Ijumaa, 7 Februari 2025

AMIDI MAHAKAMA YA RUFANI AONGOZA KIKAO MAALUM

  • Majaji wajadili maandalizi usikilizaji mashauri 139
  • Mfumo wa kuratibu mashauri kuanza kutumika

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Amidi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija leo tarehe 7 Februari, 2025 ameongoza kikao kazi maalum kuangalia maandalizi yaliyofanyika ili kuhakikisha mashauri yaliyopangwa kwa muda wa wiki tatu zijazo yanasikilizwa bila vikwazo vyovyote.

Kwa mara ya kwanza, kikao hicho kimeendeshwa kwa njia ya mtandao kikiwaunganisha Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu katika Kanda na Divisheni, Naibu Wasajili, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji na Makarani ambao walikuwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika, kikao hicho kimewahusisha Wadau kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Magereza, Jeshi la Polisi, Chama cha Mawakili Tanganyika na wengine wengi.

Kikao hicho kimejadili mashauri 139 ambayo yatasikilizwa na majopo matano, yaani matatu yatakayoketi Dar-es-Salaam na mengine mawili ambayo yapo Makao Dodoma. Kesi nyingi za Dodoma zinahusu masuala ya kodi na biashara, huku za Dar es Salaam zikihusu ardhi na madai mengine.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mwarija amewaelekeza Mawakili wote watakaohusika kwenye usikilizaji wa mashauri hayo kufika mahakamani kwa tarehe walizopangiwa ili kusiwepo na sababu zozote zitakazokwamisha usikilizaji wa mashauri ambayo yamepangwa kwenye vikao hivyo.

Kadhalika, Jaji Mwarija amewataka wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania kujiandaa vizuri kwani, kwa mara ya kwanza, Majaji wa Mahakama ya Rufani wamejipanga kuanza kutumia kikamilifu Mfumo wa Kuratibu Mashauri kusikiliza mashauri hayo.

Akiwasilisha taarifa ya Msajili wa Mahakama ya Rufani kuhusu mashauri hayo, Naibu Msajili, Mhe. Dyness Lyimo amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa maandalizi yote yameshakamilika na sehemu kubwa ya wadaawa wameshajulishwa kuhusu vikao vitakavyoanza tarehe 10 hadi 28 Februari, 2025.

“Tupo tayari kwa usikilizaji wa mashauri yote ambayo yamepangwa baada ya maandalizi kukamilika,” Mhe. Lyimo amesema. 

Amidi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija akiongoza kikao kazi maalum kuangalia maandalizi yaliyofanyika kabla ya kuanza Vikao vya Mahakama ya Rufani kwa Dar es Salaam na Dodoma.


Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa kwenye kikao hicho.

Naibu Msajili, Mhe. Dyness Lyimo (juu na chini) akiwasilisha taarifa ya Msajili wa Mahakama ya Rufani kuhusu maandalizi ya usikilizaji wa mashauri kwenye Vikao vya Mahakama ya Rufani wiki mbili zijazo.




Sehemu ya wajumbe wa kikao (picha mbili juu na mbili chini) ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.



Sehemu ya taarifa ya mashauri hayo iliyowasilishwa kwenye kikao hicho. Picha chini ikionesha sehemu ya wajumbe waliokuwa wanafuatilia mkutano huo kwa njia ya mtandao.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni