Jumapili, 26 Januari 2025

UZINDUZI WIKI YA SHERIA MANYARA WAFANA

Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga jana tarehe 25 Januari, 2025 amewaongoza Wananchi na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Manyara kwenye hafla ya ufunguzi wa Maadhinmisho ya Wiki ya Sheria kimkoa iliyotanguliwa na matembezi maalum.

Akizungumza wakati wa kufungua maadhimisho hayo yaliyofanyika Standi ya zamani ya mabasi mjini Babati, Mhe. Sendiga aliwasisitiza wananchi wa Mkoa wa Manyara kutumia vyombo rasmi vilivyowekwa kwa ajili ya utatuzi wa migogoro na utoaji wa haki na siyo kutumia watu wanaojifanya kuwa wajuzi wa masuala ya kisheria ambao wanapotosha na kuwaingiza wananchi  katika matumizi makubwa ya fedha yasiyo ya lazima.

“Mkoa wa Manyara una watu wengi wanaojifanya kuwa wajuzi wa sheria na wengi wamekuwa wakiwalaghai wananchi na kuwapotosha, ifike wakati wananchi wa Manyara mbadilike na kutambua kuwa Mahakama ipo kwa ajili yenu hivyo itumieni  bila woga na siyo kuwatumia watu wasiostahili,” alisema Mhe. Sendiga.

Aidha, Mhe. Sendiga alibainisha kuwa, Mahakama imekuwa ikitoa kauli mbiu mbalimbali kila mwaka kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria ambayo kwa mwaka huu 2025 inasema, ‘Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’.

“Hatuwezi kuwa na malengo ya kimaendeleo ya muda mrefu ikiwa tuna Mahakama ambayo ina malengo yanayokinzana na dira yetu kama Taifa, lakini ninaipongeza sana Mahakama ya Tanzania kwa kuwa malengo yake yamewekwa wazi na yamejikita katika mabadiliko chanya ya utoaji haki kwa wakati na kwa kuweka msisitizo mkubwa wa matumizi ya TEHAMA jambo ambalo tunaona kuwa linaenda sambamba na Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo,” alisisitiza Mhe. Sendiga. 

Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama na wadau wake wako tayari kuwahudumia wakati wote wa maadhimisho hayo na hata baada ya hapo, kwani bado wanayo nafasi ya kufikisha kero, malalamiko na maoni yao kwenye madawati maalum ambayo yapo katika kila Mahakama.

“Tunawasisitiza sana wananchi muweze kuhudhuria maeneo mbalimbali ambayo tutakuwa kwa hii wiki yote, kwa sababu hiki ni kipindi ambacho wananchi wataweza kupata elimu mbalimbali kutoka kwa watumishi wa Mahakama na pia mtapata huduma mbalimbali kutoka kwa wadau wa Mahakama ambao tutakuwa tumeambatana nao katika kipindi hiki chote” alisema Mhe. Kahyoza.

Wiki ya Sheria kwa Mahakama Kanda ya Manyara imeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 25 Januari, 2025 kwa kutoa elimu sehemu za Mkoa wa Manyara, kwenye mabanda yaliyopo kwenye Viwanja vya Kituo cha zamani cha mabasi Babati, mashule, vyuoni, kwenye masoko na minada pamoja na vyombo vya habari kwa lengo la kufikisha elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga akihutubia wananchi na watumishi wa Mahakama (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria mjini Babati jana tarehe 25 Januari, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza akiwahakikishia wananchi uwepo wa huduma za kisheria zitakazo tolewa wiki ya sheria kwa mkoa wa Manyara na Wilaya zake.

Meza Kuu na Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Manyara wakiwa kwenye picha ya pamoja katika hafla ya ufunguzi wa Maadhinmisho ya Wiki ya Sheria iliyofanyika kimkoa mjini Babati.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Manyara wakiwa wanafuatilia hotuba za viongozi kwenye maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga (wa pili kulia) akiwa ameambatana na Majaji wa kanda hiyo wakiwa wanakagua mabanda ya washiriki wa maadhimisho hayo. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza.




Majaji wa Kanda  ya Manyara wakiwa kwenye matembezi ya uzinduzi wa wiki ya sheri. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni