Jumapili, 26 Januari 2025

YALIYOJIRI UZINDUZI WA WIKI YA SHERIA NCHINI KATIKA KANDA, MIKOA, WILAYA

Mahakama ya Tanzania jana tarehe 25 Januari, 2025 ilizindua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kufanya matembezi/mbio kuashiria uzinduzi wa Wiki hiyo.

Tukiangazia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani Mwandishi wetu EUNICE LUGIANA, anaeleza kuwa;

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Moses Magogwa ametoa rai kwa Watendaji wote wa Wilaya hiyo kuhamasisha wananchi kupata elimu katika Wiki ya Sheria

Mhe. Magogwa aliyasema hayo jana tarehe 25 Januari, 2025 alipokuwa akizindua Wiki ya Sheria katika viwanja vya kwa Mbonde mjini Kibaha, kwamba taarifa za wiki ya sheria zipelekwe kwa wananchi wote ili wananchi wote wapate elimu hiyo.

“Rai yangu na maelekezo yangu kwa Magavana mliopo hapa pelekeni taarifa rasmi kwa watendaji wa Kata, Mitaa na Wenyeviti wote na Vitongoji kuhakikisha tunatoa hamasa ya kutosha waweze kufika kwenye maeneo wakaweze kupata elimu na kutoa changamoto zote ili Mahakama iweze kupata mrejesho wa kutenda kazi vizuri sana,” amesema Mhe. Magogwa.

Ametoa rai pia kwa watumishi wote wa Mahakama kutenda haki kama ilivyo kauli mbiu ya Mahakama isemayo Uadilifu, Weledi na Uwajibikajiili ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, ameipongeza Mahakama kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kutoa maamuzi ndani ya muda mfupi ambapo pia ni sehemu ya malengo ya Dira ya Taifa ya 2050. 

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema Mahakama ya Tanzania imekuwa na utaratibu wa kutoa kauli mbiu kila mwaka ambayo inasadifu malengo ya Taifa la Tanzania ili kuhakikisha inatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa inafikiwa bila kikwazo chochote kutoka Mahakama, ambapo ameeleza kuwa, “kauli mbiu huendana na mipango ya Serikali inayoendelea au inayokusudiwa kutekelezwa kwa kipindi tarajiwa.”

Mhe. Mkhoi ameongeza kuwa, mwaka 2025 umekua mwaka wa pekee kwa nchi kwa kumaliza robo ya karne ya 21 iliyojikita katika matumizi ya Sayansi na Teknolojia na pia ni mwaka  ambao Tanzania inahitimisha  miaka 25 ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, huku Dira nyingine ya mwaka 2025 hadi 2050 ikiendelea kutayarishwa. 

“Hivyo ni muhimu Taasisi zote zinazosimamia haki madai kujua zimejipangaje katika kuhakikisha malengo makuu ya Dira ya Taifa yanafikiwa bila kikwazo chochote pia kuhakikisha kuwa haki madai zinatolewa kwa wakati ili kuepusha mchakato mrefu ambao unaweza kuwa kikwazo katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisema Mfawidhi huyo.

Alisema kauli mbiu hiyo ina lengo la kuzihamasisha Taasisi zinazosimamia haki madai kuhusu umuhimu wa kujiandaa vema ili kuepuka kuwa kikwazo cha ukwamishaji katika kufikia maendeleo ya Dira ya Taifa ya 2050.

Katika kufanikisha azma hiyoMahakama na wadau wote wanafanya kazi kwa pamoja kutoa elimu kwa umma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Gereza la Mkuza, Shule za Sekondari na Msingi, maeneo ya Masoko, Ofisi za Watendaji Kata na maeneo ya wazi pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha.

Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Moses Magogwa (kushoto)  akiongoza maandamano kuelekea viwanja vya kwa Mbonde ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi.

Watumishi wa Mahakama na wadau wakiandamana kuelekea kwenye viwanja vya kwa Mbonde ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.


Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Moses Magogwa  akitoa hotuba katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika viwanja vya kwa Mbonde Kibaha jana tarehe 25 Januari, 2025.
 
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria jana tarehe 25 Januari, 2025.


Meza kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama  Pwani.

Meza kuu katika picha ya pamoja na wadau wa Mahakama kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Kutoka Tabora Mwandishi wetu AMANI MTINANGI anaeleza kuwa;
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imefanya Matembezi ya Amani ya kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyoongozwa na Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha kuanzia Mahakama Kuu hadi katika viwanja vya TBC vilivyopo pembezoni mwa NSSF Mafao.

Matembezi hayo yalihudhuriwa na Majaji wa Mahakama Kuu, Viongozi wa Dini, Mahakama na Taasisi za mbalimbali za Umma, watumishi Mahakama, watumishi wa Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia, Wadau na Wananchi wa ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.

Akizungumza katika ufunguzi ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha kwa aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa kuelekea miaka 50 ya Dira ya Taifa ya Maendeleo na kuwahimiza wananchi kutumia wiki ya Sheria kujipatia elimu na msaada wa kisheria bure.

“Ninaipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi kubwa ya maboresho inayoyafanya kuelekea katika miaka 50 ya Dira ya Maendeleo ya Taifa, leo tunapozindua wiki ya sheria, ninawaasa wananchi wa Tabora kujitokeza kwa wingi katika viwanja hivi ili kujipatia elimu na msaada wa kisheria bure,” alisema Mhe. Chacha.

Akitoa neno la ukaribisho, katika hafla ya ufunguzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe.Dkt. Adam Juma Mambi, aliwahakikishia wananchi kupata huduma na msaada wa kisheria zilizosheheni weledi wakati wote wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Mhe. Dkt. Mambi alisema, “Ninawakushukuru watu wote mliojitokeza kushiriki katika maonesho ya Wiki Sheria Nchini katika viwanja hivi kwa muitikio wenu, ninawahakikishia kila mmoja atakudumiwa na timu ya wataalamu wa kada na Taasisi mbalimbali waliopo hapa kwa weledi kabisa.”

Naye, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Juma Kadilu aliwawashukuru Wakuu wa Taasisi, watumishi wa Mahakama na Taasisi mbalimbali, wananchi, wadau na waandishi wa habari kushiriki katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

“Ninawashukuru wakuu wa Taasisi, watumishi wa Mahakama na taasisi mbalimbali, wananchi, wadau na waandishi wa habari kushiriki katika uzinduzi wa wiki ya sheria, uwepo wenu tusingekuwa na sababu ya kukusanyika hapa,” alisema Jaji Kadilu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha (mwenye kofia katikati) akiongoza matembezi ya Wiki ya Sheria Mkoani Tabora.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini jana tarehe 25 Januari, 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha (mwenye kofia) akiendelea na zoezi la ukaguzi wa mabanda ya wadau katika viwanja vya TBC Tabora.

Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Mhe. Asnath Msacky akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa mabanda ya maonesho uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora (hayupo katika picha).

Kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mwandishi wetu AIDAN ROBERT anatujuza kuwa, 
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Mwenyeji wao Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, watumishi na wadau wameshiriki  matembezi ya ufunguzi wa wiki ya sheria mkoani humo. 

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria, Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye alisema  kuwa, Mahakama ya Tanzania ni sehemu ya Mhimili muhimu unaotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo nchini hivyo kupitia matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria, aliwataka wananchi kuisogelea Mahakama kupata huduma stahiki za kisheria kama ulivyo utamaduni wa kila mwaka wa Mahakama kuanza shughuli zake kwa kuhamasisha wananchi kupata huduma zake kwa karibu.

“Mahakama imefanya maboresho makubwa kupitia Mpango Mkakati wake wa 2020/2021-2024/2025, tumeona maboresho makubwa kwa upande wa majengo mazuri na ya kisasa kwa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mahakama Kuu, hivyo kabla ya maboresho haya, huduma za Mahakama Kuu zilifuatwa mkoani Tabora takribani kilomita 400 kuifikia huduma ya Mhakama Kuu ukitokea mkoani Kigoma," alisema Mhe. Andengenye.

Alisema kuwa, mwaka huu 2025 ni mwaka maalum wa kujipima kujua ni hatua zipi tumefika kama Taifa katika malengo tuliyojiwekea miaka 25 iliyopita lakini pia kuona uelekeo wa miaka mingine 25 inayokuja.

Aidha, aliongeza kuwa, Dira ya maendeleo ya mwaka 2000 mpaka 2025, ilidhamiria kukuza uchumi wa kipato cha kati, kupitia kilimo cha kisasa, mageuzi ya viwanda, ujenzi wa miundombinu na teknolojia ambayo mafanikio ya kuridhisha hususani katika kuboresha hali ya maisha ukuaji wa uchumi, utawala na ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa na uchumi katika kuleta maendeleo.

Alisema kuwa, mwaka 2020 Tanzania ilifikia hadhi ya chini ya kipato cha kati ikiwa kwa  pato la chini kwa mtu mmoja mmoja ni Tshs. 1,080/= na kuinua kiwango cha maisha kwa wananchi ambapo umasikini uliokithiri ulipungua, Sekta za Afya na Elimu, udumavu wa watoto wa chini ya miaka mitano umepungua, vifo vya wanawake wajawazito vimepungua, vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vimepungua na uandikishaji wa watoto shule za msingi na sekondari nao umeongezeka.

Akizungumzia msingi wa Dira Mpya ya mwaka 2050, alisema kuwa ni utawala, amani, usalama na utulivu na imejikita katika utawala wa kisheria na haki na kulinda haki za msingi na uhuru wa raia.

“Mahakama kama Mhimili mkuu wa haki  inalo jukumu la kusimamia utawala wa sheria na haki kwa mujibu wa Katiba, Mahakama imepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha haki inapatikana kwa usawa na kwa wote lakini pia kwa wakati, hivyo migogoro ikitatuliwa kwa wakati maendeleo huchomoza bali jukumu hili lisipofanywa kwa wakati hudumaza maendeleo," alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alisema, “nimefurahi kujumuika nanyi kigoma kwenye matembezi haya muhimu ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria kwani mimi ninapenda mazoezi."

Mhe. Dkt. Ndumbaro alibainisha kuwa, kitaaluma yeye ni Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea  namba 804 hivyo, Wiki ya  Sheria naye inamuhusu na kuongeza kuwa, "niko hapa pia kwa sababu mimi ndio naiwakilisha Mahakama na kusoma bajeti yake Bungeni na kuliomba Bunge kupitisha bajeti hiyo ya Mahakama, hivyo ni heshima kubwa leo kupata fursa hii nikiwa Kigoma.”  

Aidha, alieleza kuwa, ameifahamu Mahakama tangu mwaka 1998 akiwa Wakili wa Kujitegemea ambapo amekiri kuwa Mahakama ya nyakati hizo sio kama Mahakama ya sasa kwa kuwa kuna maboresho makubwa kuliko Mahakama yeyote hapa barani Afrika kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Waziri wa Sheria wa Morocco ambaye alithibitisha kuwa Mahakama ya Tanzania ni ya kwanza Afrika.

Akitoa neno la utangulizi, Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, amesema kuwa Mahakama imejipanga kuanza kazi kwa matembezi kuwaeleza wananchi kuhusu Kauli Mbiu ya mwaka huu isemayo; “Tanzania ya 2050: nafasi ya taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya Taifa ya maendeleo” ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi mwenye kuhitaji huduma ya Mahakama  anahudumiwa katika kiwango cha juu cha huduma za  Mahakama.

Washiriki wa matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Kigoma ni pamoja na watumishi wa Mahakama, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Polisi Tanzania, wananchi, Jeshi la Ulinzi na Usalama, Red Cross, FFU, Jeshi la Magereza, Takukuru, Uhamiaji, Tanganyika Jogging, Baraza la Ardhi na Nyumba, Baraza la Usuluhishi na Uamuzi, Huduma kwa Jamii, Damu Salama, Vodacom Tanzania, Benki ya Biashara, Chuo cha Western Tanganyika na Wanafunzi wa Shule za Sekondari.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akitoa hotuba ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa Mahakama Kanda ya Kigoma jana tarehe 25 Januari, 2025 katika viwanja vya Mwanga 'Community Center'- Kigoma.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mbunge) akitoa salamu za Wizara katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2025 mkoani Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa neno la utangulizi katika maadhimisho ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria iliyofanyika jana tarehe 25 Januari, 2025 katika viwanja vya Mwanga 'Community Center' mkoani Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria (wa kwanza kushoto) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, wa pili kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mbunge) na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye (wa pili kushoto), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mbunge), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile na (wa kwanza kulia ) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi kwa pamoja wakiwa wameshika bango lenye ujumbe wa wiki ya sheria nchini wakati wa matembezi ya ufunguzi wiki hiyo yaliyofanyika jana tarehe 25 Januari, 2025.


Sehemu ya Viongozi, Kamati ya Ulinzi na Usalama, 
Askari wa Jeshi la Polisi na wananchi wakiwa katika mazoezi mara baada ya kufika katika viwanja vya Mwanga 'Community Center' Kigoma ambapo ndipo maadhimisho hayo yalipofanyika.

(Habari hizi zimehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni