Na Daniel Sichula-Mahakama, Mbeya
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Mbeya Mhe. Joachim Tiganga jana
tarehe 03 Februari, 2025 aliwaongoza wananchi na wadau wa tasnia ya sheria katika
kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini katika sherehe zilizofanyika viwanja
vya Mahakama Kuu Mbeya.
“Tunashukuru
katika maadhimisho haya ya wiki sheria tumeweza wafikia takribani ya wananchi
5000 kwa kuwasaidia na kutoa elimu ya sheria ana kwa ana, na wengine wengi
wamefikiwa kutoka kupitia vipindi vya radio mbalimbali jijini Mbeya”, alisema
Mhe. Tiganga.
Mhe.
Tiganga aliongeza kuwa, shughuli zote hizo zimefanikiwa kutokana na ushirikiano
mkubwa uliooneshwa kutoka kwa watumishi wa Mahakama wakiongozwa na Waheshimiwa
Majaji, Mahakimu, wadau mbalimbali wa sheria kutoka Taasisi tofauti za kiserikali
na zisizo za kiserikali kama vile Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea, Ofisi
ya mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Magereza na Ofisi ya Mwendesha
Mashtaka wa Serikali.
“Niwashukuru
wadau wote wa sheria kwa namna walivyojitokeza kwa wiki nzima na kutoa elimu ya
sheria na msaada wa kisheria kwa wananchi waliojitokeza katika mabanda ya
maonesho na vitu mbalimbali vilivyowekwa ili kufikisha huduma za kisheria
karibu na wananchi na wengine walifikiwa na elimu hiyo ya sheria kwa kupitia vipindi vya radio
mbalimbali zinazopatikana jijini Mbeya,” alisema Jaji Mfawidhi.
Aidha, Mhe. Tiganga alielezea kauli mbiu ya
maadhimisho ya siku ya sheria inayoenda sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya
maendeleo ya 2050 kuwa utoaji haki kwa wakati na kwa wote utasaidia kutatua
changamoto za migogoro ya haki madai na kusaidia kukuza maendeleo ya kiuchumi
na kuvutia wawekezaji.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Mbeya
kwa jitihada wanazofanya katika kusimamia na kutoa haki kwa wakazi wa Mbeya.
“Mhe
Jaji Mfawidhi na jopo lako la Majaji na Mahakimu napenda kutoa shukrani zangu
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mbeya kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya kwa kusimamia
sheria na kutenda haki, napenda kutoa wito kwa wanasiasa pale kunapokua na
migogoro kwa wananchi wenu mnaowaongoza muwape ushauri wa kwenda mahakamani
kwani wao ndiyo wanaweza kutatua migogoro hiyo kwa wakati,” alisema Mhe.
Malisa.
Wakati
huo huo, Mhe. Tiganga alipokea taarifa toka kwa wadau wa sheria Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) taarifa yao iliwasirishwa na Wakili Baraka Mbwilo
na ilijikita zaidi katika dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kugusia mambo ya
haki madai kwa ujumla na kuihamasisha Serikali na Mahakama kutilia mkazo suala
hilo kwani linagusa watu wengi.
Wakili
Mbwilo alisema kuwa, suala la ardhi katika dira ya 2050 ni la kulipa kipaumbele
ili mwananchi wa kawaida aweze kumiliki ardhi. Serikali inawajibika kuweka
mipango madhubuti katika upimaji wa ardhi na kuweka gharama ambazo mwananchi wa
kawaida anaweza kulipia na kuongeza idadi ya walipa kodi kwa ajili ya maendeleo
ya Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni