Alhamisi, 30 Januari 2025

MAHAKAMA INA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUKUZA MAENDELEO YA TAIFA; DPP

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP), Mhe. Sylivester Mwakitalu amesema kuwa, Mahakama ya Tanzania ina mchango mkubwa wa kuchangia maendeleo ya Taifa kwa kusimamia kikamilifu haki madai.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo leo tarehe 30 Januari, 2025 alipotembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

“Katika ukuaji wa kiuchumi na maendeleo, migogoro ya kimadai haiwezi kukosa, hivyo Mahakama ina nafasi kubwa sana ya kuchangia katika eneo hili ikiwa linasimamiwa kikamilifu,” amesema Mhe. Mwakitalu.

Kadhalika amesema kuwa, ili nchi iweze kuwa na maendeleo inapaswa kuwa na Mifumo imara ya kisheria ili kuwezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi.

Aidha, Mhe. Mwakitalu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuwa na Mifumo mbalimbali ambayo inarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumzia kuhusu mikakati ya Ofisi yake, Mkurugenzi huyo amesema kwamba, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi walianzisha umoja na huwa wanakutana kila mwaka kwa ngazi ya kitaifa kujadili mikakati na mipango ya kusukuma mashauri.

“Tumeweza kushughulikia majalada mengi kupitia umoja huo na hii imesaidia kupunguza msongamano wa mashauri,” ameeleza Mhe. Mwakitalu huku akiwakaribisha wadau wengine wa haki jinai kushirikiana katika kusukuma mashauri hayo.

Kuhusu Maonesho hayo, Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea mabanda ya Mahakama pamoja na wadau wake ili kupata elimu ya sheria.

“Nashukuru Mahakama kwa kunipa fursa ya kutembelea Maonesho haya, nimeona ambavyo Mahakama na Wadau wanavyofanya kazi, nitoe wito kwa wananchi kupita kwenye mabanda kupata fursa ya kunufaika na elimu ya sheria, kupata vipeperushi  na kadhalika,” amesema Mhe. Mwakitalu.

Mabanda aliyotembelea Mkurugenzi huyo ni pamoja na Mahakama ya Tanzania, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Huduma za Uangalizi, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa Mashtaka (NPS).

Maonesho ya Wiki ya Sheria yanatarajiwa kukamilika tarehe 01 Februari, 2025 huku kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria kikitarajiwa kuwa tarehe 03 Februari, 2025. 


Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP), Mhe. Sylivester Mwakitalu (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kuhusu Mifumo mbalimbali iliyopo ndani ya Mahakama ya Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha wakati alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika Kitaifa katika viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma. Aliyesimama wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria nchini, 2025, wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Peter Machalo.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP), Mhe. Sylivester Mwakitalu akipata maelezo kutoka katika mabanda mbalimbali alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

(Picha na JEREMIA LUBANGO, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni