Jumatano, 29 Januari 2025

MAHAKAMA TABORA YAPANDA MITI, YATEMBELEA KITUO CHA WAZEE NA HOSPITALI YA RUFAA KITETE

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi katika kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini wamefanya ziara maalum ya kijamii iliyojumuisha shughuli za kupanda miti, kutembelea Kituo cha Kulelea Wazee cha Amani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Kitete lengo likiwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kusaidia jamii, kuimarisha mshikamano wa kijamii, kuunga mkono ustawi wa jamii kwa vitendo na kutoa faraja kwa wenye uhitaji.

Shughuli ya kupanda miti ilifanyika katika maeneo ya Mahakama ya Mwanzo Isevya na Kituo cha Polisi Isevya, akizungumza wakati wa tukio hilo, Mhe.Dkt. Mambi alisisitiza juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kupanda miti kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira kwa vizazi vijavyo.

"Kupanda miti ni jukumu letu sote. Miti inachangia kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha tunakuwa na mazingira bora kwa siku za usoni," alisema Jaji Dkt. Mambi.

Baada ya kupanda miti, msafara huo ulielekea Kituo cha Kulelea Wazee cha Amani, ambapo wazee walipatiwa msaada wa vifaa mbalimbali kama nguo, mashuka, vifaa vya usafi, na chakula, wakiwa katika Kituo hicho, Mhe.Dkt. Mambi alisisitiza umuhimu wa kuwatunza na kuwaheshimu wazee kama hazina muhimu kwa jamii.

"Wazee ni sehemu muhimu ya jamii yetu, tunapaswa kuwaheshimu, kuwajali na kuhakikisha wanapata huduma bora. Mchango wetu ni kielelezo cha upendo na mshikamano kwao," alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Ziara hiyo pia ilifikia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete, ambapo wodi ya watoto na wodi ya wanawake wajawazito zilitembelewa, vifaa muhimu vilitolewa kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na msaada kwa watoto waliolazwa na wanawake wajawazito. Mhe. Dkt. Mambi aliwapa faraja wagonjwa na familia zao, akiwahimiza kuwa na matumaini.

"Huduma za afya ni muhimu kwa ustawi wa jamii yetu. Kama Mahakama, tunajivunia kuonesha mshikamano na kusaidia wanaohitaji msaada katika mazingira haya," alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Uongozi wa Hospitali hiyo ulitoa shukrani za dhati kwa msaada uliotolewa huku Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Amani Mtinangi, alisema, "tunawashukuru Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na wadau wote kwa msaada huu muhimu. Msaada huu utaboresha huduma zetu, hasa kwa watoto na wanawake wajawazito, tunaomba wadau waendelee kujitolea ili kuboresha maisha ya jamii yetu."

Jaji Mfawishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi (aliyevaa kofia) akizungumza na mojawapo ya familia za watoto waliolazwa katika wodi ya watoto ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete kama sehemu ya juhudi za kuonyesha mshikamano na msaada Mahakama na wadau katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu madhumuni ya ziara ya kijamii iliyohusisha kupanda miti, kutembelea Kituo cha Kulelea Wazee cha Tabora na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi (kulia) akikabidhi vifaa kwa wazee wawili kwa niaba ya wazee wa Kituo cha Amani.

Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji akizungumza na Waandishi wa Habari akitoa shukrani kwa Jaji Mfawidhi Tabora, Mhe. Dkt. Mambi msaada walioutoa katika kuboresha huduma za kijamii.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni