Jumamosi, 25 Januari 2025

RAIS MSTAAFU, DKT. KIKWETE APONGEZA MABORESHO YA MAHAKAMA

Ni wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Dodoma

Akiri kufurahishwa na hatua kubwa iliyopigwa na Mahakama katika utoaji huduma ya haki kwa wananchi

Mbio za furaha uzinduzi wa Wiki ya Sheria nazo zafana

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa iliyofanya katika miaka ya karibuni.

Mhe. Dkt. Kikwete amebainisha hayo leo tarehe 25 Januari, 2025 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma wakati akifungua Wiki ya Sheria kwa mwaka huu.

“Napenda kutumia nafasi hii pia kutoa pongezi nyingi kwako Jaji Mkuu na Viongozi wenzako kwa maboresho makubwa tunayoyashuhudia ndani ya Mhimili wa Mahakama, hususani katika kuboresha utoaji wa huduma za haki. Tumeshuhudia ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama kwa ngazi zote na ubunifu katika utoaji wa huduma, mambo ambayo yanahitaji pongezi,” amesema Mhe. Dkt. Kikwete.

Amekiri kufurahishwa na maboresha hayo huku akitaja mifano yake  kuwa ni pamoja na matumizi ya Mahakama zinazotembea (mobile courts), matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mifumo ya utoaji wa huduma.

“Katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, mfano mzuri ni matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kuratibu na kusikiliza mashauri Mahakamani (Electronic Case Management System). Haikuwa hivyo zamani na Waheshimiwa mnajua. Hakika maboresho yote haya yanayoendelea yanaakisi maana halisi ya maendeleo,” ameeleza Mgeni Rasmi huyo.

Ameongeza kuwa, alipokuwa Rais alikuwa karibu na Mhimili wa Mahakama, ambapo amesema, “nilifanya kazi na Majaji Wakuu watatu, yaani, Mheshimiwa Barnabas Samatta, Augustino Ramadhani na Mohamed Chande Othman. Naweza kusema kuwa hiki ndicho kipindi safari ya mageuzi ya ndani ya Mahakama ya Tanzania yalipopata kasi.”

Ameeleza kuwa, katika kipindi chake cha Uongozi kwa kushirikiana na Viongozi hao kila mmoja kwa mchango wake walifanya mambo mengi yaliyokuja kuwa msingi wa mageuzi yanayoendelea kufanyika sasa na kuboresha utendaji wa Mahakama nchini. 

Ametaja mifano ni mambo hayo kuwa ni pamoja na  

kutenganisha Prosecution na Investigation, kuteua Majaji na Mahakimu wengi, kuanzisha Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama, kuanzisha Mfuko wa Mahakama sambamba na Mradi mkubwa wa Benki ya Dunia ambao umechangia kuleta maboresho makubwa.

Aidha, Mhe. Dkt. Kikwete ameipongeza pia Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya sheria na pia kwa Kauli Mbiu nzuri ya wiki na siku ya sheria isemayo, ‘Tanzania Ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.’

“Mmechagua kauli mbiu muafaka kabisa kwa wiki na siku ya sheria kwa mwaka huu 2025. Ni jambo la faraja na kupongezwa kwa Mahakama ya Tanzania kutambua nafasi yake kama mmoja ya Mihimili ya Nchi unaoweza kutoa mchango muhimu katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Watanzania na Nchi yetu,” amesema Mhe. Dkt. Kikwete.

Amesema kwamba, kufuatia kauli mbiu hiyo ana matumaini ya kuwa, Mhimili wa Mahakama  utashiriki kikamilifu katika mchakato unaoendelea sasa wa kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambao umefanyika kitaifa jijini Dodoma umepambwa na mambo mbalimbali ikiwemo mbio za furaha (fun run) za umbali wa Kilometa tano na kumi sambamba na matembezi maalum ya uzinduzi yaliyoongozwa na Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Kikwete akiwa na Mwenyeji wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Wengine walioshiriki katika matembezi hayo ni pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Watumishi wa Mahakama, Wadau na wageni waalikwa.

Wiki ya Sheria ambayo ni maalum kwa ajili ya utoaji elimu ya Sheria imezinduliwa katika ngazi zote za Mahakama nchi nzima, Maadhimisho haya yatafanyika mpaka tarehe 31 Januari, 2025 huku Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria kikitarajiwa kuwa tarehe 03 Januari, 2025 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla itakayofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 25 Januari, 2025 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama pamoja na Wageni waalikwa wakimsikiliza Mgeni Rasmi (hayupo katika picha) alipokuwa akitoba hotuba ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria, 2025 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.


 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kulia) akiongoza matembezi maalum ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 25 Januari, 2025 jijini Dodoma. Kushoto kwa Mhe. Dkt. Kikwete ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla.

Matembezi yakiendelea jijini Dodoma.


Viongozi mbalimbali wa Mahakama wakiongozwa na Mgeni Rasmi katika mazoezi ya viungo walipomaliza matembezi.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akitoa maelekezo kwa wakimbiaji wa kilomita tano (5) kabla ya kuanza kwa mbio za fun ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria, 2025.

Mbio zikiendelea.
 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho (aliyeketi wa pili kutoka kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu matumizi ya TEHAMA mahakamani wakati alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza kufanyika katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma. Aliyeketi wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Aliyesimama kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Naibu Katibu anayeshughulikia Maadili na Nidhamu, Bi. Alesia Mbuya akitoa maelezo kuhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea banda hilo lililopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma. Aliyesimama kulia kwa Bi. Alesia ni Naibu Katibu anayeshughulikia Ajira na Uteuzi, Bi. Enziel Mtei.

Mgeni Rasmi akipata maelezo kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania leo wakati alipotembelea banda hilo lililopo kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Kikundi cha Ngoma cha Nyota kikitumbuiza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Meza kuu katika picha ya pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria, 2025.






















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni