- Aupongeza Mhimili wa Mahakama kwa maboresho na maonesho
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Mussa Shekimweri leo tarehe 31 Januari, 2025 ametembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea baadhi ya mabanda yaliyopo katika Maonesho hayo, Mhe. Shekimweri ameipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa pamoja na kufanya maonesho hayo yanayolenga kuelimisha wananchi.
“Naushukuru na kuupongeza sana Mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa maboresho na kwa kuendelea kuadhimisha wiki na siku ya sheria, na kuendelea kufanya maonesho haya kitaifa Dodoma,” amesema Alhaji Shekimweri.
Akizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ya mwaka huu “Tanzania ya 2050: Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,”, Mkuu wa Wilaya huyo amesema kazi ya Mahakama ni muhimu katika kuinua Taifa.
Amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama. Ametoa rai pia kwa wananchi kutembelea maonesho hayo ili kupata fursa ya elimu ya Mahakama na Sheria kwa ujumla.
Kadhalika, Mkuu wa Wilaya huyo ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kufanya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo imewafikia wananchi wengi.
Maonesho ya Wiki ya Sheria yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 01 Februari, 2025 huku kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria kikitarajiwa kuwa tarehe 03 Februari mwaka huu na Mgeni Rasmi kitaifa anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria itafanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Mussa Shekimweri (kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) jijini Dodoma leo tarehe 31 Januari, 2025 kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Mussa Shekimweri ( aliyesimama kushoto) akiwa katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Mussa Shekimweri akiwa katika mabanda mbalimbali yaliyopo kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni