Jumapili, 26 Januari 2025

WIKI YA SHERIA YAPAMBA MOTO, ARUSHA NA NJOMBE NAO WAZINDUA

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS) mkoani Arusha, Wakili Msomi George Njooka amezindua Wiki ya Sheria huku akitoa rai kwa wananchi kutumia fursa ya kutoa maoni juu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ili kuwa na Taifa lenye matokeo ya utashi wao. 

Bw. Njooka aliyasema hayo jana tarehe 25 Januari, 2025 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini  uliofanyika katika viwanja vya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)  mkoani Arusha.

Wakili huyo amesisitiza kuwa, Dira ya Taifa ya maendeleo inayomalizika mwaka huu imeleta mafanikio kadhaa ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki hususani katika Mahakama ya Tanzania hususani hatua kubwa iliyofikiwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa imewarahisishia wadau wa Mahakama kupata huduma.

“Unaingiza kesi mtandaoni, inapokelewa na kupangiwa tarehe ya kusikilizwa siku hiyohiyo, naipongeza Mahakama kwa hatua hiyo," amesema Wakili Njooka.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, Mgeni rasmi aliiomba Mahakama kuboresha mfumo wake wa kuratibu mashauri (e-CMS) ili kuwezesha upande unaoshtakiwa kuona maendeleo ya shauri kwenye mfumo husika, kama ilivyo kwa upande unaoshtaki au unaolalamika.

Aliongeza kuwa, Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, kwa mtazamo wake anaiona kuwa imemsahau mtoto wa kiume na kwamba mambo mengi ya kijinsia yanayopendekezwa yameegemea upande wa jinsia ya kike, hivyo, amewakumbusha wananchi kuendelea kutoa maoni yao ili kuwa na Tanzania yenye usawa wa kijinsia.

Vilevile, amesema kuwa zipo Taasisi za Haki Madai ambazo zina changamoto kubwa  zenye kusababisha ucheleweshaji wa haki kwa wananchi, ametaja Mabaraza ya Ardhi ambayo yanashindwa kutimiza wajibu wao kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi, hali inayochangia kuchelewesha  kusikiliza na kuamua mashauri yanayopelekwa na wananchi. Amesisitiza kuwa ni muhimu Serikali kuhakikisha kuwa inaweka mifumo madhubuti katika Taasisi zake ili kuwezesha uwepo wa amani na usalama na si kutengeneza matatizo katika jamii.

Akitoa maneno ya utangulizi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi alisema kuwa Serikali inakusudia kupanga mipango ya miaka 25 ijayo, hivyo inawashirikisha wananchi ili kupata maoni na vipaumbele vya kuzingatia katika kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo.

Uzinduzi wa Wiki ya Sheria ndio mwanzo wa juma la utoaji elimu kwa wananchi kuhusiana na mambo mbalimbali ya kisheria na kijamii ambapo wadau wanashirikiana na Mahakama katika utoaji wa elimu hiyo. Baadhi ya wadau hao ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili Wanawake Tanzania (TAWLA), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Magereza na Idara ya Huduma za Uangalizi. 

Taasisi na makundi mbalimbali kama Shule, Vyuo na wananchi watapatiwa elimu katika Wiki ya Sheria kupitia njia mbalimbali kama vile kutumia wasanii wa vichekesho (Zuri Comedy), redio, televisheni na kutembelea vituo husika.

Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini yana Kauli Mbiu isemayo; “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.” Kilele cha maadhimisho haya ya Sheria ni tarehe 03 Februari 2025.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS), Wakili Msomi George Njooka akizungumza na wananchi pamoja na wadau mbalimbali waliofika katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika jana  tarehe 25 Januari, 2025 katika Viwanja vya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria, Wakili Msomi George Njooka akikata utepe katika banda la maonesho la Mahakama kama ishara ya kuzindua Wiki ya Sheria tarehe 25 Januari, 2025. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta.


Wasanii wa kundi la 'Zuri Comedy' wakiburudisha wananchi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria tarehe 25 Januari, 2025 katika viwanja vya TBA jijini Arusha.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria jana tarehe 25 Januari, 2025 katika Viwanja vya TBA jijini humo.

Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania akizungumza na wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria Tanzania tarehe 25 Januari, 2025 katika viwanja vya TBA jijini Arusha.


Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika viwanja vya TBA wakisikiliza kwa makini hotuba za uzinduzi wa Wiki hiyo.

Mgeni rasmi, Wakili Msomi George Njooka akiwa katika banda la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) akipewa maelezo juu ya huduma zinazotolewa na Chuo hicho. Maonesho ya Wiki ya Sheria kwa upande wa Arusha yanafanyika katika viwanja vya TBA.


Wananchi na Wadau mbalimbali wakishiriki matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria jijini Arusha  tarehe 25 Januari, 2025 jijini Arusha.

Naye ABDALLAH SALUM wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe anaeleza kuwa,

Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Judika Omary ameongoza watumishi wa Mahakama Njombe pamoja na Wadau katika matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria, 2025.

Mhe. Judika alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe,Antony Mtaka katika matembezi hayo yaliyofanyika jana tarehe 25 Januari, 2025  yaliyoanzia katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Njombe hadi Stendi kubwa ya zamani ya Njombe mjini.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama alisema lengo la Wiki ya Sheria ni kutoa elimu ya kisheria kwenye majukwaa  mbalimbali, maeneo ya kata, Vijiji, Vyuoni na Shuleni ili kutoa uelewa wa sheria kwa wananchi na kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu Wiki ya Sheria, Mhe. Chamshama alisema, “Mahakama ya Tanzania inayo Mpango Mkakati wa 2020/2021-2025/2026 ambao kwa sasa unafikia mwisho, katika Mpango huo mkakati mojawapo ni kujenga imani ya mwananchi katika Mahakama kwa kuwashilikisha wananchi na wadau wa Mahakama” alisema Mfawidhi huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, naye Mhe. Judika aliwakaribisha wananchi kutembelea mabanda ya kutolea elimu, ambapo aliwaeleza kuwa, yapo mabanda mbalimbali na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi, pia wataweka banda la masuala yote ya ardhi na umiliki wa ardhi yatatolewa kwakuwa wananchi wengi hawajui kama hati zao zipo tayari hivyo aliwaomba wajitokeze ili waweze kupata hati miliki zao ili kujua mipaka yao ya ardhi kuepuka migogoro ya ardhi.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Njombe, Bw.Richard Mbambe aliwashukuru wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo na kuwakaribisha katika maonesho ya wiki ya sheria ili kupata elimu mbalimbali na kuwasihi kama wana malalamiko yoyote dhidi ya Mahakama wasisite kuyaleta katika banda la Mahakama.

Mtendaji wa Mahakama ,Bw.Richard Mbambe,aliweza kuwashukuru wananchi waliyojitokeza katika uzinduzi huo na kuweza kuwakalibisha katika wiki hii ya sheria kwa kupata elimu mbalimbali hasa za migogoro na kuwasihi wananchi kama wanamalalamiko yoyote dhidi ya Mahakama wasisite kuyaleta katika banda la Mahakama.

Maadhimisho ya wiki ya sheria nchini yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 31 Januari, 2025 huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni; ‘Tanzania Ya 2050-Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.’

Hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria Njombe ilihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Mkoa wa Njombe, Polisi, Magereza, Idara ya Maji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Damu Salama, Wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari za mkoani humo.

Matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Njombe, kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mhe,Judika Omary, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe akifuatiwa na Mhasibu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Juma Nyenzi.

Sehemu ya Mahakimu, Wadau wa Mahakama kutoka Taasisi mbalimbali pamoja na wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari za mkoani Njombe wakiwa kwenye matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria jana tarehe 25 Januari, 2025.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe,  Mhe,Liadi Chamshama akizungumza  na wananchi juu ya umuhimu wa Wiki ya Sheria nchini inayofanyika kila mwaka.  


                  
Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,  Mhe. Judika Omary (kushoto) akizungumza jambo na wananchi wa Mkoa wa Njombe (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria jana tarehe 25 Januari, 2025. Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Njombe, Mhe. Liadi Chamshama kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe.

Mgeni Rasmi Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Judika Omary (katikati) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liad Chamshama (aliyeketi kulia) na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe (aliyeketi kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mkoa, Wilaya na Mwanzo Njombe wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria tarehe 25 Januari, 2025.

 

 Wananchi pamoja na wadau wa Mahakama kutoka Taasisi mbalimbali wakiwa kwenye viwanja vya stendi ya zamani wakisikiliza hotuba fupi iliyokuwa ikitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama pamoja na Mgeni maalum, Mhe. Judika Omary Katibu Tawala Mkoa wa Njombe (hawapo katika picha).

(Habari hizi zimehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

  






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni