Na Mayanga Someke – Mahakama, Sumbawanga
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakar A. Mrisha, ametoa rai kwa wananchi kutumia fursa ya wiki
ya sheria nchini kujipatia elimu ya sheria itakayotolewa.
Wiki
ya sheria imezinduliwa jana
tarehe 25 Januari, 2025
kwa matembezi yaliyoongozwa na Mhe. Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Peter
Lijualikali. Aidha,
kilele cha maadhimisho hayo
ya siku ya sheria nchini itafanyika
tarehe 03 Februari, 2025.
Akifafanua Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo Jaji Mrisha
alisema, kauli mbiu ya mwaka 2025
kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria
inasema, ‘Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika
Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’.
“Kauli mbiu hii inabeba ujumbe mkubwa juu
ya wajibu wa Mahakama na asasi mbalimbali zinazoshughulikia haki madai katika
kuhakisha wanafikia malengo ya Dira ya mpango wa maendeleo ya Tanzania ya Mwaka
2050’’alisema Mhe. Mrisha.
Aidha, Mhe. Mrisha aliongeza kuwa, Haki
madai ni mfumo ambao unahusika na usimamizi wa haki katika masuala ya madai.
Lengo kuu la haki madai ni kuhakikisha utolewaji haki kwa mujibu wa Ibara ya
107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika wiki hii ya
sheria, Mahakama pamoja na wadau wa sheria watahusika kutoa elimu kwa Wananchi
juu ya shughuli za utoaji haki kwa Wananchi. Pia ni nafasi kwetu Mahakama kupata
mrejesho wa kazi zetu kutokea kwa Wananchi kupitia maonesho ambayo yatadumu
hapa kwa muda wa wiki nzima. Nawasihi wananchi kutumia fursa hii kujipatia
elimu ya sheria itakayotolewa katika eneo hili,” alisema Kaimu Jaji Mfawidhi.
Naye, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Peter Lijualikali ameipongeza na kuishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua mbalimbali inayochukua kuboresha
huduma za utoaji haki nchini.
“Kwa
dhati kabisa, tunapongeza jitihada zinazofanyika katika kuboresha miundombinu
ya majengo ambayo inaziwezesha Mahakama katika Mkoa wetu kutoa haki katika
mazingira bora kabisa,” alisema Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo.
Vilevile, Mhe. Lijualikali aliipongeza
Mahakama kwa hatua ya hivi
karibuni iliyochukuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuajiri Mahakimu Wakazi wapya themanini na
wanane (88) ambao naamini kuwa wataongeza nguvu katika eneo la utoaji haki
nchini.
Mhe. Lijualikali aliongeza kuwa, anatambua ya kuwa katika
kuadhimisha ya wiki na siku
ya Sheria nchini kwa mwaka 2025 inaongozwa
na kauli mbiu isemayo; ‘Tanzania
2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu
ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’.
Aidha, Kaimu wa Mkoa huyo aliongeza kwamba, Kauli
Mbiu hiyo ndiyo itakuwa muongozo
wa Mahakama na Taasisi nyingine
zitakazoshiriki maadhimisho ya wiki ya sheria yatakayo endelea kwa wiki nzima na hatimaye siku ya kilele.
“Kwa uzoefu nilionao,
natambua ya kwamba, uzinduzi huu utaambatana na utoaji wa Elimu ya sheria katika sehemu mbalimbali kama vile
taasisi za elimu, vituo vya redio, stendi za mabasi, bajaji, bodaboda na dalala
na katika utoaji wa elimu hiyo naamini ya kwamba wananchi wote wakubwa kwa
wadogo, wanaume kwa wanawake watapata fursa ya kuelimishwa kinagaubaga juu ya
kauli mbiu ya mwaka huu lakini pia, wataweza kuuliza na kujibiwa maswali na
dukuduku walizokuwa nazo juu ya masuala ya
kisheria,” alisisitiza Mhe Lijualikali.
Akielezea umuhimu wa Kauli Mbiu hiyo Mhe. Lijualikali
alisema, kwa kutambua umuhimu wa wadau wa haki madai
katika kutoa haki kwa wakati, nipongeze Uongozi
wa Mahakama ya Tanzania kwa kutambua ya kuwa Serikali inajukumu moja tu la
kuendelea kufanya kazi katika nyanja zote ili kuendelea kukuza Uchumi wa nchi.
“Maadhimisho haya yanatoa
fursa kwa wananchi kutambua nafasi ya taasisi zinazosimamia haki madai nchini
katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Pia, wananchi
watatambua kuwa utoaji haki kwa wakati unawawezesha kutumia muda wake vizuri katika kujiletea
maendeleo yao na taifa kwa ujumla,”
aliongeza Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo.
Wito wangu kwa wananchi ni kuwa tutumie vizuri
Mahakama pamoja na wadau wengine wa haki madai katika kutatua migogoro mbalimbali
ili haki iweze kutolewa kwa wakati na wananchi waweze kutumia muda mwingi
katika uzalishaji mali ili kujiinua kimaisha.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Abubakar A. Mrisha akiwahutubia wananchi, watumishi na wadau mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya wiki ya sheria mjini Sumbawanga jana tarehe 25 Februari, 2025
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Peter Lijualikali akiwahutubia wananchi, watumishi na wadau mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya wiki ya sheria mjini Sumbawanga jana tarehe 25 Februari, 2025
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni