Na BAKARI MTAULLAH-Dar es Salaam
Maofisa wa Mahakama ambao ni wanachama wa Taasisi ya kukopa na kuweka fedha Mahakama SACCOS leo tarehe 31 Januari, 2025 wametembelea Mahabusu ya Watoto iliyopo Kisutu Jijini Dar-es-salaam kama sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2025.
Mahakama Saccos kwa kujali utu na haki kwa kila Mwanadamu, wametembelea Mahabusu hiyo kwa kuwafariji Watoto hao na kuwapa baadhi ya mahitaji, ikiwemo vyakula, sabuni, Projector na vingine vingi.
Meneja wa mahabusu hiyo, Bw. Darius Kalijongo, akizungumza kabla ya kupokea zawadi hizo, alitoa elimu chache kuhusu namna wanavyowapokea vijana hao na kukaa nao kuwapa ushauri nasaha pia mafunzo ya ujasiriamali.
Meneja huyo pia aliishukuru Mahakama Saccos kwa moyo wao wa upendo na kwa namna walivyoguswa na Mungu kuweza kutembelea Mahabusu hiyo.
Kadhalika, aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa ujumla, kwani tangu kuzinduliwa kwa Wiki ya Sheria kumekuwa na Maofisa wengi wa Mahakama waliokuwa wakitembelea Mahabusu hiyo.
Meneja huyo alipata wasaa wa kuwatembeza sehemu mbalimbali za mahabusu hiyo zikiwemo zile za ufundi wa kushona, sehemu ya mafunzo ya Computer na uwanja wa kuchezea mpira.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa waliowakilisha, Mwenyekiti wa Mahakama Saccos, Mhe. Ferdinand Philip alishukuru kwa mapokezi na kupata fursa ya kuongea na vijana hao na kuwapa moyo, ushauri.
Alitoa ahadi kwa moja ya kijana ambaye ndoto zake ni kuwa Mwanasheria, kwamba pindi atakapohitaji msaada wa kimasomo ya kisheria, kwa namna moja au nyengine, wapo tayari kushiriki kama wazazi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Mahakama Saccos, Mhe. Mohammed Buruhani alisema wapo tayari kununua cherehani kwa ajili ya kijana ambaye ameweza kujifunza kushona, hivyo pindi atakapomaliza muda wake na kurejea uraiani atakabidhiwa ili akaendeleze ujuzi wake na aweze kujiajiri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni