Ijumaa, 31 Januari 2025

TUTOE SULUHISHO KWA WANANCHI WENYE CHANGAMOTO ZA KISHERIA; MASWI

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Chacha Maswi ametoa rai kwa wadau wanaoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria kutoa huduma stahiki na suluhisho kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali wanaofika kupata huduma katika Maonesho ya Wiki ya Sheria.

Mhe. Maswi ametoa rai hiyo leo tarehe 31 Januari, 2025 alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika Kifaifa kwenye Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

“Dhamira ya Serikali ni kwamba wananchi wapate huduma na kwa wakati, tujitahidi kutatua migogoro iishe tunatakiwa kutoa suluhisho, tumepewa nafasi hii si kwamba tuwepo tu, hapana bali tuamue, tufanye kazi kuisaidia Serikali yetu katika maamuzi kwa upande huu wa Sekta ya Sheria,” amesema Mhe. Maswi.

Mbali na hilo, Katibu Mkuu huyo ametoa wito pia kwa wananchi kuheshimu taratibu za kisheria zilizowekwa kwa manufaa ya nchi. 

Akizungumzia, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia amesema Wizara yake imefanikiwa kufikia wananchi kwenye Mikoa 17 sasa na matarajio yaliyopo ni kwamba mpaka kufikia mwezi Aprili mwaka huu, Mikoa yote itakuwa imefikiwa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Maswi ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kuandaa Maonesho hayo ambayo yana manufaa makubwa kwa wananchi ambapo pia amewakumbusha wananchi wanaopata elimu kupitia maonesho hayo kuwaelimisha pia wananchi ambao hawajabahatika kutembelea katika Maonesho hayo.

Mabanda aliyotemebelea Katibu Mkuu huyo ni pamoja na Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre), Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Wizara ya Katiba na Sheria na mengine.

Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 01 Januari, 2025 huku kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria kikitarajiwa kuwa tarehe 03 Februari, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Chacha Maswi (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria leo tarehe 31 Januari, 2025 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Chacha Maswi akipata maelezo kutoka kwa mabanda ya Wadau mbalimbali wa Mahakama wanaoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Chacha Maswi (kushoto) akipata maelezo alipotembelea banda la Wizara hiyo leo tarehe 31 Januari, 2025.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni