Ijumaa, 31 Januari 2025

MAHAKAMA YA MWANZO WAZO HILL YAZINDULIWA RASMI

  • Diwani awaita Wananchi kuitumia badala ya kwenda Kawe
  • Jaji Mfawidhi asema jitihada za Mahakama kusogeza huduma karibu na Wananchi dhahiri

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi leo tarehe 31 Januari, 2025 amezindua Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill, hatua inayolenga kusogeza huduma za utoaji haki karibu na Wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Maghimbi amewaambia Wananchi kuwa kuzinduliwa kwa Mahakama hiyo kumeongeza idadi ya Mahakama za Mwanzo katika Mkoa wa Dar es Salaam kutoka 14 na kufikia 15.

”Hii ni historia kwa kuwa katika Wilaya ya Kinondoni yenye Tarafa mbili na Kata 20 Mahakama za Mwanzo zimeongezeka kutoka Mahakama tatu hadi nne na ni historia kwa kuwa katika Tarafa ya Kawe yenye Kata 10 zimeongezeka Mahakama za Mwanzo kutoka moja hadi mbili,” amesema.

Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa kujengwa kwa jengo hilo na kuanzishwa kwa huduma za Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill siyo kwa bahati mbaya, bali ni utekelezaji wa programu ya  maboresho unaofanywa na Mahakama ya Tanzania.

Utekelezaji huo ni kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama ulioanza Awamu ya Kwanza Mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 na kwa sasa ukimalizia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati huo kwa mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.

Amebainisha kuwa katika maboresho hayo, yapo mambo mengi yalibainishwa na kuwekewa mikakati ya utekelezaji, ikiwemo ujenzi wa majengo mapya na ukarabati wa majengo chakavu . Mhe. Maghimbi amesema kuwa tafiti zilifanyika na matokeo kuonesha kuwepo  kwa majengo chakavu mengi na maeneo mengi kutokuwa na majengo ya Mahakama.

”Kupitia tathmini hiyo, Mahakama iliandaa Mpango wa Miaka Mitano wa  Maendeleo ya Miundombinu ambao umeainisha malengo ya ujenzi na ukarabati. Mpango huo ndio dira ya ujenzi unaoendelea katika maeneo mbalimbali  ngazi ya  Mahakama Kuu kila Mkoa, Mahakama za Hakimu Mkazi kila Mkoa, Mahakama za Wilaya kila Wilaya na Mahakama za Mwanzo angalau kila Kata...

”Kwa hiyo, jengo hili la Mahakama ya Mwanzo ni ushahidi wa kivitendo wa jitihada za Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kusogeza huduma za kimahakama karibu na Wananchi kama tulivyojiwekea katika Nguzo ya Pili ya Mpango Mkakati; lakini pia jengo hili ni  matokeo ya uboreshaji wa mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi na wadau,” amesema.

Jaji Mfawidhi ameupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na wale wanaomsaidia kwa kukubali na kuridhia Kanda ya Dar es Salaam kupewa mradi huo ambao sasa ni Mahakama kamili.

Kadhalika, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha zote asilimia mia moja zilizowezesha kujengwa na kukamilika kwa jengo hilo.

Mhe. Maghimbi ametumia fursa hiyo kuwajulisha Wananchi kwamba maboresho ya huduma za Mahakama hayajalenga tu majengo bali pia kubadili mitazamo ya watumishi kutoka kutoa huduma za haki kwa mtazamo wa zamani wa Mahakama inayotisha na sasa kutoa huduma za kimahakama zinazomlenga Mwananchi.

Amesema kuwa programu ya maboresho ya Mahakama imeleta utamaduni mpya wa utoaji huduma, wenye mitazamo ya utoaji haki kwa haraka, weledi, uwazi na ufanisi na unaomjali mwananchi ili Mwananchi atumie muda wake mwingi kwenye uzalishaji mali badala ya kupoteza muda katika kutatua migogoro mahakamani.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Bw. Beatus Benedictus alieleza kuwa jengo lilianza kujengwa na Mkandarasi Works Construction Ltd Agosti, 2022 na kutarajiwa kukamilika Februari, 2023 kwa gharama ya zaidi ya millioni za Kitanzania 600.

Alibainisha kuwa fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba jengo  limekamilika mwaka 2024.

Kwaupande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill, Mhe. Niccodemus Maroa alisema walianza kutoa huduma za kimahakama tarehe 6 Januari, 2025 na tayari mashauri 65 ya jinai yamesajiliwa na 33 kati ya hayo yameshatolewa uamuzi.

Alisema kuwa Mahakama hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi 392,587 wa kata nne ya Bunju, Mbezi juu, Wazo Hill na Mabwepande ambao awali walikuwa wakipata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Kawe iliyopo umbali wa kilometa 20.

Mhe. Maroa alibainisha changamoto zinazowakabili kama yidadi ndogo ya watumishi pamoja na umbali kutokana na barabara ya kufika mahakamani hapo kuwa mbovu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Wazo Hill, Mhe. Leonard Manyama aliwataka wananchi wa kata hiyo kutokwenda kufungua mashauri katika Mahakama ya Mwanzo Kawe na badala yake watumie Mahakama hiyo.

"Wenyeviti wa mitaa na Kata nne nawaelekeza mkaitishe mikutano katika mitaa yenu kuwaeleza Wananchi uwepo wa Mahakama hii waweze kuitumia," alisema.

Kuhusu changamoto ya umbali na ubovu wa barabara kufika katika jengo la Mahakama hiyo, Diwani huyo alisema tayari imeshapitishwa bajeti ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka eneo la Tegeta Bwawani hadi Madare kwa kiwango cha rami.

Alibainisha kuwa kabla ya ujenzi huo, barabara hiyo itakarabatiwa kwa kiwango cha changalawe. Alisema pia kuwa wataanza mazungumzo ya kuweka ruti ya daladala kutoka Tegeta Kibaoni hadi Kata ya Nyakasangwe ili wananchi waweze kufika kirahisi na kupunguza gharama za kukodi bajaji na pikipiki.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (juu na chini) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill leo tarehe 31 Januari, 2025.


Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) wakiwa mbele ya jengo la  Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill baada ya kuzinduliwa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza na Wananchi (hawapo kwenye picha) katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama hiyo leo tarehe 31 Januari, 2025. Picha chini ni Diwani wa Kata ya Wazo Hill, Mhe. Leonard Manyama.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill, Mhe. Niccodemus Maroa akiwasilisha taarifa ya Mahakama yake tangu ianze kutoa huduma za kimahakama. Picha chini ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Bw. Beatus Benedictus akieleza utekelezaji wa mradi wa jengo la Mahakama hiyo. 


Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na Wananchi (juu na picha mbili chini) wakifuatilia kilichokuwa kinajiri kwenye hafla hiyo.



Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama  waliohudhuria hafla hiyo.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wafawidhi (juu) na Mahakimu wa Mahakama mbalimbali (chini) waliohudhuria hafla hiyo.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ikiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni