Na CHARLES NGUSA – Mahakama, Geita
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, tarehe 29 Januari,2025 imeendesha Mdahalo wa kuazimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Mdahalo huo umeendeshwa katika ukumbi wa EPZA mjini Geita ambapo lengo kubwa la mdahalo huo ilikuwa ni kutaka kupata mrejesho wa shughuli zake tangu kuanzishwa kwake na hasa mafanikio pamoja na changamoto.
Wadau mbalimbali wameshiriki ikiwemo Ofisi ya Mashitaka Mkoa wa Geita, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mawakili wa Kujitegemea, Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Geita, Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama,Kampuni ya uchimbaji Madini ya Geita (GGM) pamoja na wananchi mbalimbali.
Awali akizindua Mdahalo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina amesema kuwa lengo la kuendesha Mdahalo huo ni kutaka kupata mrejesho wa shughuli za Mahakama Kuu Geita tangu kuanzishwa kwake na hasa kujua mafanikio na changamoto ambazo zimejitokeza.
”Mahakama Kuu Kanda ya Geita tangu kuanzishwa kwake leo imetimiza mwaka mmoja, mwezi mmoja na siku ishirini na tisa, hivyo tukaona ni vyema tuandae mdahalo huu utakaohusisha wadau mbalimbali ili tuweze kupata mrejesho wa kile tunachokifanya na hasa mafanikio na changamoto zilizotokana na kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita,” amesema Mhe. Jaji Mhina.
Wakati huo huo Mhe.Jaji Mhina amesema kuwa,kabla ya kuanzishwa Mahakama hiyo, wananchi na wadau mbalimbali katika Mkoa wa Geita walikuwa wanapata huduma zao kutoka Mahahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, jambo ambalo katika hali ya kawaida lilikuwa linachelewesha upatikanaji wa haki kwa wakati lakini pia lilisababisha gharama kubwa sana kwa wananchi na wadau wetu kwa ujumla.
Vile vile Mhe.Jaji Mhina ameongeza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita ilianzishwa Mahsusi kwa lengo la kuwa Mahakama ya Mfano katika Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) kwa Mahakama ya Tanzania na mpaka sasa lengo la kuifanya iwe isiyotumia karatasi (Paperless Court )limefanikiwa kwa asilimia 100.
“Mpaka sasa Mahakama Kuu Kanda ya Geita , Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mahakama za wilaya zote za Mkoa wa Geita zimefanikiwa kwa asilimia 100 kutumia TEHAMA huku Mahakama za mwanzo Mkoa wa Geita zikifikia asilimia 80 na tunatarajia hadi kufikia tarehe 01 Machi,2025 Mahakama zetu zote za mwanzo nazo zitakuwa zimefikia asilimia100,” alisisitiza.
Sambamba na hilo, Mhe. Jaji Mhina ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita jumla ya mashauri 288 yalisajiliwa na mpaka sasa mashauri 264 yameshaamuliwa na maamuzi kupandishwa kwenye mfumo.
Aidha amesema kuwa matumizi ya TEHAMA katika Mkoa huo yamekuwa na faida kubwa sana ikiwa ni pamoja na kusaidia katika usimamizi wa utoaji haki,kusaidia maafisa wakaguzi katika kukagua mashauri kwenye mfumo, inapunguza gharama katika uendeshaji, inasaidia katika utunzaji wa majalada na upatikanaji wa taarifa,kurahisisha upatikanaji wa takwimu na pia inapunguza muda wakufanya kazi.
Katika kuthibitisha umuhimu wa matumizi ya TEHAMA Mkoani Geita, Mhe. Jaji Mhina amesema “Matumizi ya TEHAMA Mkoani kwetu yamesaidia katika Mahakama zetu za mwanzo 17 zilifunga mwaka 2024 na mashauri sifuri isipokuwa mahakama nne tu ambazo zilibakiza jumla ya mashauri 74,”.
Naye mwakilishi kutoka ofisi ya Mashitaka Mkoa wa Geita Bw. Godfrey Odupoy akichangia katika Mdahalo huo amesema kuwa, kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita kumesaidia sana katika kumalizika kwa mashauri kwa wakati kwa kuwa sasa mashauri yanamalizika wakati mwingine hata chini ya mwaka mmoja ikilinganishwa na hapo awali wakati Mahakama Kuu ikiwa Mwanza ambapo mashauri yalikuwa yanachukua muda mrefu pengine hata zaidi ya miaka mitatu.
“Kwetu sisi kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita kumekuwa msaada mkubwa sana kwa kuwa imetusaidia kupunguza gharama za safari na pia gharama za kulipa mashahidi kwa kuwa sasa tunalazimika kulipa pengine nauli kidogo tu kwa mashahidi wetu badala ya kulipa gharama za malazi kama ilivyokuwa hapo awali,” amesema Odupoy.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mawakili wa Kujitegemea, Wakili Erick Lutehanga amepongeza kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita kwani kumewasaidia kupunguza gharama kwao na kwa wateja wao.
”Kwetu sisi imepunguza gharama kwa kiasi kikubwa sana kwetu na kwa wateja wetu kwa kuwa tulilazimika kusafiri kutoka Geita hadi Mwanza na wateja wetu pia gharama za malazi zilikuwa kubwa sana kwetu, lakini sasa maisha yamerahisishwa,” amesema Wakili Lutehanga.
Akiendelea kuchangia katika Mdahalo huo, Wakili Lutehanga ameonesha wasiwasi wake juu ya namna ambavyo Mahakama itaweza kuendeleza kasi iliyoifikia katika matumizi ya TEHAMA kwa ujumla katika miaka ijayo na hata kuboresha zaidi.
Akihitimisha katika Mdahalo huo, Jaji Mhina amewatoa hofu wadau juu ya kuendeleza kasi hiyo iliyoanzishwa na kuwaahidi kuwa Mahakama katika Kanda hiyo imejipanga vyema ili kuendeleza viwango walivyofikia na pengine kwenda zaidi ya hapo.

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni