Na. LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama, Iringa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa,
imefungua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kuanza na matembezi yaliyoongozwa
na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, akiambatana na Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Ndunguru.
Matembezi hayo yalianzia katika Viwanja vya
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kupita mitaa ya Manispaa ya Iringa na kuishia
katika Viwanja vya Garden (Posta) vilivyopo katikati ya Manispaa ya Iringa
ambapo watumishi na Wadau walipata fursa ya kusikiliza hotuba kutoka kwa Viongozi
hao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Serukamba
aliwahimiza Wananchi wa Mkoa wa Iringa kuitumia vyema fursa hiyo ya uwepo wa Wiki
ya Sheria ambapo watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali watakuwa
wanatoa elimu ya sheria bure kwenye maeneo mbalimbali.
Baadhi ya maeneo hayo ni kwenye mashuleni, vyuoni,
maeneo yenye mkusanyiko wa watu na kutumia vipindi vya redio mbalimbali.
Naye Jaji Mfawidhi alieleza kuwa Mahakama kwa mwaka
2025 imejikita katika kuitafakari haki na ndiyo maana Kauli Mbiu ya maadhimisho
imekuwa na mwelekeo wa kutafakari haki madai katika kufikia malengo ya Dira ya
Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2050.
Mhe. Ndunguru alisisitiza kuwa msingi wa maendeleo
na ustawi wa jamii ni amani na hakuna amani pasipo haki.
Jaji Mfawidhi aliwashukuru Wadau wa Mahakama ambao
wanashiriki katika utoaji wa elimu kwenye maadhimisho hayo na pia
amewakaribisha Wananchi kushiriki Siku ya Sheria nchini ambayo itafanyika
Februari 3, 2025 katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa.
Katika ufunguzi huo, Viongozi mbalimbali wa
Mahakama na Serikali ya Mkoa wa Iringa walipata nafasi ya kutembelea mabanda
yaliyoandaliwa na kujionea namna Mahakama na Wadau walivyojipanga vyema katika
zoezi la utoaji elimu kwa wiki nzima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni