Na CHARLES NGUSA, Mahakama -Geita
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita jana tarehe 03 Februari, 2025 kama ilivyo kwa Mahakama nchi nzima imehitimisha Wiki na Siku ya Sheria katika viwanja vya maonesho vya EPZA iliyowashirikisha wadau mbalimbali.
Maadhimisho hayo yaliongozwa na mgeni rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina akiongozana na mgeni wa heshima ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Martin Shigela.
Pamoja nao walikuwepo pia wadau mbalimbali wa haki kama vile Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Jeshi la Polisi, Mawakili wa Kujitegemea watumishi wa Mahakama na wananchi waliohudhuria katika kilele hicho.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria, kivutio kikubwa mbele ya umati wa wananchi na wadau waliohudhuria ilikuwa ni kasi ya umalizaji wa mashauri katika Mahakama za Mkoa wa Geita. Ambapo awali wakati akiwasilisha hotuba yake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Mhina amesema kuwa Mahakama za Mkoa wa Geita kwa ujumla wake katika mwaka wa 2024 zilifungua mashauri 8,774 na kusikiliza na kuamua mashauri 8,270 ambayo ni sawa na asilimia 94 ya mashauri yote yaliyofunguliwa Mkoani huo.
Jaji Mhina alitoa pongezi kwa Mahakama za Mwanzo, ambapo Mahakama 17 za Mwanzo zilimaliza mwaka na mashauri sifuri.
“Nianze kwa kuwapongeza sana watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kwa ushirikiano wenu kwani katika Mahakama Mkoa wa Geita kwa ujumla wake , jumla ya mashauri 8,774yalifunguliwa na mashauri 8,270 yote yalisikilizwa na kuamuliwa ambapo Mahakama zetu za Mwanzo 19 zilimaliza mwaka na mashauri sifuri, haya ni mafanikio makubwa sana katika kuwahudumia wananchi na hasa katika harakati za utoaji haki kwa wakati,” amesema Mhe. Mhina.
Sambamba na hilo Mhe. Mhina amesema kuwa,historia ya kuadhimisha Wiki na Siku ya Sheria nchini ilianza tangu mwaka 1996 ambapo maadhimisho haya huadhimishwa mara tu baada ya Wahe.Majaji wanaporudi kutoka likizo na hii huashiria kuanza rasmi kwa mwaka wa kimahakama.
Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka wa Mkoa wa Geita, Bw. Castus Ndyamugoba akisoma hotuba kwa niaba ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, amesema kuwa ni vyema taasisi zote zinazosimamia haki jinai na haki madai zikajikita zaidi katika malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
Hivyo amesema ili kufikia malengo ya Dira hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapitia sheria zote ambazo haziendani na nayo ili ziweze kubadilishwa na kuendana na Mahitaji ya Sayansi na Teknolojia.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapitia sheria zote ambazo haziendani na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 na kuziondoa na kutunga mpya ambazo zitakuwa zimelenga kufika lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050,” Bw. Ndyamugoba amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Mkoani Geita Wakili Yisambi Siwale akiwasilisha hotuba kwa niaba ya chama chake, amesema kuwa ,ili kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, wao kama Mawakili wanapaswa kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu za msaada wa kisheria kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kisheria katika maeneo mbalimbali. ambapo sambamba na hilo pia ni wajibu wao kufanya utafiti na kushauri taasisi zinazohusika na utoaji haki na uandaaji wa sheria mbalimbali kufanya marekebisho ya sheria zinazonyima haki na utawala wa sheria.
Aidha Wakili Siwale amebainisha kuwa changamoto kubwa inayowakibili wao ni malipo kidogo wanayopata ikilinganishwa na kazi kubwa wanayofanya, ugumu na mlolongo mrefu katika utekelezaji na ukazaji wa hukumu za mashauri ya madai dhidi ya Serikali.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akizungumza wakati wa kuhitimisha maadhimisho hayo ameishukuru sana Mahakama Mkoa wa Geita kwani kasi ya umalizaji wa mashauri kwa kuwa imechangia kuondoa malalamiko ya wananchi yaliyokuwa yakielekezwa katika ofisi yake.
“Mwaka ulioisha sijapokea tena malalamiko yanayohusu huduma za Kimahakama, sanasana yalikuwa ni yale tu yanayohusu uelewa wa wananchi wa chchache ambao nao nilikuwa nikiwaelekeza kuja kwako na wanaeleweshwa na jambo linaisha, nawashukuruni,” amesema Mhe. Shigela.
Ameongoza kuwa upatikanaji wa haki madai unachagizwa zaidi na Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) na ndiyo maana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita zaidi katika kuboresha Miundombinu ya Majengo na TEHAMA kwa ujumla lengo kuu ikiwa ni kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akiwasilisha mada katika kilele cha Siku ya Sheria Mkoani Geita.

(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni