Alhamisi, 30 Januari 2025

WATUMISHI MAHAKAMA DAR ES SALAAM WATEMBELEA MAKAZI YA WAZEE NUNGE

Watembelea pia Mahabusu ya Watoto Upanga

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam leo tarehe 30 Januari, 2025 wametembelea Makazi ya Wazee wenye Mahitaji Maalum Nunge, Wilaya ya Kigamboni na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kama sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2025.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Heriet Mwailolo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, aliwaongoza watumishi hao kwenye tukio hilo la matendo ya huruma.

Mhe. Mwailolo alishirikiana na Katibu Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine, Bi. Lightness Kiula, ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo.

Watumishi hao waliwasili katika Makazi hayo majira ya saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Jacqueline Kanyamwenge, ambaye alionesha kufurahishwa na ujio wa wageni wake hao.

Baadaye alieleza historia fupi ya Makazi hayo na kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuwafikiria, kuwakumbuka na kuwajali Wazee hao kwa mahitaji mbalimbali muhimu.

“Hili mlilolifanya ni jambo jema sana. Wazee wetu wanafurahi sana mnapowatembelea na kuwasaidia mahitaji muhimu kama haya. Tutamfikishia Katibu Mkuu wa Wizara taarifa ya ujio wenu ili naye apate kufahamu, asanteni sana,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ameeleza kuwa Viongozi wa Mahakama wameona vema katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kutuma wawakilishi kuja kuwaona kama Wadau na kuwasalimia.

“Viongozi wetu wameona tusiishie kwenye zoezi la utoaji elimu pekee, bali pia tupate fursa ya kuwatembelea Wadau wetu na kuonesha jinsi Mahakama inavyowathamini,” Mhe. Mwailolo, amesema.

Awali, Katibu wa Kamati aliwasilisha kwa Uongozi wa Makazi hayo orodha ya vitu mbalimbali walivyokuja navyo kwa ajili ya kutoa kama msaada kwa wazee hao.

Sehemu ya vitu hivyo ni kilo 100 za mchele, kilo 50 za sukari, kilo 100 za unga wa sembe, kanga za urafiki doti sita, mafuta ya kupikia lita 20, fulana za ndani dazani tisa, mafuta ya nazi dazani mbili, sabuni za unga mifuko mitano, juice boksi kubwa dazani 10 na sabuni za kuogea dazani 14.

Watumishi hao wamewasilisha pia mikeka mikubwa 15, maziwa ya unga dazani moja, sawa na kopo 24, nyanya sado mbili, vitunguu maji kilo tano, karoti kilo tano, pilipili hoho kilo tano, matikiti matatu, mananasi matatu pamoja na viungo vingine.

Wawakilishi wa Wazee hao, Bw. Mussa Muna na Bw. George Joseph wameelezea kufurahishwa na kitendo kilichofanywa na Mahakama kwa kuwakumbuka na kuja kuwatembelea.

Jana tarehe 29 Januari, 2025, watumishi hao, wakiongozwa na Mlezi wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hussein Mtembwa walitembelea Mahabusu ya Watoto Upanga na kutoa zawadi za aina mbalimbali kwa wahitaji.

Miongoni mwa zawadi hizo ni vyandarua 46, sukari kilo 25, mchele kilo 50, sabuni za kuogea, sabuni za chooni, vikombe mfupa wa Samaki dazani nne na nyingine nyingi.

Zawadi mbalimbali zikishushwa kwenye magari katika Makazi ya Wazee wenye Mahitaji Maalum Nunge Kigamboni.

Zawadi mbalimbali zilizotolewa na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam kwa Wazee hao.

Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Jacqueline Kanyamwenge (katikati) akiwasilisha neno la shukrani baada ya kupokea zawadi hizo.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Heriet Mwailolo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, akizungumza kabla ya makabidhiano ya zawadi mbalimbali zilizotolewa na Watumishi wa Mahakama kwa Wazee hao.

Katibu Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine, Bi. Lightness Kiula, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Huduma za Jamii akiwasilisha orodha ya zawadi mbalimbali kabla ya kukabidhiwa kwa Wazee hao. Picha chini ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama waliotembelea Makazi hayo.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Heriet Mwailolo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, akimkabidhi Mzee mmoja sehemu ya zawadi hizo.

Katibu Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine, Bi. Lightness Kiula, ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo, akikabidhi sehemu ya zawadi hizo kwa mmoja wa Wazee hao.

Watumishi wa Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wazee na wahudumu katika makazi hayo. Picha ya chini wakibadilishana mawazo.


Watumishi wa Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu na Maafisa Ustawi wa Jamii.

Mlezi wa Kamati ya Huduma za Jamii, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hussein Mtembwa akizungumza katika Mahabusu ya Watoto Upanga. Picha chini ni zawadi mbalimbali zilizowasilishwa kwa watoto hao.


Mlezi wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hussein Mtembwa akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama waliotembelea Mahabusu ya Watoto Upanga na kutoa zawadi za aina mbalimbali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni