Jumamosi, 1 Februari 2025

SUMBAWANGA WAFANYA HAFLA YA KUMPONGEZA JAJI NANGELA.

Na Fredrick Mahava- Mahakama, Sumbawanga

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga pamoja na wadau wamempongeza Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Deo Nangela baada ya kuapishwa rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan

Mhe. Dkt.  Deo Nangela aliteuliwa tarehe 10 Januari, 2025 na Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, kabla ya uteuzi huo, Jaji Dkt. Nangela alikuwa Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga.

Akizunguza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga pamoja na wadau Mhe. Dkt. Nangela aliwashukuru watumishi na wadau wote kwa upendo na ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote alichokuwa Jaji Mfawidhi na kuwaomba wauoneshe pia kwa Jaji Mfawidhi ajaye.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa neema yake ya kunifanya niwe hivi nilinyo leo, na bila ushirikiano, umoja, upendo, mshikamano niliopata kutoka kwenu watumishi wenzangu pengine nisingefika hapa,” alisema Mhe. Dkt. Nangela.

Aidha, aliwataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, weledi, uwajibikaji na kujiepusha na vitendo vya rushwa, pia wajikite katika shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato kwani Sumbawanga ina fursa nyingi.

Naye, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Abubakar Mrisha akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi alimpongeza Mhe. Dkt. Deo Nangela na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya na kuwahimiza watumishi kufanya kazi kwa ufanisi na weledi kwani ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Joseph Luambano akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Kanda hiyo alimpongeza Mhe. Dkt. Nangela kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuahidi kuendeleza yale mazuri ambayo amewaachia.

Vilevile, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba alimpongeza Mhe. Dkt. Nangela na kusema kwa kipindi kifupi alichofanya kazi na Mhe. Dkt. Nangela amejifunza mengi ikiwemo kuwa mtu wa kukubali mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kuwahudumia wananchi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na watumishi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga, Mawakili kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (NPS) na Mawakili wa Halmashauri  ya Manispaa ya Sumbawanga.



Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Deo J. Nangela  (katikati) akiwa kwenye Picha ya Pamoja na Watumishi, wadau wa Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda wa Sumbawanga.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Deo J. Nangela  akipokea Zawadi  kutoka kwa Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. Abubakar Mrisha (aliyenyoosha mkono) wakati wa hafla ya kumpongeza iliyofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Deo J. Nangela akitoa neno la shukurani kwa watumishi na wadau wakati wa hafla hiyo.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mhe. Abubakar Mrisha  akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kumpongeza Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Deo J. Nangela.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga Mhe. Kisasila Saguda akitoa neno wakati wa hafla hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba akitoa salamu za pongezi.

Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe, Joseph Luambano akitoa Salamu za pongezi kwa niaba ya watumishi wa Mahakama Kanda hiyo.


Mkuu wa Mashitaka Mkoa wa Rukwa Bi. Atufike Rhoda Ngole (aliyesimama) akitoa Salamu za Pongezi.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni