Ijumaa, 7 Februari 2025

SIKU YA SHERIA NCHINI YAFANA MTWARA

Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara

Mahakama Kanda ya Mtwara, kama ilivyo maeneo mengine ya Tanzania, imeadhimisha Siku ya Sheria tarehe 3 Februari, 2025 ikiwa ni ishara ya kuanza mwaka mpya wa shughuli za kimahakama.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ally Ebrahim, huku Mgeni Mahususi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya.

Sherehe hizo zilianza kwa gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi ambapo mgeni rasmi alilikagua licha ya kuwepo changamoto ya mvua kubwa. Aidha, Wimbo wa Taifa ulifuatia kabla ya dua na sala kutoka kwa Viongozi wa Dini mbalimbali.

Katika maadhimisho hayo, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika, mgeni mahususi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mtwara walipata fursa ya kutoa hotuba zao zilizokuwa na ujumbe wenye umuhimu wa Siku ya Sheria nchini.

Katika hotuba yake, Mhe. Ebrahim alieleza kuwa Mahakama inaendelea kuboresha miundombinu ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na kusogeza huduma karibu na Wananchi.

Aliongeza kuwa Mahakama imerahisisha uendeshaji wa mashauri, kuanzia usajili hadi utoaji wa uamuzi kupitia mfumo wa kielektroniki (e-CMS) na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kama njia ya kuokoa gharama na muda wa Wananchi.

"Sisi kama Mahakama tunaendelea kuboresha miundombinu ili tuendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na Wananchi. Vile vile tumerahisisha namna uendeshaji mashauri kuanzia kufungua, kusikiliza na hata kutoa uamuzi,” alisema.

Katika salamu zake, Mhe. Mwaipaya aliipongeza Mahakama kwa juhudi zao za kuboresha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuondokana na mfumo wa makaratasi. Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa haki.

"Naipongeza sana Mahakama kwa juhudi zenu za kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuondokana na mfumo wa makaratasi ni jambo la kupongezwa, kwani litasaidia kuleta uwazi na ufanisi katika utoaji wa haki," aliongeza Mkuu wa Wilaya.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkoa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Nunu Mangu alieleza kuwa ofisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha ushauri wa kisheria unatolewa na kusaidia Taasisi mbalimbali zinazosimamia haki na kutunga sheria zenye maslahi kwa Serikali.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika alisema, “Tunatambua na kupongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Mahakama za ujenzi wa miundombinu pamoja na uwekezaji mkubwa katika teknolojia ili kurahisisha usimamizi, uendeshaji na usikilizwaji wa mashauri.”

Maandimisho hayo yalipambwa na shamrashamra za kwaya kutoka Kanisa Katoliki Mtwara zilizoburudisha nyoyo za Majaji na umati wa Wananchi, huku nyimbo zao nzuri zikielezea ujumbe unaoendana na Kauli Mbiu ya Siku ya Sheria ya mwaka 2025.

Ujumbe wao ulilenga kuhamasisha umuhimu wa sheria na haki katika jamii. Haikuishia hapo, kulikuwepo pia na burudani ya muziki wa kizazi kipya uliochezwa na wanachuo kutoka VETA Mtwara. Wanamuziki hao walionyesha vipaji vyao kwa lengo la kuhamasisha utoaji wa haki kwa kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji katika jamii.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim akihutubia hadhara ya Wananchi na Wadau wa Mahakama Siku ya Sheria nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdalah Mwaipaya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akizungumza katika maadhimisho hayo.

Mdau wa Mahakama,Wakili wa Serikali Mkoa wa Mtwara kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi.Nunu Mangu akitoa hotuba fupi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim akikagua gwaride lililoandaliwa na kikosi cha Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara. Pcha chini ni kikosi hicho baada ya ukaguzi,


Viongozi wa Dini na Wadau waliohudhuria sherehe hizo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni