Ijumaa, 31 Januari 2025

JAJI MAGOIGA HATAKI KUSIMULIWA

  • Atinga kwenye mabanda Wiki ya Sheria kutoa elimu ya sheria.

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama. Morogoro

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga ameamua kwenda mwenyewe kwenye banda la Mahakama kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa Wananchi.

Kufuatia maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria yanayoendelea nchini, jana tarehe 30 Januari,2025 Jaji Magoiga alifikia kwenye banda la Mahakama, Kanda ya Morogoro na kuwasikiliza Wananchi waliofika kwenye banda hilo kupata huduma mbalimbali za kisheria na kimahakama.

Akizungumza katika banda hilo, Mhe. Magoiga alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imeweka maadhimisho hayo muhimu kwa Mahakama na Jamii, hivyo naye hana budi kuingia mwenyewe kutoa elimu kwa kuwa ni kipindi wanachowaendea Wananchi huko waliko.

“Nimeitenga siku hii kuja kwenye Banda la Mahakama kuwasikiliza Wananchi mimi mwenyewe. Ndani ya mwaka mzima Wananchi wamekuwa wakiifuata Mahakama ilipo, nasi katika kipindi hiki tunawafuata walipo na kuwapatia huduma za kimahakama ambazo ni elimu pamoja na ushauri wa kisheria bila malipo,” alisema na kuendelea kuwasikiliza Wananchi waliofika mbele yake.

Aidha, Mhe. Magoiga alipata nafasi ya kutembelea mabanda mengine ya Wadau na kuona namna wanavyoadhimisha Wiki ya Sheria kwa kushirikiana na Mahakama. Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa kutoa muda wao kuungana na Mahakama kwenye maadhimisho hayo na kutoa huduma bure kwa jamii.

“Nawashukuru sana kwa kuitikia wito na kufika hapa kuungana nasi kwenye maonesho haya, kama ambavyo kauli mbiu ya mwaka 2025 imegusa Mahakama na Wadau wake, basi tukawatumikie Wananchi hawa ili kuifikia Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisema.

Sanjari na kutoa elimu kwenye banda kubwa lililoko stendi ya daladala ya zamani, pia Mhe. Magoiga alifika kwenye banda la Mahakama lililoko Stesheni ya Treni ya Mwendokasi ya Jakaya Kikwete (SGR – Morogoro).

Tangu kuzinduliwa kwa Wiki ya sheria tarehe 25 Januari, 2025, Wananchi mbalimbali wamekuwa wakimiminika kwenye mabanda ya kutolea huduma ili kupata elimu na huduma zingine za Wadau wa Mahakama.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe.Stephen Magoiga (aliyevaa kofia nyeusi) akimsikiliza mteja aliyefika kwenye banda la Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro. pembeni yake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mhe. Janeth Boaz.

Jaji Steven Magoiga akiendelea kutoa elimu kwa Wananchi (juu na picha mbili chini).

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga (aliyevaa kofia nyeusi) akizungumza na Wadau toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kushoto kwake ni Meneja wa TRA Kanda ya Morogoro, Bw. Sylver Rutagwelera.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga (aliyevaa kofia nyeusi) akiangalia huduma zinazotolewa na Wadau walioshiriki maadhimisho ya Wiki ya Sheria (juu na picha mbili chini). Kushoto kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mhe. Janeth Boaz.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga (aliyevaa kofia nyeusi) akizungumza na mwenyeji wake toka Stesheni ya Treni ya Mwendokasi ya Jakaya Kikwete wakati alipofika kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ndani ya kituo hicho.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga (aliyevaa kofia nyeusi) akitia Saini kitabu cha wageni kabla ya kuanza kutoa elimu ya sheria ndani ya kituo cha Treni ya Mwendokasi cha Jakaya Kikwete.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni