Na INNOCENT KANSHA – Mahakama, Dodoma.
Wananchi
wataadhalishwa kuepuka kutoa rushwa ama kwa kushawishi au kushawishiwa wanapokuwa
wakihitaji huduma katika ofisi za umma kwani kwa kufanya hivyo wanatenda kosa
kisheria kwa mtoa rushwa na mpokea rushwa, ifahamike kuwa ni kosa la jinai
linaloambana na adhabu ya kifungo au fani ama adhabu zote mbili kwa wakati
mmoja.
Rai
hiyo imetolewa leo tarehe 30 Januari, 2025 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Hawa Mguruta kwa nyakati tofauti wakati wa utoaji Elimu ya sheria kwa wananchi wa
jijini Dodoma katika Viunga vya Makulu na Kikuyu kufuatia mwendelezo wa utoaji
wa elimu ya sheria katika Maadhimisho ya wiki ya sheria inayoadhimishwa kote nchini.
“Vitendo
vya rushwa ni adui namba moja wa haki kwani havitakiwi kufumbiwa macho na jamii
ya watu wasitarabu, rushwa hupofusha macho na kusababisha mwenye haki asiipate
haki hiyo anayoitafuta. Ni rai yangu, ndugu wananchi tunapoona viashiria vya
rushwa mahali popote unapotafuta huduma vilipotiwe mara moja kwenye mamlaka
husika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi wasiyokuwa waadilifu,”
amesisitiza Mhe. Mguruta.
Aidha,
Mhe. Mguruta amewambia wananchi hao kuwa, Mahakama ya Tanzania imeanzisha Kituo
cha Huduma kwa Mteja, Kituo hicho kinafanya kazi masaa 24 kupokea malalamiko,
pongezi, ushauri, maoni na hata taarifa zenye viashiria vya kudai na kupokea
rushwa kwa watumishi wasiyo waadilifu kwa lengo la kuboresha huduma za utoaji
haki kwa wananchi. Kituo kinatumia namba ya bure: 0800 750 247 ambayo mwananchi
akiitumia atasikilizwa kwa weledi mkubwa na shida yake kutatuliwa kutokana na
msingi wa huduma aliyopewa mahakamani.
“Kituo
hicho cha huduma kwa mteja cha Mahakama ya Tanzania kinachotumia namba hiyo ya
bure kimeanzishwa maalum kwa ajili ya kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji
miongoni mwa watumishi wa Mahakama na kusaidia kuongeza ufanisi wa utoaji
huduma kwa wananchi ni vema tukaitumia namba hiyo muda wote tunapoona viashiria
vya kutopata huduma stahiki ili kutatua changamoto tunazokutana nazo wakati
tunapata huduma za kimahakama,” ameongeza Naibu Msajili huyo.
Vilevile,
Mhe. Mguruta amesema, hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiimarisha katika
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupunguza mwingiliano
na mawasiliano yasiyo ya lazima na ya moja kwa moja baina ya wateja wa Mahakama
na watumishi. Kwani mteja anaweza kusajili shauri lake akiwa nyumbani,
kusikiliza shauri lake akiwa nyumbani, kutoa ushahidi wake hata akiwa nje ya
nchi, kupokea nakala ya hukumu kwa njia ya mtandao bila kufika mahakamani kwani
nakala za hukumu zinatolewa bure pasipo na malipo yoyote na hata kufanya malipo
ya ada zitozwazo na Mahakama kwa njia ya kimtandao bila kufika mahakamani.
“Matumizi
ya TEHAMA yanapunguza mianya ya rushwa na kupunguza malalamiko kwa kiasi
kikubwa, kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibakaji katika kutoa huduma kwa wananchi
wanaohudumiwa na Mahakama ya Tanzania. Ni vema ndugu wananchi tukajielisha
namna ya kutumia TEHAMA kupata huduma za kimahakama kwa njia rahisi inayookoa
muda, usumbufu usio wa lazima na kuokoa gharama ili mwananchi huyu awaze kupata
muda wa kutosha kushushiliki shughuli za kiuchumi na uzalishaji mali ili kukuza
pato lake na la Taifa,” ametanabaisha Mhe. Mguruta.
Kwa
upande wake, Mdau wa Mahakama ya Tanzania kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
(CMA), ambaye ni Msuluhishi Mwandamizi Bw. Thomas Malekela akitoa elimu kuhusu
migogoro ya kazi amewambia wananchi kuwa, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ni Taasisi
ya Serikali ambayo imewekwa mahususi kwa ajili ya utatuzi wa mashauri
yanayotokana na ajira ama kesi zinazotokana na ajira.
“Wewe
mwajiriwa ama ndugu yako ameajiriwa au wewe umeajiri, haki zako zinazotokana na
uhusiano huo na zinasimamiwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi. Watu wenye
tafsiri ambayo pengine ni potofu tungeweza kusema wanafikiri kwamba sisi kazi
yetu ni kutetea wafanyakazi la hasha. Sisi kazi yetu ni kusimamia haki kati ya
Mwajiri na Mfanyakazi katika umoja wao au mtu mmoja mmoja,” amesema Bw. Malekela.
Bw.
Malekela amesema, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi inatatua migogoro kwa namna mbili,
njia ya kwanza ni kusuluhisha na kurejesha mahusiano mahali pa kazi na njia ya
pili ni kutoa hukumu kwa pande zilizoshindwa kabisa kurejesha mahusiano mahala
pa kazi, kwa kutambua hilo ni Tume ni Taasisi maalum kwa ajili ya utatuzi wa migogoro
inayotokana na ajira.
“Baadhi
yetu tumekuwa tukienda kwa Viongozi wengine kama vile wa Mtaa, wa Kata, kwa
Diwani, kwa Katibu Tarafa, kwa Katibu Tawala Wilaya hata kwa Mkuu wa Wilaya
kueleza migogoro yetu na waajiri. Kule kwa kufanya hivyo wanakuwa wamepoteza muda
wao kwa sababu siyo mamlaka sahihi kwa utatuzi wa migogoro ya kiajira,”
amesisitiza Msuluhishi huyo.
Bw.
Malekela amebainisha kwamba, Sheria imeweka utaratibu bayana kwamba, mwajiriwa akiwa
na tatizo la aina Fulani mfano, kuachishwa kazi unatakiwa kufungua kesi kwenye
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ndani ya siku 30 bila kuchelewa ili asipoteze haki
zako za kiajira.
“Sasa
wewe ukiamua kwenda kwa Afisa Mtendaji unapoteza muda wako kwa sababu siyo
mamlaka sahihi kwa kesi uliyonayo ama mgogoro ulionao vivyo hivyo ukienda kwa
Katibu Trafa na kwa Mkuu wa Wilaya na hata wengine wasiyo kuwa na mamlaka ya
sheria ya kitume,” amesisitiza Msuluhishi huyo.
Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi ni chombo cha kimahakama kwa sababu kinatoa hukumu,
kinatoa tuzo (Decree) ambayo ina nguvu sawa na Mahakama ya Wilaya na Mahakama
ya Mkoa, na kama mtu anakuwa hajaridhika na maamuzi yaliyotolewa na Tume
anapaswa kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu, Kitengo cha ajira ama Kazi kwa muda
ulibainishwa kisheria, ameongeza Bw. Malekela.
Vilevile, Msuluhishi huyo amewasisitiza wananchi kwamba, migogoro ya ajira inautaratibu wake wa kushughulikiwa na siyo kila mtu anamamlaka ama uwezo wa kusuluhisha migogoro ya ajira. Bali Tume tu ndiyo inauwezo na mamlaka kisheria kushughulikia migogoro ya mahusiano kazini.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hawa Mguruta (mwnye tsherti nyeupe) akitoa Elimu ya sheria kwa wananchi wa jijini Dodoma katika Viunga vya Makulu na Kikuyu katika zoezi la utoaji elimu kwenye mkusanyiko wa wananchi leo tarehe 30 Januari, 2025 Viunga vya Makulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni