Na HILLARY LORRY- Mahakama
Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi ilifungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa matembezi ya zaidi ya kilometa tatu yakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe.Victoria Mwanziva ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi akiambatana na Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Lindi Mhe.Consolata Peter Singano hivi karibuni.
Akizungumza na mamia ya wananchi na wadau mbalimbali waliojitokeza katika Viwanja ya Mpira wa Kikapu Mkabala na Kituo cha Polisi Wilaya ya Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Mwanziva alifurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kutoa haki na pia alisisitiza Mahakama na wadau kutoa elimu kwa moyo na kujikita kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine wasingeweza kufika katika Mabanda ya Mahakama.
Kwa upande wake,Hakimu Mfawidhi huyo, Mhe. Singano aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.
Aidha aliwasihi wananchi wajitokeze kwa wingi katika mabanda ya utoaji elimu ili kupata elimu inayotolewa bila gharama yoyote na Mahakama ya Tanzania wakishirikiana na wadau katika kukata kiu yao ya masuala mbalimbali yanayohusu sheria.
''Mwitikio huu mkubwa ni ishara nzuri ya kuonesha imani ya wananchi kwa Mahakama ya Tanzania,napenda kuwasihi wananchi mjitokeze kwa wingi katika mabanda ili mpatae elimu na kupata ufumbuzi mambo mbalimbali ya kisheria,” alisema Hakimu Mfawidhi huyo.
Uzinduzi wa Wiki ya Sheria ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Mahakama na viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi,Stahiki Meya Lindi,Viongozi wa Taasisi mbalimbali.
Sambamba na hilo viongozi hao walipata wasaa wakutembelea na kuona mabanda mbalimbali ya wadau wanaotoa elimu kwenye Wiki ya Sheria nchini.
Hakimu Mkazi Mfawidi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe.Consolata Peter Singano akisoma hotuba wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Mpira wa Kikapu Lindi.

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni