Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara
Maadhimisho ya Wiki ya
Sheria katika Mkoa wa Mtwara yalizinduliwa tarehe 27 January 2025 katika Viwanja
vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara, huku Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa, Kanali
Patrick Sawala.
Uzinduzi huo ulifanyika tarehe
27 Januari, 2025 badala ya tarehe 25 Januari, 2025 kufuatia kibali maalumu
kilichotolewa na uongozi wa Mahakama.
Maadhimisho hayo yalianza
kwa maandamano ya Wananchi na Wadau wa Mahakama kuanzia Viwanja vya Mahakama
Kuu Mtwara hadi Viwanja vya Mashujaa ambapo shughuli ya uzinduzi ilifanyika.
Akizungumza kwenye
uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa sheria katika kukuza
maendeleo ya jamii na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote. Aliwahimiza Wananchi
kuitumia fursa hiyo ya Wiki ya Sheria kujifunza zaidi kuhusu haki zao na wajibu
wao.
Aidha, aliwasihi
watumishi wa Mahakama kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu katika kutekeleza majukumu
yao.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim, kabla ya kumkaribisha mgeni
rasmi, alizungumzia juu ya jukumu la Mahakama katika kulinda haki za Wananchi
kulingana na kauli mbiu ya mwaka 2025.
Kauli Mbiu hiyo inasema, “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia
Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.” Mhe.
Ebrahim aliahidi kuwa Mahakama itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha
kila mtu anapata haki yake kwa wakati.
Baada ya hotuba fupi,
mgeni rasmi pamoja na Viongozi wengine walitembelea mabanda ya maonyesho
yaliyoandaliwa na Taasisi mbalimbali, ikiwemo Mahakama, Magereza, Ustawi wa
Jamii, Tume ya Haki za Binadamu na Jeshi la Polisi ambapo kila mmoja alikuwa na
jambo la kipekee la msaada wa kisheria kwa jamii.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mtwara yamekuwa na mafanikio makubwa katika kuwajengea uwezo Wananchi kuhusu masuala ya kisheria na kuimarisha uhusiano kati ya vyombo vya sheria na jamii.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni