Jumamosi, 25 Januari 2025

MAHAKAMA DAR ES SALAAM YAMOTO

  • Mamia wajitokeza uzinduzi Maadhimisho Wiki ya Sheria
  • Majaji wa Rufani, Mahakama Kuu watembea kilometa tano bila kuchoka
  • Mkuu wa Wilaya atoa ujumbe mzito

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam leo tarehe 25 Januari, 2025 wamejitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Wilaya ya Ilala.

Uzinduzi huo umetanguliwa na matembezi ya kilometa tano yaliyoanzia kwenye Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupita katika Barabara mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuishia kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Katika matembezi hayo, Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Mahakimu, Watendaji, Watumishi wa Mahakama na Wananchi kutoka Taasisi mbalimbali waliungana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda kwenye matembezi hayo yaliyochukua zaidi ya masaa matatu.

Baada ya kushiriki kwenye matembezi hayo, Wananchi walifanya mazoezi mepesi na baadaye kupata burudani kutoka Kwaya ya Mahakama ya Tanzania, maarufu kama Ng’aring’ari kabla ya Mhe. Mapunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, kuzindua maadhimisho hayo kimkoa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kusimamia sheria na kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa weledi na uadilifu mkubwa.

“Mnayoyafanya yanaonekana, bahati nzuri mifumo hii ya utoaji haki, ukifanya vizuri hakuna atakayekusifia, ukifanya vibaya ndiyo utasikia kelele. Nichukue fursa hii kuwaambia, katika kipindi cha mwaka uliopita, hatujapata kelele zinazotokana na utendaji wenu, zaidi ya kusifiwa na kuonewa huruma kwa jinsi umlivyo na mzigo wa mafaili ya kuhudumia watu…

“Shughuli yenu inahitaji umakini, uzalendo na moyo wa kujituma. Hatuna shaka yoyote katika Mihimili mitatu ya Serikali, Mhimili wa Mahakama ni kimbilio la wote. Mahakama kwa kiasi kikubwa inatenda haki. Kuna changamoto za hapa na pale, lakini ukizitizama hazitokani na utendaji wa Mahakama, ila zinatokana na maandalizi ya vyombo vingine kabla ya taarifa sahihi kufika mahakamani,” amesema.

Amewaomba watumishi wa Mahakama kutumia Wiki ya Sheria kufanya tathmini ya shughuli walizofanya mwaka jana wa 2024, kubeba changamoto zote zinazowakabili na kuchukua maoni mbalimbali ya Wadau ili watakapoanza mwaka mpya wa kimahakama wawe na nguvu za kutosha kulitumikia Taifa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ameeleza kuwa jumla ya mabanda 39, yakiwemo 12 ya Mahakama na 27 ya Wadau yameandaliwa kwa ajili ya kuonesha shughuli mbalimbali za kimahakama na Wadau kwa kipindi chote cha Wiki ya Sheria.

Amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka 2025 yanahusisha kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Mahakama na Wadau, ikiwemo kufanya tathmini ya utendaji kazi na usimamizi wa mashauri kwa mwaka 2024 na kushiriki katika utoaji elimu kwa Wananchi kuhusu shughuli zinazotolewa na Mahakama na Wadau.

“Jumla ya Vyuo vya kati viwili, Shule tano za Sekondari na Shule tano za Msingi zitapata fursa ya kukutana na watoa elimu kutoka Mahakama na Wadau mbalimbali tunaoshirikiana nao. Jumla ya Magereza manne yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam ya Ukonga, Keko, Segerea na Wazo Hill na Mahabusu ya Watoto moja Upanga yatatembelewa kwa lengo la kutoa elimu ya jumla ya haki za Wananchi na huduma za Mahakama,” amesema.

Amebainisha pia kuwa maeneo ya mikusanyiko ya watu, ikiwemo Stendi ya Magufuri, Kituo cha Mwendokasi Kivukoni na Soko la Mbagala yatatembelewa na kutumika kutoa elimu sambamba na ugawaji wa vipeperushi.

Kadhalika, Mhe. Maghimbi amewaeleza Wananchi kuwa elimu kwa njia ya Vyombo vya Habari pia itatumika na tayari wamefanya matangazo yanayorushwa katika mitandao ya kijamii na katika vipindi vya matangazo vya radio na televisheni.

Jaji Mfawidhi amesema pia kuwa katika kipindi cha Wiki ya Sheria kutakuwa na maonesho kwenye mabanda mbalimbali ya Mahakama na Wadau, onesho la picha mjongeo kuhusu hatua za ushughulikiaji mashauri kwa mtandao, bonanza la michezo na uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill.

Amewaalika Wananchi kufika kwa wingi katika Viwanja hivyo kuja kupata elimu na huduma nyingine na kuwakaribisha kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria itakayofanyika katika Viwanja vya Mahakama Kuu Dar es Salaam tarehe 3 Februari, 2025.

Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka 2025 yanabeba Kauli Mbiu inayosema, “Tanzania ya 2050:Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

 Bendi ya Jeshi la Polisi ikiongoza matembezi kuelekea uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Dar es Salaam. Picha chini ni umati mkubwa wa Wananchi waliojitokeza kwenye matembezi hayo.




Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda (kulia) akiwa na Majaji katika matembezi hayo. Mweye truck suit karibu yake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi.

Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) wakikatiza mitaa ya jiji la Dar es Salaam.


Mabango ya Wadau mbalimbali wa Mahakama ambayo yamebeba ujumbe mkuu wa Wiki na Siku ya Sheria. Picha chini ni Kikundi cha 'Jogging' kikianikiza katika matembezi hayo.


Ulikuwa mwitikio mkubwa wa Wananchi katika matembezi hayo (juu na chini).




Wananchi mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (juu na chini) wakipashapasha katika Viwanja vya Mnazi Mmoja baada ya kutembea mwendo mrefu.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza katika hafla hiyo.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam (juu na picha mbili chini) wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa maadhimisho hayo.





Kwaya ya Mahakama ya Tanzania ikitumbuiza katika hafla hiyo.

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni