Jumamosi, 25 Januari 2025

DKT. KIKWETE ANA HISTORIA NDEFU YA CHIMBUKO LA MABORESHO YA MAHAKAMA; JAJI MKUU

Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema maboresho makubwa yaliyotekelezwa na yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania ni sehemu ya Uongozi wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwani anafahamu Mahakama ilipotoka na inapokwenda katika kuhakikisha inatoa huduma bora ya haki kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hotuba ya kufungua Wiki ya Sheria nchini inayoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma leo tarehe 25 Janiari, 2025 Mhe. Prof. Juma amesema, Mhe. Dkt. Kikwete ana historia ndefu ya chimbuko la Programu ya Maboresho ya Mahakama na ushawishi wake kwa Benki ya Dunia.

“Maboresho ya Mahakama yanayoendelea unafahamu chimbuko lake. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman katika hotuba yake ya kukukaribisha kama mgeni Rasmi Siku ya Sheria nchini ya tarehe 4 Februari, 2015 anatukumbusha historia hiyo,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Mhe. Prof. Juma akimnukuu Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman amesema, “Tunakushuru sana pamoja na kuwa ulikuwa kwenye matibabu kwa kututambulisha kwa Viongozi wa Juu wa Benki ya Dunia, Novemba, 2014. Tumeanza mazungumzo nao kwa kushirikiana na Hazina. Kwa upande wetu napenda kukuhakikishia kuwa viwanja, michoro, mifano (models) na maandalizi mengine yako tayari. Tegemeo letu liliobaki kwenye miradi ya maendeleo ya Mahakama ni wewe, Mhe. Rais, tuwiye radhi kwa kukusumbua tena.”

Aidha, akifafanua Kauli Mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini 2025 isemayo “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.” Jaji Mkuu Prof. Juma amesema, Inalenga kuikumbusha Mahakama kujipanga ili itekele DIRA 2050. Vilevile, Kauli mbiu inazihamasisha Taasisi za Haki Madai ili kujiweka katika utayari wa kufanikisha malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tunakumbushana kuwa Mahakama, na pia Taasisi za Haki Madai, zina wajibu wa kuhakikisha kwamba, mfumo wa sheria na utawala bora unaohitajika utaakisi Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanafikiwa kikamilifu,” ameongeza Mhe. Prof. Juma.

Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa, kila mwaka Mahakama huadhimisha Siku ya Sheria ikiwa ni kuashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza tarehe 15 Desemba, 2024 na kumalizika tarehe 31 Januari, 2025.

Siku ya sheria nchini hutanguliwa na wiki ya sheria ambayo hutumika kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuelewa masuala mbalimbali ya kisheria na hivyo kupambanua stahiki zilizo ndani ya sheria na kutafuta njia za kuzipata, amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amesisitiza kwamba, kupitia utoaji wa elimu katika ya Wiki ya Sheria, wananchi watapata fursa ya kufahamu Katiba, Sheria, Kanuni, na taratibu zinazohusu haki na wajibu wao. Wananchi watapata pia nafasi ya kushuhudia shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama na wadau wake ili kuboresha mazingira ya utoaji haki.

“Hii inasaidia zaidi wananchi watapata fursa ya kutoa mrejesho wa huduma wanazopokea kupitia maoni yao. Maoni yatakayotolewa yatatumika kama mtaji wa kuboresha utoaji haki nchini,” ametanabaisha Jaji Mkuu.

Wiki ya Sheria ya mwaka huu naanza leo, tarehe 25 Januari, 2025 na kuendelea hadi tarehe Mosi Februari, 2025. Siku ya Sheria na kilele cha wiki ya sheria kitakuwa tarehe 3 Februari, 2025 jijini Dodoma katika viwanja vya Chinangali Pack, na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma akachukua fursa hiyo, kutoa rai kwa wananchi na wadau wote wa Sheria kutembelea sehemu zote zitakazoandaliwa kwa ajili maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchi nzima.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma katika viwanja vya Nyerere Squre leo tarehe 25 Januari, 2025

Mgeni Rasmi wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa wiki ya sheria nchini.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Mgeni Rasmi wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipowasili viwanja vya IJC Dodoma kwa ajili ya kuanza matembezi ya kilometa tano ikiwa ishara ya kuanza uzinduzi wa wiki ya sheria nchini.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa kwanza kushoto) akiwa chumba cha mapumziko kabla ya kuaza matembezi. Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia) na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa kwanza kulia).
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye matembezi na Viongozi wa Mahakama na wadau wa sheria nchini.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye matembezi na Viongozi wa Mahakama na wadau wa sheria nchini.
Sehemu ya Maafisa Habari wa Serikali wakiwa kwenye matembezi ya wiki ya sheria nchini jijini Dododma.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa anapasha misuli na Viongozi wa Mahakama na wadau wa sheria nchini.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kushoto walioketi akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya usimamizi wa mashauri Mahakama ya Tanzania Mhe. Desdery Kamugisha (kushoto wa kwanza aliyesimama)

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye kisemeo) wakati wa ukaguzi wa mabanda ya kutoe elimu wiki ya sheria jijini Dodoma.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa kwanza kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa mteja cha Mahakama ya Tanzania Mhe. Denice Domician Mlashani 
 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa kwanza kulia) akipokea maelezo kutoka bada la Taasisi ya Kuthibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini jijini Dodoma.

Sehemu ya Maafisa Waadamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ufunguzi wa Maadhimisho ya wiki ya sheria nchini.


                    (Picha na Mary Gwera - Mahakama, Dodoma)

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni