Na NAUMI SHEKILINDI-Mahakama, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Kenan Kihongosi leo tarehe 25 Januari, 2025 amewaongoza Wananchi
na Watumishi wa Mahakama kwenye hafla ya ufunguzi wa Maadhinmisho ya Wiki ya
Sheria kimkoa iliyotanguliwa na matembezi maalum.
Mhe. Kihongosi aliongoza matembezi hayo kutoka katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu kuelekea katika Viwanja vya CCM Wilaya ya Bariadi ambapo ufunguzi wa maadhimisho hayo ulifanyika.
Katika matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Prisca Kayombo, Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Caroline Kiliwa, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, Watumishi wa Mahakama na Wadau wa Mahakama kutoka katika Taasisi mbalimbal.
Baada ya matembezi hayo kukamilika, Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu aliwaeleza Wananchi kuhusu ratiba ya Wiki ya Sheria ambayo itaadhimishwa mpaka kilele cha Siku ya Sheria tarehe 3 Februari, 2025.
Mhe. Kiliwa amewaomba Wananchi wajitokeze kwa wingi kupata elimu juu ya sheria katika banda la Mahakama kwa kipindi chote cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2025.
Mkuu wa Mkoa alifungua maadhimisho hayo kwa kuipa kipaumbele kauli mbiu ya Mahakama kwa mwaka 2025 isemayo “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kiongosi amesema “Sina shaka na kauli mbiu hii kwani ina lengo la kutoa hamasa kwa Taasisi zinazotoa haki madai. Ili maendeleo yapatikane pamoja na mambo mengine amani na utulivu katika nchi, ukuaji wa utawala wa sheria na uwajibikaji ni muhimu sana.”
Mkuu wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuziomba Taasisi zenye mchango katika haki madai kupitia rasimu ya Dira ya Taifa ya 2050 na kubaini malengo makuu ya Taasisi zao na kushiriki kutoa maoni na mapendekezo kwa kuboresha mambo yaliyotajwa ili utekelezaji wake uwe na tija kwa miaka 25 ijayo.
Amewakaribisha Wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya CCM na maeneo yote ambayo elimu itatolewa juu ya sheria na kuweza kupata huduma mbalimbali kutoka katika Taasisi zingine kama RITA, Uhamiaji, Polisi, Magereza, NHIF, NSSF, CRDB, TANESCO na nyingine nyingi.
Mhe. Kihongosi aliongezea kwa kuwaomba wananchi kujihusisha na kilimo kwani ni kipindi cha mvua hivyo walime ili kupata mazao. Alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi wajikinge na ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia usafi.
Baadaye, Mkuu wa Mkoa alitembelea mabanda ya Mahakama na Wadau waliokuwepo katika ufunguzi huo na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenan Kihongosi akihutubia Wananchi na Wadau wa Mahakama katika Viwanja vya CCM Bariadi ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Sheria kimkoa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni