Mkuu wa Mkoa Mara apongeza Matumizi ya TEHAMA mahakamani
Watumishi wa Mahakama Musoma washiriki kutoa msaada kwa wahitaji kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria.
Na KANDANA LUCAS- Mahakama Musoma.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi ameshiriki uzinduzi wa Wiki ya Sheria Nchini mwaka 2025 katika Manispaa ya Musoma ambapo ameongoza matembezi yaliyohusisha, Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, wadau mbalimbali wa Mahakama na wananchi wa Manispaa ya Musoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, uliofanyika jana tarehe 25 Januari,2025 Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuadhimisha Wiki ya Sheria kwani inatoa fursa kwa wananchi kufahamu masuala mbalimbali ya kisheria. Pia ameipongeza Mahakama kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika usikilizwaji wa mashauri.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha mfumo wa kieletroniki wa usikilizwaji wa mashauri kwani unasaidia wananchi kuendelea na shughuli mahali walipo. Vilevile Maadhimisho haya yanatoa fursa adhimu kwa wananchi kufahamu masuala mbalimbali ya kimahakama na ya kisheria kwa ujumla”. Mhe. Mtambi alisema.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya ameeleza namna Mahakama inavyojitahidi kutatua migogoro kwa haraka na kwa njia ya usuluhishi ili kuwawezesha wananchi kutumia muda mchache mahakamani hivyo kujikita katika shughuli zao binafsi na za kiuchumi.
“Sasa hivi Mhe. mgeni rasmi, tumetilia mkazo kutatua migogoro mahakamani kwa njia ya usuluhishi. Ni njia inatumia muda mchache kumaliza migogoro kwa haraka ili wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania kwa ujumla wakafanye shughuli nyingine,”.alisema.
Uzinduzi wa Wiki ya Sheria mwaka 2025 kwa Mkoa wa Mara umefanyika katika Wilaya sita ambazo ni Musoma (Manispaa ya Musoma ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara), Wilaya ya Butiama, Bunda, Serengeti, Rorya na Tarime ambapo Wakuu wa Wilaya katika maeneo hayo wameweza kuongoza matembezi ya kuashiria uzinduzi.
Vilevile uzinduzi huo umeenda sambamba na kutembelea kituo cha watu wenye mahitaji maalumu kilichopo Manispaa ya Musoma kiitwacho Jipe Moyo Children Centre kwa lengo la kutoa msaada (tendo la huruma).
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni