Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha kwa kushirikiana na wadau wake wanaendelea kutoa elimu ya taratibu za kimahakama na sheria kwa ujumla kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo katika Ofisi za Serikali, Shule za Msingi, Sekondari, maeneo ya wazi pamoja na katika Ofisi za Serikali za Mitaa.
Wakitoa elimu kwa watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha leo tarehe 31 Januari, 2025 Msuluhishi na Muamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Mhe. Ndimuyake Mwabeza amesema migogoro ya kazi inarudisha nyuma maendeleo ya Taifa hivyo amehimiza Waajiri na Waajiriwa kufanya suluhu na kumaliza katika hatua hiyo badala ya kuendelea mpaka kwenye uamuzi ambapo tume hukaa kama Mahakama ya kawaida kusikiliza na kuamua shauri.
Mhe. Ndimuyake amesema, hatua hiyo inasababbisha uhasama wakati ingeishia kwenye usuluhishi watu wangemaliza kwa amani na kuendelea na shughuli nyingine za kujenga Taifa, ameeleza kuwa, “mgogoro wa kazi unasababisha kurudisha nyuma maendeleo hivyo tunahimiza usuluhishi kwanza.”
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya, Bw. Ntumenwa Moses amesema kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi kama ilivyo ainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akijibu swali aliloulizwa kuhusu mtoto kumiliki ardhi, Bw. Moses amesema mtoto anaweza kumiliki ardhi kupitia mzazi wake mpaka hapo atakapofikisha umri wa miaka 18.
Akieleza kuhusu kazi za Mabaraza ya Ardhi, Mhe. Moses amesema kuna ngazi za kupitia mpaka kufika Baraza la Ardhi la Wilaya kwanza, amezitaja ngazi hizo kuwa ni Baraza la Kijiji la Ardhi, Baraza la Kata la Ardhi na endapo usuluhishi ukishindikana katika ngazi hizo ndipo huenda kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya.
Kwa upande wa Mahakama elimu kuhusu ndoa, talaka na mirathi zimetolewa kwa watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha, ambapo watumishi hao waliweza kuuliza maswali kadhaa kuhusu talaka na sababu za ndoa kuvunjwa. Mahakimu walioshiriki katika zoezi la utoaji elimu walipata nafasi ya kuwajibu watumishi hao kwa nyakati tofauti.
Akitoa shukrani baada ya zoezi la utoaji elimu kwa Watumishi wa Shirika hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi amewashukuru watumishi hao kwa kutenga muda wao kupata elimu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi akitoa elimu leo tarehe 31 Januari, 2025.
Msuluhishi na Muamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Ndimyake Mwabezi akitoa elimu kwa watumishi wa Hospitali ya Tumbi-Kibaha leo tarehe 31 Januari, 2025 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kibaha, Bw. Ntumengwa Moses akitoa elimu leo tarehe 31 Januari, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni