Jumapili, 26 Januari 2025

MAHAKAMA YA MWANZO WAZO HILL KUZINDULIWA KIPINDI CHA WIKI YA SHERIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill, ambayo ujenzi wake umekamilika hivi karibuni, itazinduliwa tarehe 31 Januari, 2025 kama sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2025 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi katika hafla ya uzinduzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jana tarehe 25 Januari, 2025.

 “Mahakama hii ambayo ilianza kufanya kazi tarehe 6 Januari, 2025 ipo Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo Hill, Tarafa ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni. Imelenga kuhudumia wakazi zaidi ya 312,394 kutoka Kata ya Wazo Hill, Mabwepande, Bunju na Mbezi ambazo zina Mitaa 19,” alisema.

Jaji Mfawidhi alitumia fursa hiyo kuwatangazia Wananchi wote wanaoishi katika Kata tajwa kiutumia Mahakama hiyo ili kupata huduma za kimahakama karibu na wanakoishi.

Alieleza kuwa kabla ya kujengwa kwa Mahakama hiyo, Wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za kimahakama katika Mahakama ya Mwanzo Kawe iliyopo katika maeneo ya Kawe.

Mhe. Maghimbi alibainisha kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo ni utekelezaji wa Dira ya Mahakama na Mpango Mkakati unaotekelezwa kupitia maboresho ya miundombinu ya Mahakama.

Akizungumzia utakelezaji wa Nguzo ya Pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama unaolenga kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na Wananchi, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam imewezeshwa kwa kufunguliwa na kuanza kazi kwa Mahakama ya Wilaya ya Ubungo iliyopo eneo la Kwembe na Mahakama ya Mwanzo Kwembe.

“Kabla ya uwepo wa Mahakama hizi, Wananchi walilazimika kufuata huduma za kimahakama katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mahakama ya Mwanzo Kimara,” alisema.

Aidha, Mhe. Maghimbi alieleza kuwa ujenzi unaendelea  wa majengo ya Mahakama mpya ya Wilaya ya Kibiti, Mahakama za Mwanzo Bunju, Msata, Kimanzichana, Mbagala na Gezaulole.

Uzinduzi wa maadhimisho hayo ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila. Mhe. Mapunda pia alipata nafasi ya kutembelea mabanda ambayo yameandaliwa na Mahakama na Wadau mbalimbali ambao wamejitokeza kutoa elimu ya sheria bure kwa Wananchi.

Mwonekano kwa nje wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Wazo Hill (juu na chini).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda akitembelea mabanda ya Mahakama la Kituo cha Huduma kwa Mteja. Picha chini akiwa katika banda la Wadau RITA katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda akiwa katika banda la TBS.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni