Na EVERINE ODEMBA – Mahakama Morogoro
Tangu kuzinduliwa kwa Wiki ya Sheria nchini tarehe 25 Januari, 2025, Wananchi wa Manispaa ya Morogoro wamejitokeza kwenye mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria ili kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama kwa kushirikiana na Wadau.
Miongozni mwa waliovutiwa na maonesho hayo na kufanya ziara ya kujifunza ni pamoja na Askari Jeshi toka Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe ambao walifika kwenye Banda la Mahakama wakiwa na kiu kubwa ya kujifunza namna ambavyo Mahakama inatekeleza majukumu yake.
Askari Jeshi hao wakiongozwa na Kepteni Seif Shunda walipokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo ambaye alishirikiana na wataalamu wa Mahakama na wadau kuwahudumia kwa maswali mbalimbali waliyowiwa kuyajua.
Mhe. Kallomo aliwapongeza askari hao na kuwaomba wakawe mabalozi wazuri wa Mahakama watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.
“Kwa niaaba ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro tumeshukuru sana kwa ujio wenu kuja kujifunza na tumefurahi kuwa katika neno lenu la shukurani mmebainisha maeneo mliyojifunza, ni imani yetu kuwa mtafikisha habari njema za Mahakama kila mtakapopata nafasi ya kufanya hivyo” alisema.
Naye Kapteni Seif Shunda aliyeongoza msafara huo alitoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa maonesho hayo ambayo yanawafikia Wananchi moja kwa moja na wao wamenufaika kupitia mada mbalimbali walizojifunza.
Miongoni mwa mada zilizotolewa kwa askari jeshi hao ni pamoja na masuala ya ndoa na talaka, mirathi, elimu ya sheria ya kodi toka TRA, Mawakili wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS) na Chama cha Mahakimu na Majaji Wanawake (TAWJA).
Mtaalamu toka Mahakama Kanda ya Morogoro, Mhe. Beatha Richard akitoa elimu kwa Askari Jeshi toka Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe waliofika kwenye Banda la Mahakama kupata elimu.
Kiongozi wa Msafara wa Askari Jeshi toka Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe, Kepteni Seif Shunda (aliyesimama aliyevaa koti jeupe) akizungumza na Mtaalamu toka Mahakama Kanda ya Morogoro Hakimu Mkazi Mhe. Renatus Barabara.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Renatus Barabara akiwaongoza Askari Jeshi kwenye mafunzo walipotembelea banda la maonesho la Mahakama.
Mhe. Mary Kallomo (aliyeketi katikati) akifuatilia mada mbalimbali.
Hakimu Mkazi Mhe. Shida Nganga akitoa elimu kuhusu Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania kwa Askari Jeshi hao.
Askari toka Jeshi la Wananchi Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe wakiinua mikono ili kupata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu sheria.
Sehemu ya mabanda ya maonesho ya kutolea elimu kwenye Wiki ya Sheria Kanda ya Morogoro.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni