemba mashauri ya mlundikano yamefikia
asilimia tatu (3). Hakika kazi hiyo siyo ndogo hivyo akaushukuru ujembe wa
Benki ya Dunia kwa ushirikiano waoutoa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa Mahakama.
Prof. Ole Gabriel amesema lengo la Mahakama ni kuendelea kuboresha utoaji wa haki na huduma za kimahakama, hasa kuanzia Mahakama za Mwanzo aidha takribani asilimia 70 ya mashauri yanayosajiliwa mahakamani yanatoka Mahakama za Mwanzo. Hivyo mwelekeo wa Mahakama ni kuhakikisha miundombinu ya Mahakama hizo inaimarika ili kupunguza mashauri katika Mahakama za juu.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete akifafanua jambo alipofika kumsalimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) akiwa kwenye ziara ya kukagua na kujifunza mambo mbalimbali ya maboresho yanatekelezwa na Mahakama ya Tanzania leo tarehe 20 Mei, 2024 jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete akiteta jambo Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni