Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Bukoba imezindua Wiki ya Sheria mkoani Kagera kwa maandamano
yaliyoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba,
Mhe. Immaculata Banzi.
Maandamano hayo yalifanyika
jana tarehe 25 Januari, 2025 kuanzia Viwanja vya Jenerali Mayunga vilivyopo
Manispaa ya Bukoba kuelekea Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba, yakihusisha Viongozi
wa Mahakama, Wafanyakazi, Wadau wa Mahakama na Wananchi kwa ujumla.
Maandamano hayo
yalipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa. Baadaye, Jaji
Mfawidhi alimuongoza Mkuu wa Mkoa kutembelea mabanda yaliyoandaliwa na Mahakama
kwa kushirikiana na Wadau na kujionea namna washiriki walivyojipanga katika
zoezi la utoaji elimu.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi huo, Mhe. Banzi aliwaalika Wananchi wote
kufika Mahakama Kuu Bukoba na kutembelea mabanda ambayo yameandaliwa na
Mahakama pamoja na Wadau ili kupata elimu mbalimbali ya kisheria.
“Elimu
itakayotolewa katika Wiki ya Sheria ni pamoja na elimu juu ya taratibu za ufunguaji wa
mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, elimu ya
ndoa na talaka, taratibu za mashauri ya mirathi,
mashauri ya ardhi na mashauri ya kazi na elimu juu ya taratibu za za utatuzi wa
migogoro nje ya Mahakama na faida zake katika jamii,” alisema.
Alieleza
kuwa elimu pia itatolewa juu ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA ya Mahakama unaoshugulikia
mashauri; ikiwemo kufungua mashauri, kusikiliza, kutunza kumbukumbu za
mashauri, utoaji wa hukumu na usambazaji wa hukumu. Vilevile, kutakuwepo usikilizaji na utatuzi wa malalamiko.
Naye Mkuu
wa Mkoa wa Kagera aliipongeza Mahakama kwa Kauli Mbiu
ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ambayo ni: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia
Haki Madai Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
” Kama wengi wetu mnavyofahamu ili Nchi
iwe na maendeleo ni lazima kuwepo na mipango na malengo ya muda mrefu na muda
mfupi, na pia iwepo mikakati ya kufikia mipango na malengo hayo…
“Mipango na malengo hayo ndiyo yanatoa miongozi, sera na mikakati ambayo itaonesha taswira jinsi ambayo hatua ya maendeleo itakuwa imefikiwa na Nchi yetu kwa miaka takribani 25 ijayo. Hii ndio maana ya Dira ya Maendeleo ya Taifa. Umuhimu wa Dira ya Maendeleo ni kuiwezesha Nchi kuweka mipango na mifumo thabiti ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa,”alimesema Mhe. Mwasa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi akizungumza wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa
kuzindua Wiki ya Sheria.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa akihutubia Wananchi na Wadau wa Mahakama katika Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba.
Picha ya juu na chini Watumishi wa Mahakama na Wadau wa Mahakama wakiwa katika matembezi kuelekea katika Viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba kwenye hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa akikata
utepe kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Kagera.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni