Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya
Watumishi
wa Mahakama, Wananchi wa jiji la Mbeya na Viunga vyake, Taasisi za Serikali na
zisizo za Serikali jana tarehe 25 Januari, 2025 wajitokeza kwa wingi katika
uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya
Kabwe stendi ya mabasi mkoani Mbeya.
Uzinduzi
huo ulitangaliawa na matembezi ya kilometa nne yaliyoanzia kwenye Viwanja vya Mahakama
Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya na kupita katika barabara mbalimbali za mitaa ya
jiji la Mbeya.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga aliielezea kauli mbiu ya
maadhimisho hayo kuwa ni, “Tanzania ya 2025: Nafasi ya taasisi
zinazosimamia haki katika katika kufikia malengo makuu ya dira ya taifa ya
maendeleo.”
“Maadhimisho
haya ya wiki sheria yanabebwa na Mahakama ikiwa ndiyo chombo mama katika
kusimamia sheria bila kuwasahau wadau ambao wanaisaidia Mahakama katika
kutimiza wajibu wake kisheria,” alisema Jaji Mfawidhi.
Vilevile,
Mhe. Tiganga alieleza kuwa, maadhimisho ya wiki ya sheria yanaenda sambamba na
utoaji wa elimu wa kisheria kutoka kwa Maafisa Mahakama na Wadau mbalimbali wa
sheria.
Maeneo
mbalimbali yatatembelewa kutoa elimu ya masuala ya kisheria yakiwemo mashule,
Vyuo Vikuu, Taasisi za umma na binafsi alikadhalika maeneo ya stendi ya mabasi ya
Mbalizi na Uyole jijini Mbeya kutakuwa na watoa elimu mbalimbali waliobobea
kwenye masuala ya kisheria na kutoa vipeperushi kwa wananchi kwa hiyo wananchi
msisite kufika kupata elimu hiyo, alisisitiza Mhe. Tiganga.
Kwa
upande wake, Mgeni rasmi wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Mhe. Juma Homera akitoa hotuba yake ya ufunguzi aliipongeza Mahakama Kuu, Kanda
ya Mbeya kwa kuendelea kutoa haki kwa wananchi na kuipongeza Mahakama Tanzania
kwa hatua waliyochukua ya kuendesha shughuli za kimahakama kwa mtandao, ambayo
inaenda sambamba na kauli mbiu ya taifa iliyozinduliwa mwaka 2024.
“Kauli
mbiu ya mwaka huu inaikumbusha Mahakama na wadau wa kusimamia sheria kutenda
haki kwa nafasi waliyonayo katika kufikia lengo la dira ya taifa 2050, suala la
haki na madai ni mtambuka haihusu Mahakama tu bali hata Taasisi za Serikali na
pia Taasisi binafsi na wadau wote,” alisema Mhe. Homera.
Naye,
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa
akihitimisha kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na mgeni rasmi kwa kufika kwake katika siku ya
uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria na kumwongoza kupita katika mabanda
mbalimbali ya Taasisi zilizojitokeza katika uzinduzi huo, wakiwemo TAWJA,
Kitengo cha TEHAMA Mahakama Kuu, Mbeya, Kitengo cha Masjala, Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Ofisi ya
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ofisi ya Mawakili wa Kujitengemea, NMB bank,
Yas Tanzania, Vodacom, Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama,
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali na Mtandao wa Waleta Mabadiliko Chanya Ulipo (LeMaChu).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni