Jumamosi, 1 Februari 2025

MBEYA YAHITIMISHA MAADHIMISHO YA WIKI SHERIA VIWANJANI KABWE

Na Daniel Sichula-Mahakama, Mbeya

Katika kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mkoa wa Mbeya, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga atembelea mabanda yaliyokua yanatoa huduma ya elimu ya sheria kwa wakazi wa jiji la Mbeya katika kipindi chote cha maadhimisho hayo na kusikiliza mapendekezo, maoni na mafanikio waliyopata ili kuboresha maadhimisho yajayo.

Taasisi zilizokua zinatoa huduma kwa wananchi katika viwanja vya stendi ya mabasi Kabwe jijini Mbeya walishukuru Uongozi wa Mahakama Mbeya kwa mwaliko waliopewa, kwani imekua inamanufaa kwao kwa kuwa wananchi wengi waliweza kufika katika mabanda yao kupataa taarifa mbalimbali za kitaalam kuhusu sheria, ukatili wa kijinsia, upatikanaji wa huduma za uandikiashaji wa vyeti vya uzazi na kifo na huduma mbalimbali za kimfumo wa Mahakama katika kufungua mashauri kwa njia ya mtandao, kusajili na kusikiliza mashauri.

Aidha, katika Banda la Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya Kitivo cha Sheria, walisema, kufanikiwa kwao katika maadhimisho ya wiki sheria toka yameanza tarehe 25 Januari, 2025 kunatokana na kuwahudumia wananchi wengi wa rika tofauti na kuwapatia msaada wa kisheria pamoja na mambo mbalimbali yanayohusu tasnia ya sheria kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mhe.Tiganga akitoa nasaa zake kwa Taasisi zote zilizoweka mabanda na kutoa huduma katika maadhimisho hayo kwa kipindi cha wiki nzima alisema

“Maadhimisho haya yamekua na tija kwa jamii kulingana na maelezo ya washiriki pia na wadau mbalimbali waliotembelea katika viwanja hivi vya Kabwe kupata elimu ya kisheria na huduma kutoka kwenye Taasisi na Kampuni mbalimbali, kwa hili napenda kuwashukuru kwa kujitoa kwenu kwa hali na mali na tumeonesha utumishi wetu kwa watu,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Mhe. Tiganga na timu yake ya watoa elimu ya sheria walifika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CuoM) kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria ya mirathi, wosia na sheria ya mwenendo haki madai.

Aidha, mtoa mada kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali alijikita zaidi katika ufunguaji wa mashauri ya madai, usikilizaji wa kesi za madai pamoja ufungaji wa kesi hizo, akifanunua juu ya ufunguaji wa mashauri hayo ya madai amesema, kuwa migogoro ya kesi za madai inafunguliwa sehemu husika ambako mgogoro umetokea, kwa hiyo shauri likifunguliwa sehemu ambayo mgogoro haujatokea Mahakama hiyo inakuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Vilevile, mada iligusia vigezo vya kuzingatia kabla ya ufunguaji wa shauri la madai dhidi ya Serikali, na kueleza kwamba kesi ya ardhi kupeleka Mahakama ya Biashara inaondoa uhalali wa shauri hilo kusikilizwa.

“Kanuni takribani 60 zimefanyiwa marekebisho juu ya haki madai ili kuzipa kibali Mahakama zote uhalali wa kuweza kusikiliza kesi za haki madai na hili linatokana kwamba, haki madai inagusa watu wengi na kupitia hili Mahakama na Serikali zinafanya jitihada kubwa katika kuondoa migogoro katika haki madai,” alisema mtoa mada.

Wakti huo, kupitia Uongozi wa CuoM walimuomba Mhe. Tiganga na timu yake kuja kutoa elimu ya sheria zaidi kwa wanafunzi wote kwani waliobahatika kupata elimu hiyo ni kutoka Kitivo cha Sheria pekee.

Akihimisha, Mhe. Tiganga aliushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu Cha Katoliki Mbeya na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Romuard Haule pamoja Mkuu wa Kitivo Cha Sheria wa Chuo hicho Dkt. Abdullaman Kaniki kwa mapokezi na ushirikiano walitoa kwa kipindi chote cha maadhimisho ya wiki ya sheria, na kuwaahidi kuleta wataalam wa sheria kutoka Mahakama Mbeya kuja kutoa elimu zaidi Chuoni hapo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akitoa hotuba ya kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mkoa wa Mbeya katika banda la Mahakama Kuu kwenye viwanja vya Kabwa jijini Mbeya. Kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Bi. Mervis Miti. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama Kanda hiyo na Viongozi wa  Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CuoM) na wanafunzi mara baada ya kutoa elimu ya sheria.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akipokea maelekezo kutoka kwa mdau Banda la Chama cha Wanasheria Tanganyika TLS chata ya Mbeya.
Mkuu wa Kitivo Cha Sheria wa Chuo hicho Dkt. Abdullaman Kaniki akitoa shukurani kwa Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akisaini Kitabu cha wageni walitembele Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CuoM) kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akiteta jambo na mteja aliyefika kwenye banda la Mahakama kupata huduma ya kisheria.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni