Na INNOCENT KANSHA – Mahakama, Dodoma.
Utoaji
Elimu ya Sheria mtaani na maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko wa wananchi imezidi
kuwavutia wengi na kuacha gumzo kwa wananchi wakiwa wenye furaha na kusaidia kuongeza
uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria ikiwa ni jitihada ya Mahakama ya
Tanzania kujaribu kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha.
Katika
hatua hiyo Mahakama ya Tanzania na wadau wake wa utoaji haki leo tarehe 29
Januari, 2025 wametoa elimu hiyo katika maeneo ya Nane Nane standi ya Mabasi
yaendayo mikoani na Kituo kilichofuata ilikuwa ni Soko la SabaSaba jijini
Dodoma, shauku ya wananchi kutaka kujua taratibu za kisheria ilileta shangwe
kwa wananchi, hamasa na maswali mengi kuulizwa kwa maafisa mbalimbali
walioshiriki kutoa elimu hiyo.
Akizungumza
na wananchi kwa nyakati tofauti katika maeneo hayo akitoa elimu ya Mirathi,
Wasia, Ndao na masuala ya Talaka. Hakimu Mkazi Mhe. Sifa Jacob kwa ubobevu
mkubwa amesema, mashauri ya mirathi yamekuwa yakishuhudiwa kuwa na changamoto
kubwa katika jamii nyingi hapa nchini kutokana na uelewa mdogo wa wanajamii, kutawaliwa
na ubinafsi na kutotambua taratibu za kutatua changamoto za masahuri hiyo.
Akifafanua
taratibu za ufunguaji wa mashauri ya mirathi na uendeshaji wake mahakamani,
Mhe. Sifa Jacob amesema, ili mtu afungue mirathi sharti azingatie mambo kadhaa
ikiwemo kuwa na cheti cha kifo cha marehemu ili kuthibitisha kwamba, mali anayotaka
kuisimamia mmiliki wa mali hizo zinazodaiwa ni zake amefariki.
Aidha,
mfungua mirathi anatakiwa awe na muhutasari wa kikao cha ukoo uliokubaliana kwa
pamoja uteuzi wa mpeleka maombi mahakamani ya kuomba kuteuliwa kwake kuwa
msimamizi wa mirathi hiyo. Vilevile mtu hiyo atachukua nyaraka hizo ikiwa ni
pamoja na wosia kama marehemu atakuwa ameacha wosia wa maandishi au wa mdomo
utakao takiwa kuthibitisha mahakamani na mashahidi waliyoshudia maneno hayo ya
wosia yakitamkwa na marehemu.
Mhe.
Jacob akatanabaisha kuwa, jambo la msingi ni mwombaji kutambua kuwa ni Mahakama
gani angepende kwenda kuomba ateuliwe kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu. Kwani,
kwa kuzingatia mashauri hayo Mahakama za Mwanzo zote nchini zina mamlaka
kisheria kusikiliza mashauri hayo, lakini pia Mahakama za Wilaya au Mahakama
Kuu.
Mahakama
ya Mwanzo ina mamlaka pale ambapo sheria inayotumika kusimamia mirathi hiyo ni
sheria ya Kiislam au sheria ya kimila. Hivyo kama marehemu alikuwa inaonekana kuwa,
mirathi yake itasimamiwa kwa sheria ya kiisilam ama ya kimila mpeleka maombi ya
kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya maehemu atakwenda Mahakama ya mwanzo. Lakini
kama sivyo hivyo, basi mpeleka maombi ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ataenda
Mahakama ya Wilaya au Mahakama Kuu akiwa na nyaraka husika za kumsaidia
kufungua mirathi hiyo.
Mhe.
Jacob ameongeza kuwa, jambo lingine la msingi ni utaratibu wa mpeleka maombi
atakapo fika mahakamani. Mahakama itamuamuru atoe tangazo akiutaarifu umma
kwamba, mpeleka maombi ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi husika ameomba
usimamizi wa mirathi ya marehemu bini Fulani, kama kutakuwa na mtu mwenye
pigamizi juu ya mleta maombi basi pingamizi lake litasikilizwa na Mahakama na
kulitolea uamuzi.
Lakini
Mahakama ikilizika kwamba mleta maombi amekidhi vigezo vya kuteuliwa kuwa
msimamizi wa mirathi basi Mahakama itamteua mleta maombi na kumpatia barua na
nyaraka muhimu za kusimamia mirathi hiyo.
“Na
kama msimamizi huyo aliomba hati ya kutekeleza wosia basi Mahakama itatoa hati
ya kutekeleza wosia wa mali za marehemu ili kazi ya utekelezaji wa majukumu
hayo uanze,” amesema Hakimu Mkazi huyo.
Mhe.
Jacob ameongeza kuwa, baada ya kuteuliwa na Mahakama msimamizi wa mirathi ana
kazi zipatazo tatu hadi nne, mosi Msimamizi wa mirathi ndiyo mwakilishi wa
marehemu kwenye masuala yote ya kisheria na mali zake. Kwa hiyo ana wajibu wa
kukusanya mali zote za marehemu kokote ziliko, anamamlaka ya kushitaki na pia
mtu anayemdai marehemu anamamlaka ya kumshitaki msimamizi huyo wa mirathi.
Aidha,
Msimamizi wa mirathi anawajibu wa kukusanya mali zote za marehemu na kulipa
madeni yote yaliyothibitishwa aliyokuwa anadaiwa marehemu na kisha kugawa mali
za marehemu kwenda kwa warithi halali waliothibitishwa na vikao vya ukoo kwa
mujibu wa mali zilizoachwa na marehemu.
“Jambo
moja la msingi la kuzingatia ndugu wananchi ni kwamba msimamizi wa mirathi siyo
mmiliki wa mali za marehemu lakini pia msimamizi wa mirathi anateuliwa na
Mahakama na mchakato wote wa usimamizi wa mirathi unafanyika mahakamani hayo ni
mambo ya msingi ya kuzingatia na si vinginevyo,” ameongeza Mhe. Jacob.
Mhe.
Jacob amesema, kuteuliwa kwa msimamizi siyo kwamba mchakato unakuwa umekamilika
ni lazima msimamizi huyo akusanye mali alipe madeni na agawe mali hizo kwenda
kwa warithi halali na mwisho awahamishie mali hizo kwenda kwanye majina ya
warithi kwa maana ya majina yao mfano; kama marehemu ameacha nyumba inatakiwa
umiliki uhame na isomeke ni nyumba ya mrithi Fulani ama kama ni gari itafanyika
vivyo hiyo. Baada ya mchakato huo kukamilika Mahakama itafunga jarada hilo na
haita pokea malalamiko mengine kuhusiana na mirathi hiyo.
Kwa
upande wake, akitoa elimu kwa wananchi
ya `Zimamoto na Uokoaji, Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Konstebo
Jegu Dosela amesema, Jeshi hilo lina majukumu makuu mawili muhimu la kwanza ni
kuzima moto pale unapotokea lakini jukumu la pili ni kufanya Uokoaji.
“Lakini
ili mambo haya makuu mawili yafanyike kwa ukamilifu wake aidha, la kuzima moto
uliotokea kuna vitu vinavyofanywa ili kuhakikisha moto huo hauleti madhara
makubwa au hasara kubwa kwa wananchi. Kitu cha kwanza ni ukaguzi wa kinga na
tahadhali dhidi ya majanga ya moto na ukaguzi huo unapokuwa umefanyika basi mwananchi
atashauriwa kuweka vifaa ambavyo vitamsaidia mwananchi kukabiliana na tukio
hilo endapo litatokea,” amesema Konstebo huyo.
Konstabo
Dosela amesema, jukumu la tatu ni kutoa elimu ya majanga ya moto kwa wananchi
matahalani kutoa namba ya kupiga wakati wa dharura ya Jeshi la zimamoto na
uokoaji ambayo inapatikana muda wote pasipo changamoto na jeshi likipigiwa
litafika eneo husika kwa ajili ya kazi ya uokoaji ama kutoa huduma hiyo.
“Changamoto
inatokea mara nyingi mwananchi anapoona tukio la moto unatokea anaanza kuzima
mwenyewe na anapoona moto unamzidia ndipo anakumbuka kupiga namba 114 ya Jeshi
la zimamoto na uokoaji. Mwananchi
unashauriwa unapogundua kuna moto wakati jitihada za kuzima zikiendelea basi
taarifa itolewe kwa wakati na Jeshi litafika kwa wakati. Vinginevyo itabaki
kuwa lawama kama ambavyo zipo nyingi kwamba Jeshi linachelewa kila siku, lakini
ukitoa taarifa kwa wakati Jeshi litafika kwa wakati,” amesisitiza Konstebo
Dosela.
Majukumu
ya uokoaji yamegawanyika katika maeneo mengi mfano, ajali barabrani, kuokoa
watu waliozama kwenye maji, watu kudumbukia kwenye makalo ya vyoo mathalani
watoto kutupwa huko Jeshi linahusika moja kwa moja. Hayo majumu yote
yanatekelezwa na Jeshi la zimamoto na Uokoaji chini ya sheria ya sheria ya
Jeshi la zimamoto na uokoaji ya mwaka 2007.
Afande
Dosela akaelezea suala la usalama wa moto jikoni, hususani matumizi ya gesi
inapokuwa inatumika kwa matumizi ya nishati ya kupikia wananchi wanashauriwa
kuongeza umakini katika matumizi yake. Ili ikitokea mlipo wa gesi isiwadhuru
watumiaji na kupoteza mali na maisha.
“Gesi
inapokuwa imevuja ndani hakikisha mtungi unatoka nje ya nyumba na hakikisha
unafungua madirisha na milango ili ile gesi iweze kuisha ndani ya nyumba na
nyumba itakuwa salama, vinginevyo itakuwa kama mlipuko mkubwa ambao unaweza
kukusababishia ulemavu ama kifo ni tahadhali za kuzingatia,” amesema Aande
Dosela.
Hakimu Mkazi Mhe. Sifa Jacob (mwenye tisherti nyekundu) akitoa elimu ya Mirathi, Wasia, Ndao na masuala ya Talaka kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni