Na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma
Jumla ya maamuzi 60,348 yamepandinshwa katika Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania kwenye Mfumo wa Mtandao wa Mahakama ya Tanzania ujulikanao kwa jina la (TanzLii) ili kuwezesha wataalamu wa sekta ya sheria kufanya tafiti za kisheria na rejea.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania na Mkurugenzi wa Maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Mhe.Kifungu Mrisho Kariho jana tarehe 31 Januari, 2025 wakati akifungua mafunzo ya Tafiti za Kisheria ya Mtandao iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Dodoma.
“Huwezi kukwepa matumizi ya teknolojia kwenye masuala ya kisheria, kwani hivi sasa maamuzi yote tunayaweka kwenye mfumo wa Tanzlii na yanatumiwa kufanya rejea na wanafunzi wa sheria, wanasheria, mawakili na hata waandishi wa habari,” amesema Mhe. Kariho.
Kariho amesema kwamba Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania wanapomaliza vikao vya kuendesha mashauri maamuzi yao yanawekwa kila siku katika mfumo huo ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa za sheria na maamuzi hayo kwa kuwa ni taarifa za wazi kwa umma (public documents) na zinapatikana bure.
Ameongeza kuwa sasa hivi kunaLmabadiliko kwani wananchi walikuwa wanapata maamuzi hayo ndani ya siku 90 au 21 lakini sasa wanayapata ndani ya siku moja.
Kuhusu maamuzi hayo kupatikana kwa Lugha ya Kiswahili,ambayo inayotumiwa na Watanzania wengi amesema hivi sasa Mahakama inatumia Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri, ambao unawasaidia wananchi wengi kuyapata kwa lugha hiyo.
Aidha amefafanua kuwa mfumo huo unawezesha kufanya tafiti ili kuweza kufahamu Jaji aliyefanya maamuzi mengi, likiwemo suala kuchunguza ni kesi zinaongoza katika mkoa fulani kuliko mkoa mwingine, hivyo matumizi ya mfumo huo ni muhimu katika kupata taarifa.
Kwa upande wake mtoa mada mwingine katika mafunzo hayo, ambaye ni Meneja Mhariri wa AfricanLII, Bi. LindaAwuor amesema ni vizuri iunapofanya tafiti katika mfumo huo, kuzingati kitu unachotaka ili kuweza kuokoa muda kwa kuangalia yaliyomo na kufahamu mabadiliko ya sheria na sababu zipi zimesababisha mabadiliko hayo, huki ukizingztia kuainisha na nchi nyingine, kupitia AfricanLII.
Mafunzo hayo yamewashirikisha baadhi ya washiriki, ambao ni Majaji, Naibu Wasajili, Wasaidizi wa Sheria, Mawakili, Mahakimu, Tume ya Utumishi wa Mahakama,Magereza kutoka Dodoma na Singida.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania na Mkurugenzi wa Maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Mhe.Kifungu Mrisho Kariho akitoa maelezo ya kuingia kwenye mfumo huo.
Sekretarieti ikifuatilia.
(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni